MWANASIASA NGANGARI: Ushawishi wa Jaramogi Oginga ulivyonata katika siasa za Kenya
NA KENYA YEARBOOK
NI dhahiri kwamba Oginga Odinga alikuwa kigogo wa siasa za upinzani kabla na baada ya uhuru mnamo 1963.
Tangu wakati wa ukoloni, mwanasiasa huyo alijulikana kwa kuelezea misimamo yake bila kumwogopa yeyote.
Alikuwa kiongozi shujaa. Kinyume na wanasiasa wengine, Odinga alidumisha msimamo mkali kuhusu yale aliyoyaamini licha ya hali ilivyokuwa.
Alikuwa katika baraza la kwanza la mawaziri kama Waziri wa Masuala ya Ndani. Mnamo 1964, baada ya Kenya kutangazwa kama nchi huru, Mzee Jomo Kenyatta alimteua kuwa Waziri wa Masuala ya Ndani na Makamu wa Rais.
Hata hivyo, alijiuzulu mnamo 1966 baada ya kutofautiana na Rais Kenyatta.
Odinga alijiunga na upinzani mara tu alipojitosa katika ulingo wa siasa. Mnamo 1961, aliandikisha historia kama mwanachama wa kwanza wa Kanu kuondolewa chamani kama makamu wa rais kwa “kutoa matamshi yaliyoegemea mfumo wa kisoshalisti, kuwaunga mkono wagombea wasio wa chama na kuunga mkono vuguvugu la Kenya Action Group.”
Hatua ya kumwondoa chamani ilitangazwa na mwenyekiti wa chama hicho James Gichuru, baada ya kufanya mkutano uliodumu saa moja na Katibu Mkuu Tom Mboya.
Odinga aliamini kwamba ujamaa ndio ulikuwa mfumo bora zaidi wa kiuchumi kuwapa nguvu watu maskini.
Aliutaja kama njia pekee ambayo ingeleta usawa wa kimapato kati ya watu maskini na matajiri.
Odinga alizaliwa mnamo 1911, ambapo alisomea katika shule za upili za Maseno na Alliance. Alipenda masomo ya Hisabati na Historia. Alipenda mchezo wa magongo. Baada ya kumaliza masomo ya shule za upili, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, alikosomea diploma katika ualimu.
Baadhi ya watu aliosoma nao ni Godfrey Binaisa, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu nchini Uganda. Binaisa pia alihudumu kwa kipindi kifupi kama rais wa mpito wa taifa hilo. Odinga pia alisoma pamoja na Walter Odede, aliyekuwa daktari wa kwanza wa mifugo nchini.
Baada ya kumaliza masomo yake chuoni Makerere, Bw Odinga alipata kazi ya ualimu katika shule ya Maseno ambako alisomea.
Alikuwa akipanga kuendelea na masomo zaidi nchini Uingereza, ila mwalimu mkuu, Carey Francis akamwambia kwamba elimu aliyokuwa amepata ilimtosha kuwasaidia watu wengine.
Odinga alianza uanaharakati wake zamani. Alipokuwa akifunza shule ya Maseno, alikosoa mfumo wa kutumia majina ya Kiingereza. Aliacha jina lake la Kiingereza ‘Adonijah’ na kuanza kutumia Ajuma.
Kwenye wasifu wake Not Yet Uhuru (Bado Hatujajikomboa), Odinga anarejelea mapenzi yake kwa somo la Hisabati.
“Nilipenda kufunza Hisabati. Ningetumia muda wangu mwingi kuwasaidia wanafunzi kuhusu matatizo yaliyowakumba katika somo hilo,” akasema.
Alijitosa siasani na kuchaguliwa kuhudumu katika mabaraza ya ushauri ya Nyanza African District na Kata ya Sakwa kati ya 1947 na 1949. Alikutana na Mzee Kenyatta kwa mara ya kwanza mnano 1948 kupitia mpiganiaji uhuru Achieng Oneko.
Alikutana na Kenyatta mnamo Juni 1952 kabla ya kwenda kuhutubia mkutano wa chama cha KAU. Hali ya hatari ilitangazwa mnamo Oktoba 20, 1952. Viongozi 183 wa KAU walikamatwa na kuzuiliwa. Alikamatwa ila akaachiliwa baadaye.
Odinga alikuwa miongoni mwa viongozi wa kitaifa walioshinikiza kuachiliwa kwa Wafungwa Sita wa Kapenguria, akiwemo Mzee Kenyatta.
Mnamo 1957, alikuwa miongoni mwa Waafrika wanane waliochaguliwa Bungeni (LegCo). Waliochaguliwa pamoja naye ni Daniel Moi, Bernard Mate, Masinde Muliro, Katana Ngala, Lawrence Oguda na Joseph Murimi.
Mnamo 1960, Kanu ilibuniwa na akateuliwa kama naibu kiongozi huku, chini ya uongozi wa James Gichuru. Mboya alichaguliwa kama katibu mkuu.
Hata hivyo, tofauti zilibuka chamani mnamo 1966, baada ya katiba ya chama hicho kubadilishwa kubuni nafasi nane za umakamu wa rais. Odinga alihisi mamlaka yake yamepunguzwa, hali iliyomfanya kujiuzulu. Alibuni chama cha Kenya Peoples’ Union (KPU). Miongoni mwa waliojiuzulu pamoja naye ni Oneko na Bildad Kaggia.
Uhusiano wa Kenyatta na Odinga uliharibika zaidi mnamo 1969 baada ya wawili hao kuzozana katika mkutano mjini Kisumu wakati wa kufunguliwa kwa Hospitali ya Mkoa wa Nyanza ambapo ujenzi wake ulifadhiliwa na serikali ya Urusi.
Alitiwa kizuizini na kuachiliwa mnamo 1971. Masaibu yake hayakuisha. Mnamo 1977, alizuiwa kuwania nafasi ya naibu mwenyekiti wa Kanu baada ya uchaguzi huo kuahirishwa ghafla.
Mnamo 1980, Rais Daniel Moi alijaribu kumrejesha katika ulingo wa kitaifa kwa kumteua kama mwenyekiti wa kampuni ya Cotton Lint and Seed Marketing Board.
Hata hivyo, aliondolewa baadaye baada ya kuonekana ‘kuipinga’ serikali. Alirudi bungeni mnamo 1980 baada ya kuteuliwa kama mwenyekiti wa Bondo baada ya Hezekiah Ougo kujiondoa kwa hiari.
Mnamo 1982, yeye pamoja na mbunge George Anyona wa Kitutu Masaba walianza kubuni chama cha kuikabili Kanu. Wawili hao walikuwa wamefukuzwa chamani. Baadaye, aliwekwa katika kizuizini cha nyumbani.
Mnamo 1991, alijaribu kusajili chama cha kisiasa cha National Democratic Party (NDP) bila mafanikio.
Alikuwa miongoni mwa viongozi wa kisiasa waliobuni chama cha Ford ila kikagawanyika.
Mnamo 1992, Ford iligawanyika katika mirengo miwili; Ford-Kenya iliyoongozwa na Odinga na Ford Asili, iliyoongozwa na Ken Matiba. Kwenye uchaguzi wa 1992, Bw Odinga aliibuka wa nne kwenye kinyang’anyiro cha urais. Alichaguliwa kama mbunge wa Bondo baada ya kukaa miaka 23 nje ya siasa.
Alifariki mnamo Januari 1994 na kuzikwa nyumbani kwake katika eneo la Bondo. Alikuwa na wake wanne na watoto 17.