MWANAMKE MWELEDI: Ni daktari wa moyo mwenye ndoto kuu
Na KENYA YEARBOOK
JINA lake sio geni katika ulimwengu wa matibabu kwani yeye ni mmojawapo wa madaktari wa moyo wanaotambulika hapa Kenya.
Dkt Betty Muthoni Gikonyo alikuwa miongoni mwa madaktari wa kwanza kuwahi kufanya upasuaji wa moyo hapa nchini.
Pamoja na mumewe, ni waanzilishi wa The Karen Hospital na hazina ya The Heart-to-Heart Foundation inayohusishwa na miradi ya The Mater Heart Run na The Karen Hospital Heart Run, ambapo kwa pamoja imesaidia maelfu ya watoto kutoka familia maskini kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Mbali na hayo, yeye ni mwanzilishi wa chama cha wanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Nairobi.
Aidha, alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya usimamizi wa masuala ya afya Nairobi (Nairobi Health Management Board) kwa miaka saba, kati ya 2004 na 2011 na kuhudumu kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi kwa miaka saba.
Kwa Dkt Gikonyo, uamuzi wa kuwa daktari ulitochochewa na kakake aliyekuwa na mazoea ya kumhimiza na kummiminia sifa kwa sababu ya matokeo yake mazuri shuleni.
Kadhalika, anasema kwamba mumewe, ambaye walioana wakiwa bado wanafunzi, pia amekuwa nguzo kuu katika taaluma yake.
“Tulishauriana na kuhimizana katika masuala ya familia yetu na vipaji vyetu,” aeleza Dkt Gikonyo.
Lakini hii haikuwanasua kutokana na changamoto za kifedha na iliwalazimu kusawazisha baina ya familia, masomo na ajira kuafikia malengo yao.
Kadhalika safari ya Dkt Gikonyo haikuwa rahisi hasa alipokuwa akisomea shahada yake ya uzamifu.
Alipata pigo miezi kadha kabla ya kukamilisha masomo yake baada ya kukataliwa kwa tasnifu aliyokuwa akiishughulikia kwa miaka miwili kuhusu maradhi ya kuendesha miongoni mwa watoto.
Kushauriana
Kisa? Hakuwa ameshauriana na chuo kikuu kabla ya kutumia uchanganuzi kutoka kwa maabara huru nchini Uholanzi.
Hata hivyo huku akiwa amesalia na miezi mitatu pekee kabla ya kukamilisha masomo, Dkt Gikonyo alizama tena na kutafiti rekodi za matibabu za watoto wanaougua maradhi ya moyo katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta na baadaye kupita mtihani na kuhitimu kama daktari wa watoto.
Lakini bado alikuwa na tamaa ya kusomea ‘Neonatology’, sehemu ya tiba ya watoto inayohusisha kushughulikia watoto wachanga, hasa waliozaliwa mapema.
“Nilifahamu kwamba nilihitaji kuimarisha taaluma yangu. Nilijua kuna fursa nyingi hapa na nilifahamu kwamba ningezipata,” aeleza.
Tasnifu yake ya shahada ya uzamifu kuhusu maradhi ya moyo miongoni mwa watoto ilimsaidia kupata ufadhili kusomea tiba ya moyo hasa miongoni mwa watoto, katika Chuo Kikuu cha Minnesota, nchini Amerika.
Aidha pamoja na mumewe, walianzisha kliniki ya matibabu ya moyo wakiwa wanafanya kazi katika Nairobi hospital. Lakini licha ya ratiba yao kali ya kikazi, alihakikisha kwamba anaipa kipaumbele familia yake.
“Tulihakikisha kwamba tunawapa watoto wetu muda wa kutosha. Hakuna taaluma isiyomruhusu mtu kuwa na wanawe. Tangu wanangu wakiwa watoto, ilikuwa lazima niwe karibu nao,” aeleza.
Anakumbuka jinsi wakati mwingine mumewe alilazimika kushikilia zamu yake hospitalini na hata kujitolea kumpa siku zake za likizo ili awashughulikie watoto wao.
Mwaka wa 1993, walianzisha hazina ya Heart-to-Heart Foundation ili kuchanga pesa katika harakati za kurahisisha shughuli za upasuaji wa moyo wa watoto kutoka familia maskini. Huku wakiwa na imani na ujuzi wa matabibu nchini, walinunua vifaa vya kufanya upasuaji ili kuendesha shughuli hizo hapa nyumbani.
Mwezi Oktoba mwaka uo huo, Dkt Gikonyo pamoja na wenziwe walifanya upasuaji wa kwanza wa moyo nchini Kenya.
Ni ari hii iliyowapa moyo wa kuanzisha The Karen Hospital, hospitali ambayo imekuwa ikiendesha shughuli kwa zaidi ya mwongo mmoja huku ikitoa ajira kwa zaidi ya Wakenya 400 na kupokea hati ya mfumo wa kimataifa wa kudhibiti ubora- ISO.
Huo haukuwa mwisho wa ngoma kwa Dkt Gikonyo kwani baadaye aliendelea na masomo kwa kusomea shahada ya uzamifu katika usimamizi wa biashara.
Anasema kwamba kufumbia macho ukubwa wa mradi wa hospitali yao, kulichangia pakubwa ufanisi wake.
“Ukianza jambo, Mungu hawezi kukuruhusu kuona kila kitu kwa sababu ni kikubwa sana,” aeleza.
Mwaka wa 2013, wawili hawa walifungua chuo cha mafunzo ya utabibu kama awamu ya kwanza ya taasisi ya mafunzo Karen Hospital.
Bi Gikonyo ananuia kuhusika pakubwa katika kufunza kizazi kijacho cha wahudumu wa kiafya, kufikia kiwango cha chuo kikuu. Anaona hii kama sehemu ya suluhu ya matatizo ya huduma ya kiafya nchini, vile vile kama mbinu ya kukabili tatizo la wataalamu kuondoka nchini na kuajiriwa katika mataifa ya kigeni.
Amepokea tuzo kadhaa kutokana na mchango wake katika sekta ya matibabu ikiwa ni pamoja na Giants Federation of Kenya Award.
Pia yeye ni mshindi wa tuzo za The Silver Star of Kenya (SS) aliyopokea mwaka wa 1998 na Moran of the Burning Spear (MBS) aliopata mwaka wa 2008.
Mwaka wa 2016, Dkt Gikonyo alizindua tawasifu yake kwa jina The Girl Who Dared to Dream, kitabu kinachosimulia kwa undani safari yake udaktari.
Licha ya ufanisi huu wote, anasema safari bado inaendelea.
“Kuwa daktari ulikuwa ni msingi tu. Bado sijafika mwisho, lakini nakaribia,” asema.