MWANAMKE MWELEDI: Ni kidedea katika kikosi cha ulinzi
Na KEYB
YEYE ni miongoni mwa wanawake wachache ambao mchango wao katika kikosi cha jeshi nchini umehisiwa huku akihudumu katika nyanja hii kwa zaidi ya miongo mitatu.
Jina lake ni Fatumah Ahmed, Meja Jenerali wa kwanza wa kike kwenye kikosi cha ulinzi hapa Kenya.
Sio hayo tu, yeye pia ni brigedia wa kwanza wa kike katika jeshi la Kenya, na mwanamke wa kwanza kuteuliwa Kanali wa Brigedia.
Kando na hayo ni mwanamke wa kwanza kuteuliwa mkurugenzi msimamizi wa mradi wa bima ya afya ya wanajeshi (DEFMIS).
Bi Ahmed ambaye alikuwa mwanafunzi wa zamani The Aga Khan High School, alijiunga na jeshi la Kenya mwaka wa 1983 baada ya kukamilisha masomo ya shule ya upili.
Alihudumu chini ya kikao cha huduma ya wanawake (Women’s Service Corps) ambapo mamlaka yake yalikuwa kusaidia vikosi vya vita hasa katika majukumu ya usimamizi, vile vile kutoa fursa za nafasi za kazi kwa wanawake katika tasnia inayotawaliwa na wanaume.
Huduma hii ya wanawake ilipovunjwa mwaka wa 1999, wanachama wake walihamishwa katika vikosi vitatu, ambapo Ahmed alipelekwa katika jeshi la wanahewa na kuhudumu katika idara ya kushughulikia maslahi ya wafanyakazi ya kikosi cha wanahewa.
Safari yake katika nyanja hii iling’aa zaidi Agosti 2015 alipopandishwa cheo hadi Kanali wa Brigedia, na hivyo kuandikisha vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo.
Huo tu ulikuwa mwanzo wa ufanisi wake kwani taa yake ilizidi kung’aa Julai mwaka jana, alipoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa Meja Jenerali.
Isitoshe, pia amewahi hudumu katika idara ya usimamizi wa shughuli za kudumisha amani za Umoja wa Mataifa ambapo alikuwa afisa wa mafunzo. Mwaka wa 2001, alihudumu katika kikosi cha kudumisha amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Bi Ahmed ambaye ni mhitimu wa chuo cha ulinzi nchini (National Defense College) na chuo cha mafunzo ya kijeshi (Kenya Military Academy), amehudumu katika kikosi cha jeshi la Kenya kwa zaidi ya miaka 30 katika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Afisa wa wafanyakazi (Staff Officer II Audit Personnel Records), amiri wa pili wa kikosi (BN 21C), Kanali wa utumishi katika makao makuu ya Jeshi la wanahewa, na afisa wa utumishi wa wafanyakazi na usimamizi.
Bi Ahmed ni mama wa watoto wawili, na mkewe Meja Jenerali George Owino ambaye ni Kamanda wa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Kenya.