MWANAMKE MWELEDI: Licha ya dhoruba kali, hakutikisika
Na KEYB
MWAKA wa 2014 alituzwa na jarida la kibiashara la Forbes kama mwanamke shupavu wa mwaka katika sekta ya ujasiriamali eneo la Afrika, na hivyo kudhihirisha ubabe wake katika masuala ya kibiashara.
Kutana na Tabitha Karanja, mmiliki wa Keroche Breweries, mojawapo ya kampuni kuu za kutengeneza pombe katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Chini ya uongozi wake, Keroche Breweries imekua kutoka duka dogo la vyumba vitatu na wafanyakazi kadha, hadi kufikia sasa, kiwanda kikubwa chenye uwezo wa kuzalisha chupa 600,000 za mvinyo kila siku na kinachoajiri mamia ya wafanyakazi.
Na katika harakati hizo, amekuwa kigezo cha wanawake wengi wanaonuia kusimamia na hata kumiliki biashara kubwa.
Safari yake ya subira na bidii ilianza zaidi ya miongo miwili akiwa mwanamke wa kawaida kijijini. Japo alikuwa na ndoto ya wakati mmoja kuwa tajiri, hakudhania kwamba angeshindana na mashirika makubwa.
Hiyo ilikuwa miaka ya tisini, mumewe Joseph Karanja, alipofunga duka lake la bidhaa za ujenzi mjini Naivasha ili kujaribu bahati yake katika kutengeneza pombe.
Huku idadi ya wafanyakazi wake wakati huo ikiwa chini ya kumi, Bi Karanja alijitosa katika shughuli ya kuunda mvinyo.
“Alinishawishi kwamba mvinyo ulioimarishwa (fortified wine) ndio mbinu ya itakayotusaidia kumiliki biashara kubwa,” asema.
Lakini mambo hayakuwa rahisi.
“Tulikumbana na upinzani mkubwa katika kila pembe nchini,” aeleza.
Anakumbuka jinsi alivyolia huku watu wenye ushawishi mkubwa nje na ndani ya serikali walipomshambulia. “Hawakunichukulia kama mwanamke anayejitahidi kujiundia riziki.”
Kuna wakati baadhi ya wanasiasa waliongoza vita hivi na hata kuwaambia wananchi waziwazi kususia bidhaa zake walizoziita chang’aa. Huu ulikuwa mwanzo wa vita vikali huku mara kwa mara akishuku iwapo wangefua dafu.
“Mara nyingi safari hii ilikuwa ya upweke huku mimi na mume wangu tukipambana vikali na dhoruba hiyo,” aeleza huku akidokeza kwamba ni wakati huu ukakamavu wake ulijitokeza akilinganishwa na mumewe.
Anasimulia jinsi baadhi ya maafisa wakuu serikalini wangewatembelea na kuitisha hongo ya mabilioni ya pesa, suala lililowalazimu kufunga biashara wakati mmoja.
“Si mara moja nilisaka usaidizi wa mahakama ili kulinda kampuni hii kutokana na washindani waliokuwa wakitiwa hofu na biashara yetu,” asema.
Ni ukakamavu huu ambao umemtambulisha na kumshindia tuzo mbalimbali. Mwaka wa 2009 alipewa tuzo ya Moran of the Burning Spear. Huu ulikuwa mwanzo wa utambuzi kwa mfanyabiashara huyu kwani mwaka wa 2013 alikuwa mwanamke wa pili barani kuangaziwa na jarida la kibiashara la Ventures Africa magazine.
Mwaka huo huo, alipewa tuzo ya Golden Jubilee Award kutokana na ufanisi wake katika sekta ya uzalishaji.
Agosti 2016, Bi Karanja alikuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kutwaa tuzo ya ujasiriamali ya Entrepreneurial Excellence in Africa, baada ya Rais wa zamani Mwai Kibaki na mfanyabiashara Dkt Manu Chandaria. Desemba mwaka huo huo alipewa tuzo ya Global Inspirational Women Leadership Award.
Mbali na hayo, ameangaziwa katika majarida mbalimbali ambayo yamemtambua kama mmojawapo wa wafanyabiashara wakuu barani. Aidha, ametambuliwa miongoni mwa wanawake 13 shupavu barani Africa, miongoni mwao, Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda na Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf.
Lakini licha ya ufanisi wake, Bi Karanja amekuwa akitenga wakati kwa mumewe na wanawe wanne. “Mara nyingi chakula cha usiku kinaliwa pamoja huku siku za kuzaliwa pia zikiadhimishwa kama familia,” aeleza, akisisitiza kwamba famila yake ndio maafikio makuu maishani mwake.
“Tangu jadi nimekuwa nikikumbwa na wajibu mkuu wa kufanikiwa na kutoishusha familia yangu. Mara nyingi, walikuwa wakiniinua na kunihimiza,” asema.
Uhisani
Mbali na masuala ya kibiashara, Bi Karanja pia amekuwa mstari wa mbele katika uhisani.
Alianzisha wakfu wa Keroche Breweries Foundation kusaidia angaa watoto wanne werevu kutoka familia maskini kuendelea na masomo ya shule ya upili kila mwaka.
Pia, kampuni yake huendesha mpango wa kusambaza maji kwa jamii na kutoa mchango wa kifedha kwa miradi kama vile Naivasha Safe House, makao ya watoto waliodhulumiwa kutoka maeneo ya karibu.
Aidha, amekuwa mstari wa mbele kufadhili klabu za kandanda na michezo mingine ili kusaidia vijana kuwajibika. “Lazima nisisitize majukumu yanayotokana na biashara hii. Sharti nifuate sheria kali zinazoongoza biashara hii na kuwakumbusha Wakenya kila mara kunywa pombe kwa kuwajibika. Hii imekuwa kupitia kampeni ambazo hugharimu pesa nyingi,” asema.
Anawashauri wanawake wanaoendesha biashara kubwa kutopoteza matumaini.
“Hawapaswi kuogopa kushindana na wanaume ili kuendelea kuwa vigezo kwa wanawake wenzao,” asema.
Bi Karanja ambaye wakati mmoja alikuwa mkutubi katika idara ya serikali, anaangazia kusambaza bidhaa za kampuni ya Keroche katika sehemu zingine barani Afrika.