MWANAMKE MWELEDI: Sanaa i mishipani na azidi kuipa uhai
Na KENYA YEARBOOK
AMECHANGIA pakubwa kukuza vipaji vya wasanii humu nchini.
Hii ni kupitia kituo cha GoDown Arts Centre, ambapo anahudumu kama Mkurugenzi Mtendaji.
Kupitia kituo hiki, Joy Mboya amesaidia kuimarisha vipaji vya wahusika katika sanaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uigizaji na muziki miongoni mwa zingine.
Kwa zaidi ya mwongo mmoja, kituo cha GoDown Arts Centre, kimetoa nafasi na mazingira mwafaka kwa wasanii kuonyesha vipaji vyao, vile vile kuwaunganisha na hadhara ya Afrika Mashariki na hata sehemu zingine duniani.
Aidha, kituo hiki huandaa kongamano mara mbili kila mwaka na kuwaleta pamoja wahusika wakuu katika sekta ya utamaduni ili kujadiliana jinsi ya kuimarisha sekta hii.
Na hivyo, GoDown Arts Centre imewezesha umma kuwasiliana vyema na wasanii na kutambua zaidi aina mbalimbali za sanaa. “Mwongo mmoja uliopita, maonyesho ya sanaa yalivutia vikundi vidogo vya raia wa kigeni na wasanii wachache, lakini sasa tumeshuhudia wasanii wengi wa humu nchini wakijihusisha na sanaa,” aeleza.
Hii imefungulia milango wasanii wengi kwa kuwapa fursa za kusafiri katika sehemu zingine duniani, na hivyo kujitambulisha.
Mmoja kati ya watoto saba wa Elmad na Catherine Mboya, msanii huyu alikuzwa jijini Nairobi na kusomea shule ya msingi ya Kilimani na ya upili ya Alliance Girls’. Mapema maishani, alikumbwa na changamoto ya kuchagua kati ya sanaa na masomo. Alikuwa na penzi kwa masomo ya sayansi na sanaa katika shule ya msingi na hata ya upili, lakini bado alitatizika kuchagua somo atakalosomea chuoni.
“Ningechagua muziki lakini wakati huo tasnia hii haikuwa imeshamiri vilivyo. Kutokana na penzi langu kwa sayansi na sanaa niliamua kusomea usanifu majengo,” asema.
Kwa hivyo alisomea shahada ya digrii ya usanifu majengo katika Chuo Kikuu cha Princeton, Amerika, kati ya 1980 na 1985. Akiwa huko, penzi lake kwa muziki lilizidi, penzi alilolikoleza hata zaidi aliporejea nchini Kenya.
Safari yake katika sanaa ilianza rasmi akiwa mwanachama wa bendi ya muziki ya Musikly Speaking, iliyojumuisha pia wanamuziki, Suzanne Gachukia, Susan Matiba na Ciru Gecau.
Bendi hii ilitikisa kuta za burudani nchini katika miaka ya tisini, kupitia vibao kama vile Jamriambo na Saturday Nite. Aidha, kupitia umaarufu wake, bendi hii iliandalia wanamuziki njia, vile vile vikundi vya muziki vilivyofuatia kama vile Hart, Five Alive, Kalamashaka, Zanaziki, Gidi Gidi Maji Maji na hata Jimmi Gathu.
Mbali na kujihusisha na masuala ya uimbaji na burudani akiwa katika kikundi hiki, pia aliandika na kuelekeza michezo ya kuigiza katika Phoenix Theatre Group. Kumbuka kwamba alikuwa akifanya haya huku akiendelea kufanya kazi yake ya usanifu majengo.
Umaarufu wa kikundi hiki ulizidi kuongezeka waliposafiri Amerika kwa ziara ya miezi mitatu. “Tukiwa hapa tulipata fursa ya kufanya uchunguzi zaidi kuhusu muziki katika harakati za kutafuta jinsi ya kuimarisha sekta hii nchini,” asema.
Baada ya mwongo mmoja kwenye mwangaza, kikundi hiki kilivunjika huku kila mmoja akifuata mkondo tofauti maishani. Mwaka wa 1993, alienda nchini Australia ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha New South Wales kusomea shahada ya ziada katika masuala ya sauti. Akiwa huko, alipata fursa ya kufunza pia.
Alirejea nchini mwaka wa 1998 na kupitia hazina ya Fame Trust, akazindua mpango wa mafunzo kwa wanafunzi wa shule ya upili waliokuwa na nia ya kusomea sanaa. “Niliangalia safari yangu na kupatwa na haja ya kufunza vijana jinsi ya kujiendeleza kisanaa.”
Kituo chafunguliwa
Mpango huu uliendelea kwa mwaka mmoja na mshawasha wa kuimarisha sanaa, muziki na densi ukamsukuma kuanzisha kituo cha GoDown Arts Centre.
Kilifungua milango 2003 lengo lake likiwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kupitia sanaa.
Mbali na hayo, yeye ni mdhamini wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Hazina ya Gaara Dance Foundation, inayonuia kuunganisha muziki wa Kenya kupitia utafiti, mafunzo na mauzo.
Aidha, yeye ni mdhamini wa tuzo za filamu za Kalasha Film Awards huku akiwa amewahi kuhudumu katika Bodi ya wadhamini ya Action for Music and the Governing Council of the Kenya Cultural Centre.
Pia, yeye ni mhisani ambapo amekuwa akiunga mkono mradi wa maradhi ya fistula, unaodhaminiwa na shirika la AMREF. Vile vile, amekuwa akisaidia watoto kutoka familia maskini kupata elimu.
Lakini licha ya mwangaza huu, ni mke na mama wa mabinti wawili Tamara na Khadija. Anasema kwamba anafurahia majukumu yake kama mke na mama, lakini pia anakiri kwamba haijakuwa rahisi kwake kusawazisha masuala hayo mawili.
Matumaini yake katika kipindi cha mwongo mmoja ujao ni kuona wasanii wamejumuishwa katika masuala ya elimu na uongozi utakaoshinikiza sera za kuimarisha sanaa.
Anapanga kukuza zaidi kituo hiki huku akiendelea kujishughulisha na jinsi ya kupanua nafasi zaidi kusaidia wasanii kufanya mazoezi na kupiga msasa vipaji vyao.