Mwanamume asimulia jinsi kuoa mapema kumemzimia nyota ya masomo, kazi nzuri
NA FRIDAH OKACHI
KATIKA kijiji cha Daraja Mbili, kilomita 20 kutoka mji wa Kisumu, shughuli za kuvuna mchanga na kilimo hutumika kuwa kitenga uchumi kwa wakazi hao.
Kijijini humo, Stephen Owiyo Ochieng amesalia kuwa mlezi kwa wanawe wanne, baada ya kuachwa na mke licha ya kuacha masomo ya chuo kikuu ili kutafuta kazi na kusaidia familia yake.
Bw Ochieng alizika ndoto ya kuwa mwanahabari miaka kumi na mitatu iliyopita, katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro na kuanza kutafuta kazi ya kukimu familia yake na kumfurahisha mkewe.
“Mwaka wa tatu, majukumu ya nyumbani yaliongezeka maradufu. Pesa nilizofadhiliwa na serikali (HELB), hazikuwa zinatosha. Mke wangu alinisukuma kutafuta kazi. Nilifanya uamuzi wa kukatiza masomo nikiwa na fikra ya kupata kazi nzuri na labda nirudi shule tena,” alianza kusimulia Bw Ochieng.
Ochieng, 34, aliambia Taifa Leo alijiunga na chuo kikuu miaka miwili baada ya matokeo ya KCSE – 2007. Wakati huo alijikuta katika msukumo wa kuanzisha mahusiano yaliyompelekea kuwa kwenye ndoa ya shubiri.
“Nilifanikiwa kupata jiko na kisha tukapata kifungua mimba ambaye kwa sasa yupo gredi ya 8. Miaka miwili baadaye, mke wangu alipata ujauzito mwingine, na tukapata watoto pacha,” alisema Ochieng.
Mwaka wa kwanza kujiunga na chuo kikuu, alijipata kwenye mtihani mgumu alipoachiwa wanawe watatu na mkewe aliyeondoka nyumbani bila kumfahamisha.
“Pacha wangu walikuwa miezi minne na siku kadhaa. Bahati ni kuwa, shule na nyumbani haikuwa mbali sana. Nilichukua wale watoto na kupelekea mama na kuanza kumtafuta mke wangu. Katika harakati za kumtafuta niliweza kubaini alikuwa kwenye ndoa nyingine na watoto wengine wawili jambo ambalo hakuwahi kunieleza,” alisikitika Bw Ochieng.
Alimshawishi mkewe akakubali kurejea nyumbani. Majukumu ya familia yalimlemea tena baada ya ufadhili aliopokea wa Sh48,000 ulipokosa kumfurahisha mkewe na akaacha masomo kutafuta kazi.
“Nilipata msukumo kutoka kwake nitafute kazi ya kulisha familia. Maamuzi ya kuacha shule yalinijia. Mwaka 2021, mke wangu aliniacha tena na mtoto mchanga. Ilibidi nihamie karibu na nyumbani ili kupata usaidizi kwa mama mzazi,” alisema Bw Ochieng.
Mwaka huo, mkazi huyo wa Daraja Mbili alihisi kutumiwa na mkewe ambaye alimwacha akiwa ananinginia baada ya kuondoka nyumbani na vitu vyake akimwachia mavazi na watoto.
“Nilitamani nife kwa kujitia kitanzi, lakini wazo la watoto wangu kunihitaji…likanipa motisha na nikajipa moyo.”
Kinachomkera zaidi ni jinsi jamii humchukulia kuwa mwanafunzi aliyekuwa na maono makubwa ila sasa amesalia kufanya vibarua vya kulima kupata riziki.
Bw Ochieng alikuwa na ndoto ya kuwa mwanahabari, ndoto hiyo imedidimia na kuwa mkulima ili kulea familia yake licha ya kupata alama ya 389 katika mtihani wa KCPE na Alama ya B+ (KCSE) katika shule ya Mangu 2007.