Makala

Mwanamume aliyebadili jinsia adai kudhulumiwa akiwa gerezani

June 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA TITUS OMINDE

ALIZALIWA na kulelewa katika kaunti ndogo ya Moiben, Uasin Gishu kama mvulana na kutahiriwa chini ya mila za Wakalenjin, lakini akiwa na umri wa miaka 15, alitamani kuwa mwanamke na hatimaye kubadili mtindo wake wa maisha na hata kughushi stakabadhi muhimu za utambulisho ili kujitambulisha kama mwanamke.

Alibadilsha jina lake la kuzaliwa Hillary Kiprotich na kujitambulisha kama Shieys Chepkosgei.

Licha ya ‘kukamatwa’ kwake na kushtakiwa kwa kughushi stakabadhi, amewasilisha ombi katika mahakama kuu ya Eldoret akidai kuwa haki zake zilikiukwa alipokamatwa na kuwekwa katika seli ya wanawake katika gereza la wanawake la Eldoret.

Katika ombi hilo anawashutumu maafisa wa kike katika Gereza la Wanawake la Eldoret kwa kumdhulumu walipogundua kuwa alikuwa mwanamume katika seli za wanawake aliposhtakiwa kwa kujifanya muuguzi wa kike katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Mo MTRH.

Wakati wa ukaguzi wa kawaida katika gereza hilo, mahakama iliambiwa afisa wa kike alipiga mayowe kuwa mahabusu aliyedhaniwa kuwa mwanamke alikuwa mwanamume.

Hata hivyo, akiulizwa maswali na wakili wa serikali kortini, Mark Mugun alikiri mahakamani kwamba alizaliwa mwanaume na wakati wa ukuaji wake akiwa na umri wa miaka 15 alianza kuchukia kuwa mwanaume ndio maana alianza mchakato wa kumbadilisha jinsia maarufu, transgender.

Kupitia wakili wake Colbert Ojiambo, alidai kuwa maafisa wa gereza la wanawake la Eldoret walimnyanyasa kwa kutaka kubaini jinsia yake.

Katika ombi alilowasilisha mahakamani Juni 20, 2019 likiwashtaki Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Kamishna Mkuu wa Huduma za Magereza na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi kwa madai ya kugeuka haki zake za kibinadamu.

Aliiambia mahakama kuwa washtakiwa walikiuka haki zake za kibinadamu kwa upekuzi wa mwili unaohusisha kuvuliwa nguo, kugusa sehemu zake za siri, kupima sehemu zake za siri miongoni mwa malalamishi mengine.

“Nilipitia aibu nyingi gerezani, niliguswa sehemu za mwili wangu huku wakitumia lugha ya aibu dhidi yangu, haki zangu zilikiukwa,” aliambia Jaji Reuben Nyakundi siku ya Alhamisi.

Akijibu shutuma hizo, wakili wa serikali Bw Mugun aliambia mahakama kwamba upekuzi dhidi ya mlalamishi ulifanywa kwa ajili ya usalama wake.

Bw Mugun aliambia mahakama kuwa iwapo mlalamishi angewekwa katika kizuizi kinachofaa katika gereza hilo huenda mahabusu wengine wangemdhulumu.

Kinachoshangaza ni kwamba mlalamishi alikiri kwamba msako huo ulimsaidia kukwepa kubakwa na wafungwa wa kike endapo wangetambua jinsia yake.

“Ndio, msako huo ulinisaidia kukwepa kufanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kubakwa na wafungwa wengine katika gereza la wanawake,” alijibu Chepkosgei alipoulizwa na wakili wa serikali ikiwa ukaguzi huo ulikuwa wa manufaa kwake.

Aliambia mahakama kuwa ingawa ana viungo vya kiume vinavyofanya kazi angependa kutambuliwa kama mtu aliyebadili jinsia.

Alithibitisha mbele ya mahakama kwamba ana maumbile yote ya mwanamume lakini amepoteza hamu ya kuwa mwanamume badala yake anatamani kuwa mtu aliyebadili jinsia.

“Nilipokuwa kijana nilichukia jinsia ya kiume na ndiyo maana napendelea kuwa mtu aliyebadili jinsia,” alisema Chepkosgei.

Hata hivyo, alikiri kwamba alitahiriwa kulingana na mila za Wakalenjin.

Washtakiwa wote wamekanusha ukiukaji wowote wa haki za binadamu dhidi yake.

Wakili anayeiwakilisha MTRH aliiambia mahakama kuwa hospitali hiyo ilimfanyia uchunguzi kutokana na agizo la mahakama ili kujua jinsia yake ili kufahamu mahali pazuri pa kumweka akiwa kizuizini.

Alishutumu hospitali kwa kuchukua damu yake kwa ajili ya kupimwa ili kubaini jinsia yake bila yeye kuridhia.

Mahakama iliambiwa kwamba kipimo cha estrojeni kutoka hospitali ya MTRH kilithibitisha kwamba alikuwa mtu mzima wa kiume na viungo vya uzazi kamilifu.

Aidha, aliishutumu Hospitali kwa kumfanyia uchunguzi wa radiolojia bila ridhaa yake.

Hakupinga matokeo ya uchunguzi katika hospitali hiyo lakini alisisitiza kuwa haki zake zilikiukwa kama mtu aliyebadili jinsia.

Wakili wa serikali alimwambia kwamba hakuwa na stakabadhi yoyote ya kuthibitisha kwamba alikuwa amebadilisha jinsia yake kutoka kwa mwanamume hadi mtu aliyebadili jinsia kama inavyotakiwa kisheria.

Wakili wake alisisitiza kuwa licha ya kutokuwa na stakabadhi, haki zake za faragha na haki nyingine za binadamu zilikiukwa wakati wa kukamatwa kwake.

Mahakama iliagiza kesi hiyo kutajwa Juni 19 ili kutoa agizo kwa mtaalam wa watu waliobadili jinsia kufika mahakamani ili kutoa mwanga zaidi kuhusu masuala ya kisheria ya watu waliobadili jinsia.

Kesi hiyo itatajwa Juni 19 na itaendelea kusikizwa Julai 10.