MWANAMKE MWELEDI: Usukani wake katika KWFT umeinua wengi
Na KENYA YEARBOOK
ALIPOJIUNGA na shirika la kutoa mikopo midogo la Kenya Women’s Finance Trust (KWFT), lilikuwa katika hali mbaya, lakini sasa kwa takriban miongo mitatu kwenye hatamu, amelibadilisha na kuwa mojawapo ya mashirika yanayoongoza katika sekta ya fedha barani.
Huo ni muhtasari wake Dkt Jennifer Riria aliyehudumu kwa muda mrefu kama afisa mkuu mtendaji wa Kenya Women Finance Trust na sasa ni afisa mkuu mtendaji wa Kenya Women Holdings (KWH).
Kama kiongozi wa shirika hili, Dkt Riria alichangia pakubwa katika kubadilisha maisha ya wanawake wengi pamoja na familia zao.
Akiwa kwenye hatamu, KWFT imekuwa mojawapo ya taasisi kuu za kutoa mikopo midogo barani Afrika huku shirika hili likipata tuzo mbali mbali. Mwaka wa 2008, shirika hili lilikuwa shirika tanzu la Kenya Women Holding (KWH) –shirika lisilo la faida linalotoa huduma za kifedha zinazopigania haki za wanawake na kuwapa nguvu za kiuchumi.
Kufikia mwaka wa 2013, shirika hili lilikuwa na zaidi ya afisi 230 na matawi katika kaunti 45.
Aidha, linajivunia kuwa na zaidi ya wateja milioni moja huku likitoa huduma za kifedha na zisizo za kifedha.
Mwaka wa 2014, shirika la Kenya Women Finance Trust Deposit Taking Microfinance lilibadilika na kuwa benki kamili, Kenya Women Microfinance Bank Limited.
Mzaliwa wa eneo la Kathangari, Kaunti ya Meru, kama mtoto wa nne miongoni mwa wengine kumi, msukumo wake wa kubadilisha maisha ya wanawake ulianza akiwa angali mdogo huku ari hiyo ikichangiwa na maisha magumu kijijini.
“Nilishuhudia mama yangu pamoja na akina mama wengine kijijini wakipitia magumu, na hivyo nilijua kwamba sikutaka kukumbana na hali sawa na hiyo maishani,” aeleza Dkt Riria.
Mamake alimhimiza kutia bidii shuleni ili kuepuka matatizo ya aina hiyo.
“Hiyo ilinipa msukumo na hivyo niliamua kuwa nilihitajika kufanya jambo ili kusaidia wanawake,” aeleza.
Alijiunga na shule ya msingi ya Kathangari, Kaunti ya Meru, ambapo kama watoto wengi katika maeneo ya mashambani, alilazimika kusawazisha muda wa masomo na kazi za nyumbani zilizojumuisha kuwashughulikia wadogo wake, kupika, kuteka maji, kukata kuni na kuchunga mifugo.
Hata hivyo, hali hiyo haikuwa kizingiti kwake kimasomo kwani alitia bidii shuleni na kujihifadhia nafasi katika shule ya upili ya Precious Blood, Riruta.
Mwaka wa 1972 alikamilisha shule ya upili na kufanya vyema, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisomea elimu na masuala ya kiuchumi.
Bidii yake haikukomea hapo kwani alifanya vyema tena na kupata ufadhili wa kusomea shahada ya uzamili katika usimamizi wa elimu katika Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza.
Uchu wake wa kuleta mabadiliko ulimrejesha nchini Kenya pindi baadaye, ambapo alihudumu kama mwalimu kabla ya kusomea shahada yake ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Kisha baadaye, Dkt Riria alihudumu katika shirika la Umoja wa Mataifa na licha ya kufanya vyema, bado alikumbwa na kiu ya kutaka kubadilisha maisha ya wanawake.
Oktoba mwaka wa 1991 alichukua hatamu katika shirika la KWFT ambapo wakati huo lilikuwa katika hali mbaya.
“Hatukuwa na wateja na tulikuwa katika hatari ya kufungwa,” akumbuka.
Alipochukua hatamu, shirika hili lilikuwa na wafanyakazi wanne pekee wa kudumu, bila wateja na mikopo ya takriban Sh2,000,000 iliyohitajika kudaiwa, ambapo shirika hili likikumbwa na hatari ya kufungwa.
Chini ya uongozi, KWFT ilienda hatua zaidi na kubadili maisha ya wateja na hivyo kubadilisha maisha ya familia nyingi nchini kote huku, shirika hili likiunda bidhaa kuambatana na mahitaji ya wateja.
“Ikiwa mteja atakuja na kuzungumzia tatizo la maji, tunakaa chini na kuunda bidhaa kama vile matangi ya maji kwa wanawake katika eneo husika ili waweze kuvuna maji safi,” aeleza.
Alienda hatua zaidi na kuongoza usimamizi katika sekta hii kuambatana na mahitaji ya kijamii, wakati huo akihudumu kama mwenyekiti wa Halmashauri ya kitaifa ya mashirika ya kutoa mikopo midogo (AMFI).
Mbali na masuala ya kifedha, yeye pia ni mwanzilishi wa TUVUKE Initiative, vuguvugu la amani analoongoza na lililoanzishwa mwaka wa 2011 baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa kitaifa wa 2007/2008.