• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
MWANAMKE MWELEDI: Ni gwiji wa mahusiano mema

MWANAMKE MWELEDI: Ni gwiji wa mahusiano mema

Na KENYA YEARBOOK

Novemba mwaka wa 2013, jarida la The New African lilimuorodhesha miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa barani Afrika.

Ni kitambulisho ambacho Gina Din-Kariuki amejiundia kupitia tajriba yake ya takriban miongo mitatu katika sekta ya mahusiano mema, kama mfanyakazi wa baadhi ya mashirika makuu, vilevile kupitia kampuni zake za Gina Din Group of Companies.

Mzawa wa Nanyuki, eneo la Mlima Kenya, Gina ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa shule za St Christopher School, eneo la Nanyuki na The Green Acres School-Limuru, hakubarikiwa sana katika masuala ya darasani.

Gina Din Kariuki (kulia). Picha/ Maktaba

Hata hivyo, alikuwa amepiga msasa kipaji chake cha uandishi kiasi kuwa akiwa na umri wa miaka 18 pekee tayari alikuwa anachangia kwenye mojawapo ya magazeti yanayotambulika nchini.

Hii ilikuwa kupitia makala yake ya ‘Talking Aloud‘, yaliyokuwa yakichapishwa kila Jumapili kwenye gazeti la Sunday Nation.

Aliandika makala haya kwa miaka minne kabla ya kuelekea nchini Uingereza alipojiunga na Chuo Kikuu cha London School of Journalism na kusomea Uanahabari.

Baadaye alirejea nchini na kupata ajira yake ya kwanza akiwa na miaka 21 pekee.

Alihusika pakubwa katika uzinduzi wa idara ya mahusiano mema katika Benki ya Barclays, idara ambayo kwa zaidi ya miaka 12 ilihusishwa naye.

Ni wakati huo alipojiundia jina na muunganisho mkuu katika sekta hii, suala lililomsukuma kuwazia kitambulisho chake haswa na mwaka wa 1996 akaamua kuanzisha kampuni yake ya Gina Din Corporate Communications Company.

Ujuzi wake katika ujasiriamali ulitoka kwa wazazi wake walioendesha biashara ya hoteli eneo la Nanyuki.

Gharama kubwa

Mwanzoni haikuwa rahisi kuendesha kampuni yake kutokana na gharama kubwa zinazohitajika kuanzisha biashara ya aina hii, huku akihitajika kulipa kodi ya afisi na mshahara wa wafanyakazi.

Lakini ni hali ambayo iliimarika miezi sita baadaye alipoanza kushuhudia ongezeko la wateja.

Pia, haikuwa rahisi hasa ikizingatiwa kwamba alilazimika kushindana na mashirika ya kimataifa ambayo yalikuwa yanatawala soko wakati huo.

Hata hivyo mkakati wake ulikuwa kudumisha utaalamu huku akijitosa katika fani hii akiwa ametawaliwa na penzi na hisia za kujitolea kutoa huduma ambazo huenda hazikupatikana katika mashirika haya.

“Baadhi ya changamoto zilikuwa kujaribiwa kwa imani na uaminifu wangu. Nilijifunza kusimama kidete na imani yangu kwamba Mungu ni Mkuu,” anasema Gina Din, akiongeza kwamba hilo limemwezesha kudumu katika biashara hii kwa muda huu wote.

Kulingana naye, katika biashara, ni muhimu kupokea usaidizi ambapo mara nyingi aliupata kupitia familia yake, vile vile ushauri na mwongozo kutoka kwa watu wengine.

Gina Din Kariuki. Picha/ Maktaba

Anamtaja hasa Bob Bard, Mkurugenzi Msimamizi wa zamani wa Benki ya Barclays kwa kumsaidia kukuza kipaji chake cha usimamizi.

Aidha, mumewe wa miaka 25, Chris Kariuki, amesalia kuwa nguzo muhimu hasa ikizingatiwa kwamba alimsaidia pakubwa kuanzisha biashara yake.

Pia, amehusisha pakubwa katika majukumu ya nyumbani na hasa kushughulikia watoto wao wawili. “Nikisafiri, mume wangu anahakikisha kwamba yuko nyumbani,” aeleza.

Aidha, anawataja dada zake kama nguzo kuu ya taaluma yake huku akiwatambua wazazi wake, ambao wote ni marehemu, kwa kukuza maadili ambayo yamekuwa mwongozo kwake.

Na licha ya ufanisi wake kama mjasiriamali, hajalegeza majukumu yake nyumbani. Mara nyingi amekuwa akilazimika kusawazisha muda ili kushughulikia majukumu yote.

“Kila mara nawapa wanangu nafasi ya kwanza. Nimewekeza muda mwingi kwao na nina uhusiano wa karibu nao,” aeleza.

Ufanisi wake haujakosa kutambuliwa kwani ameshinda tuzo mbalimbali.

Yeye ni mshindi wa tuzo ya Presidential Order of the Burning Spear, utambuzi aliopokea mwaka wa 2003 kutokana na mchango wake katika shughuli za ufadhili.

Pia, amewahi kupokea tuzo ya SABRE Award kutokana na mchango wake katika sekta ya mahusiano mema.

Mwaka wa 2017 alishinda tuzo ya Gold Stevier Award kutokana na mchango wake katika sekta ya matangazo ya kibiashara, mauzo na mahusiano mema, ushindi aliotwaa pia mwaka 2018.

Kando na masuala ya mahusiano mema, yeye ni mwanzilishi wa hazina ya Gina Din Foundation, inayowapa vijana fursa ya kuunda muunganisho na watu wenye ufanisi mkuu.

Aidha ni mjumbe wa heri njema wa shirika la kitaifa la Msalaba Mwekundu (KRCS), wadhifa ambao ameshikilia tokea Agosti 2008, ambapo kama wa kwanza kuteuliwa katika nafasi hii, ameratibu shughuli mbalimbali za uhisani.

Mwaka wa 2016, Hazina ya kutathmini idadi ya watu ya Umoja wa Mataifa – Kenya ilimteua kama mjumbe. Katika wadhifa huu, anafanya kazi ya kuhamasisha wanawake na wasichana kuhusu masuala kama vile kuangamiza visa vya ukeketaji, kuzuia ndoa za mapema, bali na kuimarisha afya.

Hii ni kando na kuwa ni mwanachama wa bodi za kampuni tofauti ikiwemo CAMAC Energy Kenya.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Dada ya mpenzi wangu ananipa umbea dhidi...

MWANAMUME KAMILI: Mfujaji jasho lake hana budi kujiandaa...

adminleo