MWANAMKE MWELEDI: Profesa Julia Ojiambo, gwiji aliyepasua anga
Na KENYA YEARBOOK
ITAKUWA vigumu kutaja wanawake wenye ufanisi mkubwa kielimu, kitaaluma na kisiasa nchini pasipo kuorodhesha jina lake miongoni mwao.
Yeye ni Profesa Julia Ojiambo.
Kando na kuwa mwanamke wa kwanza kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi, pia alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka Bara Afrika kusomea Chuo Kikuu cha Harvard nchini Amerika.
Pia, alikuwa mhadhiri wa kwanza wa kike katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Isitoshe, alikuwa mwanamke wa kwanza mwenye Shahada ya Uzamifu katika chuo kikuu hicho.
Alisaidia kuzindua mafunzo ya shahada ya masuala ya lishe katika Chuo Kikuu cha Kenyatta University College ambapo wakati huo kilikuwa chuo tanzu cha Chuo Kikuu cha Nairobi.
Yeye pia alikuwa miongoni mwa wasichana wanane wa kwanza wa Shule ya Upili ya African Girls High School ambayo kwa sasa inafahamika kama Alliance Girls High School.
Aidha, Prof Ojiambo alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka jamii ya Waluhya kuwa mbunge na wa kwanza kuteuliwa kama waziri msaidizi katika utawala wa Hayati Mzee Jomo Kenyatta, wakati huo akiwa na umri wa miaka 38 pekee.
“Haikuwa rahisi. Mojawapo ya tatizo nililokumbana nalo kila wakati lilikuwa kukataliwa kwa ajenda za wanawake,” afichua.
Atakumbukwa kwamba kama mbunge mteule aliyevunja rekodi kwa kuwasilisha miswada mingi zaidi mbele ya bunge.
Hizi ni baadhi ya sifa zinazojumuisha tawasifu ya Prof Ojiambo, suala ambalo limemfanya kutambuliwa nchini na mbali.
Penzi lake katika masomo lilianza akiwa mchanga ambapo wakati mwingi angeandika kwenye udongo au kutumia makaa ukutani. Ni werevu uliomfanya kuvuka madarasa mawili akiwa katika shule ya msingi.
“Katika familia yetu tulikuwa tunapanda pamba ili kupata pesa za karo, na hivyo nikiwa na umri wa miaka mitano pekee tayari nilikuwa nimeanza kulima,” asimulia.
Aliolewa na Bw Hillary Ojiambo mwaka wa 1961, na kuungana naye mjini Kampala, Uganda, ambapo alikuwa anafanya kazi kama msajili wa kimatibabu katika hospitali ya Mulago.
Kwa upande wake, yeye alikuwa akihudumu kama meneja wa nyumba za wageni wa Chuo Kikuu cha Makerere, huku pia akiwa mtafiti msaidizi katika hospitali hiyo.
Wakati huo maradhi ya Kwashiorkor na marasmus yalikuwa yamekithiri katika eneo la Afrika Mashariki na kusababisha vifo vingi miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano.
Prof Ojiambo aliungana na madaktari wawili wa watoto kuunda biskuti yenye viwango vya juu vya protini ambayo ilitumika kutibu maradhi haya.
Mwaka wa 1962 shirika la Chakula na Kilimo chini ya Hazina ya watoto ya Umoja wa Mataifa lilimpa ufadhili wa kusoma masuala ya lishe katika jamii katika Chuo Kikuu cha London.
Akiwa nchini Uingereza, Prof Ojiambo alitia bidii na kufanya vyema katika masomo ambapo pia alikuwa anasomea shahada ya lishe katika Chuo Kikuu cha London’s Queen Elizabeth College.
Baada ya kumaliza masomo, aliajiriwa kama mhadhiri msaidizi wa somo la sayansi katika bewa la elimu la chuo hicho, na baadaye kuwa mwanamke wa kwanza Mwafrika kuwa msimamizi wa mabweni ya wanawake katika taasisi hiyo.
Kama mwenyekiti wa taasisi ya wataalam wa lishe (Kenya Nutritionists and Dieticians Institute), Prof Ojiambo amekuwa akihusika katika kuendeleza mafunzo ya lishe nchini.
Kadhalika, kwa muda mrefu amekuwa akihudumu kama mdhamini katika Hazina ya Kitaifa ya walemavu.
Nyumbani kwao, ufanisi wake ulidhihirika kila mahali.
“Kuna wakati ambapo karibu kila mtoto msichana aliitwa Julia,” asema.
Ni kutokana na sababu hiyo ndipo mwaka wa 1974, jamii yake ilimuomba kuwania kiti cha ubunge cha Busia ya kati ambapo alimshinda mpinzani wake katika kampeni kali.
Ni ufanisi huu ambao umemfanya kutambuliwa katika majukwaa mbalimbali.
Kati ya mwaka wa 1966 na 1968 alipewa tuzo ya Dean’s Research Grant Award katika Chuo kikuu cha Nairobi kutokana na utafiti wake katika masuala ya lishe kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.
Mwaka wa 1976, shirika la chakula na kilimo (FAO) lilimpa tuzo ya Ceres Gold Medal Winner kutokana na huduma zake za kipekee katika mipango ya nyumbani na kuendeleza wanawake.
Mwaka wa 2007 shirika la Kenya Coalition for Action in Nutrition (KCAN) lilimtambua kama mtaalam wa lishe wa mwaka.
Mwaka wa 2003, alipewa tuzo ya Moran of the Burning Spear (MBS) ili kumtambua kutokana na juhudi zake kuwapa wanawake na watoto nguvu.
Na ufanisi huu kamwe haukumzuia kuendesha majukumu yake kama mke na mama.
Kwa mfano alipoenda nchini Amerika kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard, alikuwa na watoto watatu ambapo kitinda mimba alikuwa na wiki tatu pekee.
“Watu walidhani kwamba nilikuwa wazimu lakini nilimakinika.”
Prof Ojiambo anasema nguvu zake zinatokana na watoto wake, vile vile malezi yake ambapo alikuzwa kwa njia za Kikristu.
“Imani yangu katika Mungu imenipa amani ambapo pasipo hiyo pengine singeweza kufanya haya,” asema.
Mume japo marehemu apata sifa
Anamsifu mumewe ambaye sasa ni marehemu kama nguzo kuu ya ufanisi wake.
“Alikuwa mwenzangu, rafiki, mkufunzi na mhimili wangu.”
Aidha, anasema kuwa mamake alichangia pakubwa kufinyanga sifa zake.
“Alikuwa na moyo wake mkunjufu sana ambapo alimkaribisha kila mtu nyumbani, hasa wanawake waliodhulumiwa katika ndoa na hata walemavu,” aongeza.
Pia, huku akimtaja dadake mkubwa Bi Ruth Auma Vuyiya, mwanamke wa kwanza kuteuliwa msimamizi katika idara ya magereza nchini, Prof Ojiambo anasema kwamba ndugu zake walichangia pakubwa ufanisi wake kiamasomo.