Makala

MWANAMKE MWELEDI: Mwanadiplomasia shupavu na msomi

June 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na KEYB

NI Waziri wa Mashauri ya Kigeni, wadhifa ambao anahudumu katika nafasi hiyo kutokana na utaalamu wake katika masuala ya amani na usalama.

Aidha, ustadi wake Dkt Monica Juma umezidi kuthibitisha kwamba anastahili nafasi hii kwani aliwahi kuhudumu kama Katibu Mkuu katika wizara za mashauri ya kigeni na ulinzi, vile vile kama balozi wa Kenya nchini Ethiopia na Djibouti, miongoni mwa nyadhifa zingine.

Akiwa angali mtoto, Bi Juma alikumbana na tamaduni tofauti nchini Kenya kwani wazazi wake walikuwa wakihamishwa kikazi katika sehemu mbalimbali. Alisomea shule za msingi na upili mijini Nairobi, Mombasa, Nakuru, Meru na eneo la Magharibi, na ni mfichuo huu ulionoa ari yake ya kutaka kuafikia mengi maishani.

Alipojiunga na chuo kikuu kufanya shahada yake ya digrii, alijua kwamba angeongeza maarifa kwa kusomea shahada ya uzamili na hata ya uzamifu.

Baada ya kuhitimu na shahada yake ya usimamizi katika serikali, baadhi ya wenzake waliamua kuwa wakuu wa tarafa (DO), ila yeye alikata kauli kufanya kazi katika afisi ya rais.

“Tulirejelea shughuli za kuweka miundo msingi mipya ambayo ingeimarisha utoaji huduma. Kwa mfano nilichangia katika uundaji wa bodi ya kitaifa ya kudhibiti viuawadudu,” asema.

Baada ya hapa, alirejea kuhudumu katika Chuo Kikuu cha Moi kama mhitimu msaidizi kutokana na kuwa wakati huo chuo hiki kilikuwa kipya na kilikumbwa na matatizo kama vile uhaba wa wafanyakazi.

Ni wakati huu mwaka wa 1991 ambapo serikali ya Rais Siad Barre wa Somalia ilipinduliwa. Katika harakati hizi, wakimbizi walianza kuingia nchini Kenya. “Kama wasomi tuliona haja ya kuunda kituo cha wakimbizi,” aeleza.

Haikuwa muda kabla ya Dkt Juma kuteuliwa kushiriki katika mafunzo ya masuala ya wakimbizi katika Chuo Kikuu cha Oxford, nchini Uingereza. “Baada ya masomo yangu nchini Uingereza, nilifanya kazi na kikosi kilichosaidia kuunda kituo cha mafunzo ya masuala ya wakimbizi katika Chuo Kikuu cha Moi,” aeleza.

Baadaye, walisaidia kuunda vituo vingine vya masomo kuhusu wakimbizi katika vyuo vikuu vya Dar es Salaam nchini Tanzania na Makerere nchini Uganda ambavyo bado vinaendelea na kushamiri.

Baadaye Bi Juma alirejea katika Chuo Kikuu cha Oxford kusomea shahada ya uzamifu katika masuala ya Falsafa kupitia ufadhili wa kimasomo. Katika harakati hizi alisafiri kwingi huku utafiti wake ukimpeleka nchini Uganda, Tanzania, Norway na Switzerland miongoni mwa mataifa mengine.

Baada ya kukamilisha masomo, alialikwa kujiunga na jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu amani na usalama wa kimataifa, wakati huo likijulikana kama International Peace Academy (IPA) na kisha baadaye International Peace Institute (IPI). Jopo hili liliundwa kutoa ushauri kuhusu masuala ya amani na usalama ambapo yeye hasa alihusika na mradi wa Afrika.

Kushuku uwezo

Mojawapo ya sababu zilizomfanya kujiunga na IPA ni kwamba wakati huo, mashirika mengi ya kutoa misaada yalikuwa yameanza kushuku uwezo wa bara la Afrika kujikwamua kutokana na changamoto ambazo zilikuwepo wakati huo.

Alipewa wajibu wa kuchunguza jinsi Hazina ya Ford ingehakikisha utoaji wa mikopo barani Afrika hasa kuzuia majanga. Kwa hivyo Dkt Juma alirejelea utafiti uliohusisha mataifa 18 ya Kusini mwa jangwa la Sahara.

Mradi huu ulisababisha kuanzishwa kwa shirika la TrustAfrica lenye makao yake jijini Dakar, Senegal ili kuongeza uwezo wa taasisi za Afrika kukabiliana na majanga.

Baadaye Dkt Juma alielekea nchini Afrika Kusini ambapo alifanya kazi katika shirika la Safer Africa kama mchanganuzi mkuu wa masuala ya kisiasa. Shirika hili lilichangia pakubwa katika kubadilishwa kwa Umoja wa Afrika (OAU) kuwa Muungano wa Afrika (AU) mwaka wa 2001. Baadaye alihudumu katika shirika la Africa Institute of South Africa (AISA) kama Mkurugenzi Mtendaji.

Hii ilifuatiwa na uteuzi wake kama balozi wa Kenya nchini Ethiopia na Djibouti, na mwakilishi wa kudumu katika shirika la AU, Shirika la maendeleo ya mataifa ya Afrika (IGAD) na Tume ya Umoja wa Kimataifa ya Afrika (UNECA).

“Nilifurahia sana kufanya kazi kama mwanadiplomasia kisha baadaye katika Jeshi la Kenya (KDF) ambapo tulienda nchini Somalia chini ya ‘Oparesheni Linda Nchi’.

Afisi yake ilitumika kama kigezo eneo hili katika masuala ya amani na usalama. Maafikio yao makuu yalikuwa ni pamoja na kuongoza Baraza la amani na usalama mara tatu, na uhusishaji wa KDF katika Jeshi la Muungano wa Afrika nchini Somali (AMISOM).

“Aidha, tulifanya mashauriano na kutia saini makubaliano na nchi ya Ethiopia ambapo Kenya ingepata megawati 4,400 za umeme kutoka taifa hili,” asema.

Dkt Juma alihudumu kama balozi kwa miaka mitatu unusu kabla ya uteuzi wake kama Katibu Mkuu katika Wizara ya Usalama, mwaka wa 2013.

Mbali na masuala ya kidiplomasia, Dkt Juma pia amekuwa akihusika pakubwa katika kazi ya uhisani. Hasa, yeye husaidia shule za upili anakotoka na alikofunza baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu.

Kama mke na mama wa mabinti wawili, anasema mumewe, Peter Kagwanja na familia yake kwa jumla wamemsaidia kufika alipo.