Makala

MWANAMKE MWELEDI: Mfinyanzi aliyepata shavu ulimwenguni

October 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEYB

AMEJIUNDIA jina katika sekta ya sanaa huku mchango wake ukitambulika sio tu humu nchini bali pia ng’ambo.

Kwa miaka, Magdalene Odundo amejiundia jina kama mwanasanaa stadi hasa katika ufinyanzi wa vyombo vya udongo kwa kutumia mikono, huku kazi zake zikichochewa haswa na sanaa ya kutoka mataifa kama vile China, Mexico, Ugiriki na mitindo ya Kirumi.

Yeye ni Profesa wa Ufinyanzi katika chuo cha University for the Creative Arts (awali Surrey Institute of Art and Design University College) eneo la Farnham, Uingereza, na aliwahi kufunza katika taasisi ya Commonwealth Institute jijini London miongoni mwa taasisi zingine nchini Amerika na Uingereza.

Kazi zake zimepokea utambuzi huku akipokea tuzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Officer of the Order of the British Empire (OBE) katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Malkia wa Uingereza mwaka wa 2008, na kuwa Mkenya pekee kuwahi kutambuliwa katika jukwaa hili.

Aidha, alipokea tuzo ya utambuzi kutoka taasisi ya Detroit Art Institute’s Friends of African and African-American Art. Hii ni kando na kuteuliwa kama mlinzi na mdhamini wa National Society for Education of Art & Design (NSEAD).

Aidha, kazi zake zimekuwa zikionyeshwa katika maonyesho mbalimbali tangu mwaka wa 1977. Kazi zake zimeshirikishwa katika maonyesho tofauti nchini Uingereza, Amerika, Uholanzi na Ujerumani.

Kando na hayo, amefunza katika taasisi mbalimbali za masomo ya juu katika sehemu tofauti duniani.

Pia ameshirikishwa kama mwandishi na mhusika wa machapisho kadhaa ikiwa ni pamoja na vitabu, makala kuhusu ufinyanzi wa vyombo vya udongo na ushairi.

Pia ameshirikishwa katika vipindi kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na Out of Africa, Magdalene Odundo and Ceramic Gestures: A Conversation with Magdalene Odundo.

Bi Odundo alizaliwa mwaka wa 1950, ambapo alisomea hapa Kenya na India. Maonyesho yake ya kwanza ya sanaa yalifanyika katika hafla ya African Heritage wakati wa kongamano la maadhimisho ya mwongo mmoja wa wanawake katika Umoja wa Mataifa (the United Nations Decade of Women’s Conference) jijini Nairobi, mwaka wa 1985.

Ana shahada ya digrii katika sanaa kutoka chuo cha sanaa na usanifu cha St Josephs College of Art and Design, vilevile shahada ya uzamili kutoka chuo cha Royal College of Art jijini London.

Nchini Uingereza, amejiundia jina kama mmojawapo wa wafinyanzi watajika ulimwenguni. Mwaka wa 1994, vyombo vyake vya udongo vilizoa Ksh21 milioni katika maonyesho ya mnada ya Sotheby’s Auction. Hapa nchini, kazi zake zimeonyeshwa katika Nairobi Heritage Gallery na African Heritage.

Mbali na ufinyanzi, Bi Odundo anatambulika kama mmojawapo ya walimu watajika wa sanaa nchini Uingereza.