Mwanasiasa Chania aliyezuiliwa jela avutana na Kanisa kuhusu nyumba
MWANASIASA wa Kiambu Gladys Chania, aliyezuiliwa katika Gereza la Wanawake la Lang’ata tangu Oktoba 2022 kwa kuumua mumewe George Mwangi, amejipata katika mzozo mwingine na Kanisa la Jeshi la Wokovu kuhusu umiliki wa nyumba moja mjini Thika, Kaunti ya Kiambu.
Bi Chania, ambaye aliwania kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kiambu katika uchaguzi mkuu wa 2022, aliachiliwa kwa dhamana miezi michache iliyopita.
Yeye na mfanyakazi wake Maurice Mbugua wamekuwa gerezani tangu Oktoba 2022 baada ya kuhusishwa na mauaji ya Mwangi mnamo Oktoba 8, 2022 nyumbani kwake Mangu, Gatundu Kaskazini.
Mwili wake ulipatikana katika Msitu wa Kieni, Kaunti ya Nyeri.
Katika kisa cha sasa, Bi Chania sasa ameshtaki Kanisa la Jeshi la Wokovu, Thika, ambako yeye ni muumini, kwa kumfurusha kutoka kwa nyumba aliyotumia kama afisi za shirika lake, “Right At Home Rehabilitation Centre.”
Bi Chania anadai kanisa hilo lilimtimua kutoka nyumba hiyo miaka sita iliyopita, hata kabla ya kukamatwa kwake kwa tuhuma za kuua mumewe.
Mwaka jana, Chania na Mbugua walikana kuhusika na mauaji ya Mwangi.
Baada ya mwili huo kupatikana, Bi Chania aliwaambia wapelelezi kwamba Bw Mwangi aliondoka nyumbani kwake Mangu mnamo Oktoba 9, 2022 na hakurejea.
Baadaye wapelelezi waligundua kuwa Bw Mwangi aliuawa ndani ya nyumba yake kwani visu na nguo zilizotumika katika mauaji hayo zilipatikana ndani ya nyumba hiyo.
Bw Chania alikamatwa mara moja kama mshukiwa mkuu.
John Mwangi, aliyekuwa mfanyakazi wa marehemu na aliyekamatwa na kuzuiliwa kuhusiana na mauaji hayo, sasa ni shahihi wa serikali katika kesi hiyo.