MWANAMKE MWELEDI: Ukoloni uliwasha moto wa uandishi
Na KENYA YEARBOOK
ALISHUHUDIA mojawapo ya nyakati ngumu sana katika historia ya Kenya ambapo utamaduni wa jamii asili uligongana ana kwa ana na mtazamo mpya wa kigeni uliotokana na utawala wa kikoloni.
Ni suala lililofinyanga mawazo yake Muthoni Likimani, na hivyo kumwezesha kung’aa katika nyanja mbalimbali.
Bi Likimani ameshamiri kama mwandishi wa makala na vitabu vya watoto. Hii ni mbali na wakati mmoja kuhudumu kama mwanahabari na hata mtaalamu katika sekta ya mahusiano mema.
Katika miaka ya sitini, alikuwa mmojawapo wa wanawake wa kwanza kuajiriwa kama produsa katika stesheni ya Sauti ya Kenya(VOA) inayofahamika kwa sasa kama Kenya Broadcasting Corporation (KBC).
Jina lake lilihusishwa na Shangazi na Watoto, kipindi cha watoto kilichoangazia hadithi za Kiafrika huku nia yake ikiwa kudumisha utamaduni miongoni mwa watoto. Wakati huo pia, alikuwa produsa wa Kipindi cha Akina Mama, kilichoangazia ustawi.
Isitoshe, alikuwa Mkenya wa kwanza wa asili ya Kiafrika nchini kumiliki kampuni ya masuala ya mahusiano mema.
Bi Likimani alizaliwa mwaka wa 1925 ambapo alikuwa binti ya mmojawapo wa wahubiri wa kwanza wa Kianglikana, Levi Gachanja na mkewe Mariamu.
Alikuwa mnufaishwa wa elimu ya kikoloni. Alisoma katika shule za msingi nyumbani kwao kabla ya kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Kahuhia iliyofahamika kama Government African Girls Teachers’ College (GAGTC), 1947.
Kama mtoto wa mhubiri, aliepushwa na utamaduni ambao kanisa la Kianglikana halikukubaliana nao. Anakumbuka jinsi alivyoshuhudia Waafrika waliokuwa wameikumbatia imani ya Kikristu walivyokumbwa na ugumu wa kusawazisha mtazamo huu mpya na maisha yao ya kale.
Hii ilimlazimu kuandika kitabu chake cha kwanza They Shall be Chastised, kilichozungumzia mgongano kati ya utamaduni wa Kiafrika na Ukristu katika enzi za kikoloni na jinsi waliobadili imani walivyotatizika kuidumisha.
Pia, anakumbuka kushuhudia ukatili ukitekelezwa na wakoloni dhidi ya hasa wanaume wa Kiafrika na jinsi wanawake walivyoteseka sawa na wanaume kwa kufanyishwa kazi ngumu bila malipo.
“Walikuwa wanawaandalia waume wao vyakula huku wakihatarisha maisha yao katika harakati za kupigania uhuru,” aeleza.
Ni matukio haya yaliyochochea uandishi wa kitabu chake maarufu Passbook Number F47927: Women and Mau Mau in Kenya.
Kitabu chake cha tatu What Does a Man Want? kilitokana na jinsi alivyoshuhudia mabadiliko ya kitabia miongoni mwa wanaume wa Kiafrika walipoanza kupata ajira nzuri na kupokea mshahara mnono baada ya kujinyakulia uhuru.
Mwaka wa 1958 akiwa mkufunzi katika chuo cha mafunzo ya Ualimu cha Kahuhia Women’s Teaching College, alipata ufadhili wa kusomea elimu na ustawi wa jamii katika taasisi ya elimu ya chuo kikuu cha London, nchini Uingereza.
Safari yake katika fani ya Uanahabari ilianza alipofanya kazi katika Shirika la Habari la Uingereza (BBC) ambapo alikuwa na kipindi kwa lugha ya Kiswahili.
Aliporejea nchini, aliajiriwa na kituo cha habari cha Sauti ya Kenya (VOA) kama produsa wa kwanza mwanamke ambapo baadaye aliondoka na kujitosa katika sekta ya mahusiano mema.
Wanawake na watoto
Alianzisha kampuni ya Noni’s Publicity, shirika ambalo hasa lilikuwa likifanya kazi na brandi zilizolenga wanawake na watoto.
Mchango wake katika sekta mbalimbali umemfanya kutambuliwa na kutuzwa. Mwaka wa 2008 alipewa tuzo ya Presidential Moran of the Burning Spear (MBS) Award.
Pia, amewahi kupewa tuzo ya Grace Githu Award for Human Rights, mbali na Young Women’s Christian Association (YWCA) Award.
Pia, amewahi twaa tuzo ya Public Relations Society of Kenya (PRSK) Golden Honour Award kutokana na uongozi wake wa kipekee katika sekta ya huduma ya mahusiano mema, miongoni mwa tuzo zingine.
Ustawi wake haukumzuia kuwa na familia. Bi Likimani aliolewa na Dkt Jason Clement Likimani akiwa chuoni. Wakati huo Dkt Likimani alikuwa daktari wa kwanza wa kimatibabu wa asili ya kiafrika, akihudumu katika hospitali ya Fort Hall Hospital, ambayo kwa sasa inafahamika kama Murang’a District Hospital.
Dkt Likimani alitoka jamii ya Wamaasai ambapo uchumba wa wawili hawa uliibua minong’ono hasa ikizingatiwa kwamba ndoa baina ya watu kutoka makabila tofauti lilikuwa jambo geni enzi hizo.
Lakini hilo halikutikisa uhusiano wao kwani ndoa yao ilidumu hadi kifo cha Dkt Likimani mwaka wa 1989. Pamoja walijaliwa mabinti watatu.
Bi Likimani anaendelea kuandika vitabu vya watoto chini ya kitambulisho cha Grandmother Fire Series Label. Hadithi hizi hasa zinahusisha tamaduni za jamii mbalimbali nchini.
Kitabu chake Women of Kenya in the Decade of Development kinaangazia wanawake wenye ushawishi na mchango wao katika ustawi.
Kitabu hiki kiliandikwa kwa minajili ya Kongamano la wanawake la Umoja wa Mataifa lililoandaliwa jijini Nairobi mwaka wa 1985.
Kitabu chake cha hivi punde kwa jina Fighting Without Ceasing, kilizinduliwa mwaka wa 2013 na kinazungumzia matatizo na changamoto wanazokumbana nazo wanawake barobaro.
Bi Likimani angependa kuona wanawake zaidi wakiandika. Pia, anapendekeza kutumia lugha zingine mbali na Kiingereza huku akiwarai waandishi kuchapisha vitabu kwa Kiswahili au lugha zingine za kiasili.
Kwa sasa anashughulikia miswada kadha inayoangazia umuhimu wa kuwapa wanawake nguvu.
Pia, anapanga kuunda hifadhi ya nyaraka nyumbani kwake jijini Nairobi ili kusaidia wanawake kufikia vitabu vya mada tofauti kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.
Aidha, anahusika katika miradi kadha ya kanisa na ustawi wa kijamii. Alianzisha kituo cha Mariamu Home Economics Training Centre katika mtaa wa Kangemi, Nairobi, kinachotoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wasichana kutoka familia maskini.