MWANAMKE MWELEDI: Ukakamavu ulimpa shavu serikalini
Na KEYB
ALIKUWA mwanamke wa kwanza kuteuliwa kama waziri, huku akijitosa kwenye siasa katika miaka ya sabini, enzi ambazo wanawake hawakuwa wengi katika fani hii.
Jina lake ni Winfred Nyiva Mwendwa, aliyewahi kuhudumu katika Wizara ya Utamaduni na huduma za kijamii katika serikali ya Rais mstaafu Daniel arap Moi, wadhifa aliopata baada ya kuchaguliwa kama mbunge kwenye uchaguzi wa mwaka wa 1992.
Aidha, anafahamika kwa kutawala siasa za eneo bunge la Kitui Magharibi tangu mwaka wa 1974, na kuwa mmoja wa wanawake wachache waliokuwa wabunge wakati huo kama vile Julia Ojiambo, Eddah Gachukia, Jemima Gecaga na Chelagat Mutai.
Bi Mwendwa ambaye alikuwa mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya Alliance Girls’ aliandkisha vitabu vya kumbukumbu mwaka wa 1992, alipoteuliwa na Rais mstaafu Moi katika baraza la mawaziri.
Aidha, mwaka wa 1995 aliongoza wajumbe 450 wa Kenya katika kongamano la wanawake jijini Beijing, Uchina.
Bi Mwendwa amehudumu katika vipindi vitatu kama mbunge wa Kitui Magharibi. Alichaguliwa mara ya kwanza chini ya chama KANU ambapo alihudumu hadi mwaka wa 1979.
Bi Mwendwa alichaguliwa tena kama mbunge mwaka 1997. Aliwania tena kiti hicho mwaka wa 2002 na kushinda chini ya chama cha National Rainbow Coalition. Alihudumu hadi mwaka wa 2007.
Mwaka wa 2013, aliwania na kushinda kiti cha Mwakilishi mwanamke, Kaunti ya Kitui kupitia chama cha Wiper Democratic Movement.
Huenda mojawapo ya mambo yaliyochangia kunawiri kwake katika siasa ni kwamba fani hii ilikuwa thabiti katika familia yake. Kwa mfano, baba mkwe marehemu Mwendwa Kitavi, alikuwa chifu.
Mbali na hayo, marehemu mumewe, shemejiye Kyale Mwendwa, wakati mmoja walihudumu kama wabunge wa Kitui Magharibi. Pia, shemejiye mwingine, Ngala Mwendwa, aliwahi kuwa waziri.
Mojawapo ya mambo yaliyomweka upeoni ni ujasiri wake wa kuzungumzia masuala tata pasipo woga. Kwa mfano, katika miaka ya sabini, alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kupigania haki ya ugawaji sawa wa nafasi za uongozi miongoni mwa wanaume na wanawake.
Aidha, mara nyingi alinukuliwa akiwaomba wapiga kura kuwachagua wagombeaji wa kike huku akipinga waziwazi viongozi wanaume wafisadi.
Isitoshe, kuna wakati ambapo bila kusita alimwambia Rais Moi kuhakikisha kwamba angaa nusu ya wabunge 12 walioteuliwa ni wanawake ili kuhakikisha usawa.
Mwaka wa 1979, akichangia bungeni, aliomba kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa huku akihoji kwamba wake zao waliteseka zaidi kwa sababu waliachiwa mzigo wa kuwalea wanao pekee yao.
Mwaka wa 1996, alipinga vikali pendekezo kutoka kwa baadhi ya wenzake kuanzisha chama cha kisiasa cha wanawake, akihoji kwamba huo ulikuwa woga na ubaguzi.
Hata hivyo, alisisitiza mwito wake kwa serikali, wakati huu akitaka asilimia 25 ya nafasi bungeni kuachiwa wanawake na kutoa mifano ya mataifa kama vile Uganda, Malawi na Afrika Kusini.
Mbali na masuala ya kisiasa, Bi Mwendwa amekuwa kigezo kwa wanawake na wajane kwa njia nyingi kwa kuendelea kupambana na maisha katika uongozi na kuhudumia jamii hata baada ya kifo cha mumewe.
Japo Bi Mwendwa ambaye ni mama wa watoto wawili, Kavinya na Maluki, hakuwahi kuolewa tena baada ya kifo cha mumewe, amekuwa mstari wa mbele kuwahimiza wanawake wajane kuolewa tena endapo wako tayari.
Safari ya Bi Mwendwa katika siasa ilifikia kikomo mwaka wa 2016, alipotangaza kwamba hangewania tena kiti cha mwakilishi mwanamke, Kaunti ya Kitui katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017 huku akistaafu rasmi kutoka siasa na kusema kwamba ulikuwa wakati mwafaka kutoa nafasi kwa viongozi wachanga.