• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:55 AM
Mwanamume ndani kwa kudaiwa kuiba za ndani

Mwanamume ndani kwa kudaiwa kuiba za ndani

NA MWANGI MUIRURI

MWANAMUME mmoja anayeshukiwa kuwa kinara wa wizi wa nguo za ndani za wanawake katika Kaunti ya Murang’a, ametiwa mbaroni katika mji wa Mukuyu.

Inadaiwa huwa anaziiba nguo hizo na kisha kuziuza kwa wanaume wasio na wake kwa Sh50 kwa kila mojawapo ya chupi hizo.

Nao wanaume hao inadaiwa huzitumia nguo hizo kujiridhisha hisia zao za kimwili kupitia kuigiza tendo la ndoa, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya polisi wa Murang’a Mashariki kuhusu operesheni hiyo, msako wa mshukiwa huyo ulizinduliwa baada ya kuripotiwa kwamba alikuwa akiendesha kashfa hiyo ya wizi wa chupi.

“Kupitia maelezo ya waathiriwa ambayo yalituwezesha kujichorea taswira ya maumbile ya mshukiwa, polisi walifanikiwa kumkamata Jumanne mchana,” ripoti hiyo inasema.

Baada ya kufumaniwa, kwake kulipatikana chupi 17 za wanawake wa unene tofauti, vifaa vya kielektroniki vya matumizi nyumbani zikiwemo televisheni, ala za kutoa muziki almaarufu woofer na pasi za kulainisha nguo. Aidha kulikuwa na baiskeli kadha.

Baadhi ya vitu vilivyopatikana ndani ya nyumba ya mshukiwa mbali na chupi. PICHA | MWANGI MUIRURI

“Pia, alipatikana na sindiria nane na baada ya uchunguzi zaidi, ikabainika kwamba yeye sio mchuuzi wa bidhaa hizo na pia hana mke au wasichana wanaoishi naye kuhalalisha uwepo wa mavazi hayo ndani ya nyumba yake,” ripoti hiyo yasema.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kainga Mathiu, mshukiwa huyo atasaidia wachunguzi kubaini kiini hasa chake kupatikana pia na visu, vingine vikionekana kama vilivyotumika kutekeleza uhalifu.

“Tunamchukulia kama mshukiwa hatari ambaye anayeweza kuwa kwa mtandao wa kufanya ushirikina,” akasema Bw Mathiu.

Mshirikishi wa muungano wa vijana eneo hilo, Bw Stephen Makau aliambia Taifa Leo kwamba wamepata dokezi kwamba mshukiwa huyo amekuwa akiuza chupi hizo kwa Sh50 kwa kila moja kwa vijana ambao hawajaoa na wana matamanio makali ya masuala ya chumbani.

Bw Makau alidai kwamba wanaume hao hutumia chupi hizo vitandani mwao kuiga tendo la ndoa ili kujiridhisha kimahaba.

“Niko na ushahidi kwamba hiyo ndio biashara ambayo huendelezwa ndani ya kashfa hiyo ya chupi. Vijana wengi na pia wazee wasio na wao wa kuwatuliza kimahaba, huzinunua na kisha kuzitumia kwa njia hiyo. Hilo ni suala linalofahamika mtaani,” akadai Bw Makau.

Bw Kainga alisema mshukiwa huyo amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Murang’a na ambapo wito umetolewa kwa waliopoteza chupi, sidiria na vifaa vya kieletroniki wafike hapo ili kutambua chao kilichopotea na hatimaye waandikishe taarifa za ushahidi dhidi ya mshukiwa.

Mshukiwa aliyetiwa mbaroni mjini Mukuyu kwa kupatikana na nguo za ndani za wanawake. PICHA | MWANGI MUIRURI
  • Tags

You can share this post!

Wa Iria akana shtaka la ufisadi wa Sh351m

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta atoa Sh2 milioni kusaidia...

T L