Makala

MWANAMKE MWELEDI: Mtetezi mahiri wa haki za wanawake

March 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KEYB

ANAKUMBUKWA kutokana na mchango wake kama msimamizi wa zamani wa chama cha Maendeleo ya Wanawake, shirika ambalo tokea mwanzo lilinuiwa kuunganisha, kukuza na kuwapa wanawake nguvu za kijamii, kiuchumi na kisiasa ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo katika jamii.

Katika wadhifa wake, Zipporah Kittony alifanya kampeni za kupambana na ukeketaji miongoni mwa jamii za Ameru na Maasai, vile vile kupigania usawa wa kijinsia katika siasa, elimu ya mtoto msichana na lishe bora miongoni mwa wanawake.

Bi Kittony alibahatika kwenda shule nyakati ambapo wasichana wengi hawakupata fursa ya kusoma. Alisomea shule ya Kapsabet, kisha baadaye shule ya upili ya wasichana ya Kapropita.

Baada ya kumaliza masomo, alipokea mafunzo ya ualimu kati ya mwaka wa 1961 na 1962, ambapo baadaye alifanya kazi katika shirikisho la upangaji uzazi nchini – Family Planning Association of Kenya.

Mwaka wa 1970, pamoja na mumewe na wanawe walihamia jijini Nairobi ambapo aliajiriwa na shirika la World Assembly of Youth, mpango uliofunza vijana nidhamu na jinsi ya kujitegemea.

Alihudumu hapa kwa miaka sita huku kazi yake ikimlazimu kusafiri katika sehemu mbalimbali ulimwenguni – fursa iliyompanua mawazo.

Mwaka wa 1975, alihudhuria kongamano la kimataifa la vijana la Umoja wa Mataifa nchni Mexico.

Baadaye mwaka wa 1976, alihamia eneo la Kitale ambapo aliandikisha vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa shirika la Royal Agricultural Society.

Akihudumu katika wadhifa huu, Bi Kittony alilazimika kudhihirisha uwezo wake miongoni mwa wafanyakazi wenzake kwani mara nyingi alisutwa na kubaguliwa kwa msingi wa kijinsia. Alitumia sauti yake katika wadhifa huu kupigania haki za wanawake.

Katika miaka ya themanini, alijiunga na chama cha Maendeleo ya Wanawake. Alihudumu kwa miaka 13 kama mwenyekiti wa tawi la Trans Nzoia hadi alipotawazwa kuwa Mwenyekiti wa kitaifa wa shirika hilo mwaka wa 1996; wadhifa alioshikilia kwa miaka 11 ingine.

Alikuwa mmoja wa kikosi kilichoendesha kampeni za kuleta makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira (UNEP) hapa nchini Kenya.

Aidha, Bi Kittony alisaidia kuanzishwa kwa hospitali za akina mama kujifungua katika Pwani ya Kenya ikiwa ni pamoja na Kilifi, Malindi, Kwale na Taita, ambapo akina mama hawangeweza kufikia huduma hizi.

Alikuwa Seneta mteule huku akiwahi hudumu kama mbunge mteule katika Bunge la nane na pia naibu mwenyekiti wa Kamati kuhusu afya, fedha, biashara na bajeti katika bunge.

Amekuwa akifanya kampeni na kushawishi maamuzi huku akishirikiana na kampeni ya Beyond Zero iliyoanzishwa na mkewe Rais, Bi Margaret Kenyatta, kwa minajili ya kutoa huduma bora za kiafya ili kupunguza vifo vya watoto na akina mama wakati wa kujifungua.

Juhudi zake katika harakati za kuwagutusha wanawake zimetambuliwa nchini na kimataifa. Kwa mfano, mwaka wa 1999 alitambuliwa kama mwanamke wa mwaka na taasisi ya American Biographical Institute. Aidha, alipewa tuzo ya Order of the Grand Warrior (OGW) na The Moran of the Burning Spear (MBS).

Mwaka wa 2008, alipokea shahada ya heshima kutoka chuo kikuu cha United Graduate College University, nchini Amerika.

Mwaka wa 2009 alitambuliwa kama mjumbe a shirika la watu walio na matatizo ya kiakili.

Licha ya kustaafu kutoka siasa, Bi Kittony anaendelea kutoa ushauri kuhusiana na masuala ya kuwapa wanawake nguvu za kujitegemea huku akiwarai wanawake barubaru kujihusisha vilivyo na siasa. Anawaomba wanawake nchini Kenya kutia bidii ili kufanikisha usawa wa kijinsia vilivyo.