Makala

Mwanamume aliyefungwa jela na malaria ya ubongo arejea nyumbani

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA TITUS OMINDE

HUKU machozi ya furaha yakimtiririka, Bw Philip Kipkemoi Bor alijumuika na wenzake kijijini Cheptel katika wadi ya Kapsoit kaunti ya Kericho kusherehekea kuachiliwa kwake kutoka jela baada ya kutumikia kifungo kwa zaidi ya miongo mitatu baada ya kupatikana na hatia licha ya kuwa na malaria ya ubongo.

Taifa Leo ilipozuru kijiji hicho, tulikaribishwa kwa nyimbo za sifa na ushindi kutoa shukrani kwa Mungu kufuatia kuachiliwa kwa Bw Kipkemoi ambaye sasa ana umri wa miaka 56.

Bw Kipkemoi ndiye kifungua mimba katika familia ya watoto sita.

Mama yake, Bi Grace Misik, 72, hakuficha furaha yake baada ya kumpokea mwanawe ambaye amekuwa gerezani tangu 1988.

“Nakosa maneno ya kuMshukuru Mungu, nasema tu asante Mungu, asante Mungu,” alisema Bi Misik kwa mtiririko wa mtu anayeghani shairi.

Bi Misik alisema licha ya muda mrefu ambao mwanawe alikaa gerezani, hakukata tamaa kumwombea akiwa na matumaini kwamba yaliyompata Paulo na Sila wa Biblia siku moja yangetokea kwa mwanawe.

“Kutokana na matumaini makubwa tuliyokuwa nayo kwa Mungu, tulikuwa tukimtembelea karibu mara tatu kwa mwaka ili tu kumwonyesha jinsi tunavyomthamini mwana wetu,” alisema mzazi huyo.

Kaka yake, ambaye ni Bw Musa Kipkorir hakuficha furaha ya kumpokea kaka yake mkubwa.

“Kama Wakalenjin, mtu hawezi kuchukua nafasi ya kaka mkubwa ikiwa kaka yake yuko hai. Nilikuwa nikishikilia tu lakini sasa nimefarijika kwa kuwa mwenyewe amerejea,” akasema Bw Kipkorir.

Naye Bi Alice Cherono ambaye ni dadake, alisema sala na kufunga ilikuwa kawaida katika familia hiyo kukiwa na matumaini ya kumuona Philip akirudi nyumbani.

Maoni kama hayo yalitolewa na majirani wa Bw Kipkemoi wakiongozwa na Bw Samuel Langat ambaye alimtaja kama mtu mwenye adabu ambaye alikuwa mwadilifu kijijini.

“Tulipokua pamoja, Bw Kipkemoi alikuwa mtu mzuri na kilichotokea kilitushangaza. Ndio maana tumekuwa tukitumai kwamba siku moja atakuwa mtu huru jinsi ilivyo leo,” akasema Bw Langat.

Bw Kipkemoi ambaye alikuwa ametumikia takriban miaka 35 gerezani kuhusiana na mauaji, aliachiliwa na Mahakama Kuu ya Eldoret kufuatia rufaa yake iliyofaulu.

Alipatikana na hatia ya mauaji ya jirani yake akiwa na umri wa miaka 18.

Marehemu Jaji Daniel Aganyanya alimpata na hatia hiyo ya kutekeleza mauaji ya jirani yake kwa kutumia kitu butu. Hii ni licha ya ripoti ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Eldoret kusema wakati wa kitendo hicho, mshtakiwa alikuwa na malaria ya ubongo, kumaanisha alikuwa ametatizika kiakili.

Ilielezwa kwamba wakati wa tukio, Bw Kipkemoi alikuwa chumbani mwake na akamvaa mzimamzima jirani yake aliyevuruga usingizi wake kwa kumwamsha.

Siku ya tukio ilikuwa ni mnamo Februari 26, 1988, katika eneo la Lessos katika Kaunti ya Nandi.

Wakati wa mapigano hayo, Bw Kipkemoi alimpiga jirani kwa kifaa butu na akazirai na kufariki papo hapo.

Lakini Jaji Reuben Nyakundi alitoa amri ya kuachiliwa huru kwa Bw Kipkemoi mnamo Aprili 19, 2024, hatua ambayo ilimfanya kuondoka katika gereza la Eldoret GK baada ya kutumikia kifungo hicho kwa takriban kipindi chote cha maisha yake ya ujana.

Ana mpango wa kuoa atakapotulia.

“Sijakata tamaa maishani. Ninatumaini kuoa hivi karibuni na kuendelea kuMtumikia Mungu pamoja na mke wangu,” alisema Bw Kipkemoi.

Jaji alimwachilia huru kufuatia ripoti ya uchunguzi wa kiakili kutoka Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi ambapo Bw Kipkemoi alikuwa amepelekwa kwa maagizo yake ambapo ilithibitishwa kwamba sasa yuko sawa kiakili.

Hii ilikuwa baada ya ombi lake kufanikiwa kupinga kufungwa kwake kwa hisani ya Katiba ya 2010.

Soma Pia: Aliyetupwa jela akiwa na malaria ya ubongo aachiliwa

Kupitia wakili wake Oscah Oduor kutoka Kituo cha Usaidizi wa Kisheria na Urekebishaji wa tabia ya Wafungwa (CLESIR), Bw Kipkemoi aliwasilisha ombi la kupinga kifungo chake mwaka 2023.

Wakili Oduor aliambia mahakama kwamba kulingana na Katiba ya 2010, ni kinyume cha sheria kumfunga jela mtu ambaye hana akili timamu wakati wa kusomewa mashtaka, na hivyo basi, mteja wake anastahili kuachiliwa baada ya kutekelezwa kwa Katiba ya Kenya ya 2010.

Amekuwa akihudumu kifungo chake akisubiri kuona kama angepata Msamaha wa Rais.

Inaidaiwa kuwa Bw Kipkemoi alitenda makosa hayo mnamo Februari 26, 1988, katika Kijiji cha Lessos kaunti ya Nandi ambapo alikuwa amehamia na mamake mzazi.

Familia yake imelazimika kufanya baadhi ya matambiko ili kumsafisha kulingana na kanuni za Kipsigis.

“Kabla hatujamsaidia kuoa, tutamfanyia baadhi ya matambiko ya kumsafisha tunapopanga kumjengea nyumba,” alisema Bw Langat, ambaye ni rafiki yake Bw Kipkemoi.

Bw Langat alisema matambiko hayo yanakusudiwa kuzuia nguvu za mapepo zinazohusishwa na roho ya mauaji ambayo yalisababisha kufungwa kwake.