MWANAMKE MWELEDI: Mtangazaji mahiri si hapa nyumbani tu!
Na KEYB
ATAKUMBUKWA kama kitambulisho cha Kenya katika shirika la habari la kimataifa la CNN ambapo alifanya kazi kama mtangazaji na mwanahabari.
Sasa Zain Verjee ni mmiliki wa kampuni ya Zain Verjee Group, inayorekodi video na habari kwa hadhari ya Afrika.
Bi Verjee alijitosa kwenye ulingo wa uanahabari humu nchini kama mtangazaji wa redio katika kituo cha Capital FM na baadaye kujiunga na kituo cha televisheni cha KTN ambapo alikuwa mtangazaji wa habari za jioni.
Ni akiwa hapa alipata fursa ya kujiunga na kituo cha CNN kama mtangazaji na mwanahabari.
Baadhi ya vipindi alivyochangia ni pamoja na World One, Inside Africa, Your World Today, World Report na The Situation Room.
Aidha, amehusika katika kipindi cha Third Opinion cha kituo cha kimataifa cha Uingereza cha BBC, mbali na kuhudumu kama mtangazaji huru wa vipindi vya kituo hicho hicho ikiwa ni pamoja na African Perspectives, baada ya mashambulizi ya kigaidi katika balozi za Amerika, Afrika Mashariki.
Baada ya kujiunga na kituo cha CNN mwaka wa 2000, Bi Vergee alipewa jukumu la kutangaza baadhi ya matukio ya haiba ya juu ikiwa ni pamoja na Kongamano la AGRA kati ya India-Pakistan, Maasi ya Mashariki ya Kati, harusi ya ufalme nchini Uingereza, michezo ya Olimpiki jijini London 2012, kesi ya aliyekuwa kiongozi wa Yugoslavia, Slobodan Milosevic, mashambulizi ya kigaidi ya 9/11, ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini mwaka wa 2007/8 na vita nchini Iraq.
Aidha, aliwahi kuwahoji baadhi ya viongozi wakuu katika ulingo wa kisiasa ikiwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Iran Mohammed Khatami, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, marehemu Benazir Bhutto na Rais wa zamani wa Amerika Bill Clinton.
Mbali na hayo, ni mwandishi wa Live & On The Air, kitabu cha watoto kuhusu msichana anayehamia jijini Nairobi kuwa mtangazaji. Pia, amehusika na kazi za uhisani kuhusu uhamasishaji wa virusi vya HIV/Aids, Hepatitis B na maradhi ya kupooza.
Bi Verjee ana shahada ya digrii ya Kiingereza kutoka Chuo Kikuu cha McGill nchini Canada, na pia ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha York University, pia nchini Canada.
Penzi lake katika masuala ya uandishi lilimsukuma kusomea shahada ya uzamili ya uandishi wa kifasihi katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.