MWANAMKE MWELEDI: Ni nahodha wa kwanza wa kike wa meli nchini
Na KEYB
ALITUPILIA mbali ofa ya ufadhili wa kusomea sheria kwa sababu nia yake ilikuwa kujihusisha na jambo lisilo la kawaida.
Na bila shaka alifanikiwa kufanya hivyo kwani Elizabeth Marami, al-maarufu Liz Marami ndiye nahodha wa kwanza wa kike wa meli (marine pilot) sio tu humu nchini bali Afrika Mashariki yote.
Utaalamu huu unatokana na mafunzo ya teknolojia ya ubaharia aliyopokea katika chuo cha mafunzo ya unahodha nchini Misri ambapo alikuwa mwanafunzi pekee wa kike kujiunga na kozi hiyo mwaka huo.
Kwa sasa anafanya kazi katika Halmashauri ya kusimamia bandari nchini (KPA) ambapo pia anasimamia kamati ya unasihi wa wanawake katika nyanja ya ubaharia eneo la Afrika Mashariki na Kusini (Womesa).
Kazi yake inahusisha kuongoza meli za kigeni kuingia na kuondoka kwenye bahari kuu ya Kenya.
“Kwa kawaida mimi huelekea kwenye bahari kuu nikiwa nimeandamana na rubani mkuu ambapo chini ya amri yake, natarajiwa kuongoza meli za kigeni kuingia na kuondoka kwenye bahari ya Kenya. Kisheria, meli za kigeni zinapowasili au kuondoka katika bandari ya Mombasa zinapaswa kuongozwa na nahodha Mkenya,” aeleza.
Ni kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu ambapo kila mara anajitahidi kuhakikisha kuwa kila kitu kimeenda kuambatana na mipango.
Mwaka wa 2015 alitambuliwa na gazeti la Business Daily kama mmojawapo wa wanawake chini ya umri wa miaka 40 wenye ushawishi mkubwa nchini na waliofanikiwa katika taaluma mbalimbali.
Mzaliwa wa Mombasa, Bi Marami amesomea shahada ya sayansi katika teknolojia ya ubaharia ambapo ana leseni ya afisa wa pili.
Ndoto yake ilianza akiwa mdogo lakini hakuwa na wazo kuwa angejipata katika fani hii. “Maishani mwangu nilijua kuwa nilitaka kuwa tofauti na wenzangu wa kike,” aeleza.
Anasema kuwa tamaa yake ya kutaka kutimiza ndoto yake ndiyo iliyomsukuma kuingia katika ubaharia pasipo kuzingatia mipaka ya kijinsia. “Lakini pia nilipata msukumo kutoka kwa wanawake wengine waliokuwa na ushawishi katika jamii,” aeleza.
Kulingana naye, mojawapo ya changamoto ni kudhihirisha kuwa anaweza kazi hii kama wafanyakazi wenzake wa kiume hasa ikizingatiwa kuwa yeye ndiye mwanamke pekee hapo.
“Kadhalika kuna wakati ambapo nakumbana na marubani wa kigeni ambao bado wanatawaliwa na kasumba ya kiume ambao wana tashwishi na uwezo wangu. Lakini nimekuwa nikipata usaidizi mwingi kutoka kwa wafanyakazi wenzangu na pia kutoka kwa jamaa zangu,” aeleza.
Mbali na hayo Bi Marami ameanzisha mradi kwa jina ‘Against the Tide’ ili kupigania usawa wa kijinsia katika taaluma za ubaharia. Wazo la kuanzisha mradi huu limechochewa na ugumu aliokumbana nao alipokuwa akitafuta ajira.
Kinyume na wenzake wa kiume waliopata ajira upesi, kwa upande wake alikumbana na changamoto mara kadha kwa sababu anaamini kwamba baadhi ya mashirika ya ubaharia yanaogopa kuajiri wanawake ili kujiepusha kukabiliana na visa vya dhuluma za kimapenzi.
Aidha kama nahodha na mnasihi wa kike, Bi Marami anafurahia fashoni na ana blogu anayoangazia masuala ya fashoni. Tangu utotoni alifurahishwa na wanawake waliovalia nadhifu wakienda kazini. Alikuwa anatamani siku ambapo angeajiriwa na kupata mshahara ili pia aweze kujinunulia mavazi kama hayo.
Kinaya ni kwamba kazi alionayo kwa sasa anahitajika kuvalia unifomu na hivyo yeye hutumia blogu yake kuonyesha ubunifu wake katika fashoni.
Marami aidha ni mjumbe wa kampeni ya ‘Stand up Campaign’, ya visodo vya Always na kwa pamoja na nahodha wa timu ya taifa ya basketiboli Silalei Owuor wanahusika kwenye kampeni ya ‘Keeping Girls in schools.
Mawaidha yake kwa wasichana wanaotamani kufanya kazi hii ni kufuata ndoto zao.
“Kwa kawaida ni dhana za kijamii zinazowafanya wasichana kufikiria kuwa kuna taaluma zingine zisizowafaa. Lakini uwe mwanamke au hata mwanamume, unapaswa kugundua kuwa mradi unajiamini, basi hakuna kitu ambacho kinaweza kukushinda kutekeleza,” ashauri.