Makala

Mwanaume wa Kisii aliyetupa familia miaka 34 apatikana Baringo kaoa mke mwingine

Na KEN RUTTO October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NI katika mji wa Kabartonjo, Kaunti ya Baringo ambapo mzee mpotevu Bw Joseph Nyaanga Andima aliselelea, baada ya kutoweka machoni mwa familia yake kwa zaidi ya miaka 30.

Aliacha familia yake kaunti ya Kisii, mke na watoto watatu, na kuanza familia nyingine Baringo ambapo ana watoto watano.

Familia yake iliyomtafuta kwa udi na uvumba bila mafanikio, iliamua hali hiyo ipotelea pote walipokufa moyo kuwa huenda jamaa yao amefariki asijulikane alikofia.

Waliamua hivi baada ya kumsaka katika hospitali na mochari mbalimbali.

Tukipiga darubini nyuma, Bw Andima, akiwa na umri wa miaka 35, aliaga kwao nyumbani na kuzamia shughuli ya kusakatonge katika kazi za mijengo ya uwanja wa ndege wa Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Kisha baadaye akatokwa jasho akijenga barabara ya Kipsaraman, Bwawa la Kirandich na nyumba za ghorofa miaka ya tisini (1990s).

“Nilikuja maeneo haya miaka ya tisini kufanya kazi za ujenzi wa nyumba, uchimbaji visima, ujenzi wa barabara,” alieleza Bw Andima.

Katika pilikapilika zake za kutafuta unga, Bw Andima aliamua kuishi Kabartonjo.

Chambilecho, milima haikutani ila binadamu hukutana. Mmoja wa viongozi wa Kabartonjo Isaiah Andere alishirikiana OCS wa Loruk Moses Ondigi kuanzisha safari ya kumrejesha kwao Suneka Kaunti ya Kisii.

“Tuliwasiliana na mke wa hapa Baringo aliyetuambia kuwa hali ya mume wake imedhoofika. Ikabidi tuanze kutafuta jinsi ya kujua kwao nyumbani,” alisema Bw Andere.

“Nilishirikiana na OCS wa Loruk kwa ushirikiano na mke wake na tukawezesha ‘Mogaka’ akutane na familia yake ya kwanza.”

Baadhi ya wanakitongoji walipigwa na butwaa kuwa Andima alitoweka kwao na kuanza maisha mapya.

“Kumbe huyu jamaa alikuwa na mke na watoto wakubwa huko Kisii. Hatukujua hilo!” alishangaa jirani Stanley Kipkechem.

Baada ya haya kufichuka, habari zikaenea kama moto jangwani na kufikia jamaa yake huko Kisii. Andima akaanza kupokea simu kutoka nyumbani.

Alirejea nyumbani

Ilikuwa ni vifijo, nderemo, chereko na hoi hoi kijijini Kirwanda huko Bonchari Kaunti ya Kisii jamaa ya Nyaanga walipoandamana kwa nyimbo za furaha kumkaribisha nyumbani.

Mkewe Esther Andima aligubikwa na furaha kutahamaki kuwa mume wake, baba ya watoto wake, yu hai.

La kuzingatia kwake sasa, si eti bwana aliwatoroka, ni kwamba watoto wake watatu watamuona baba yao.

Bi Andima anavuta taswira nyuma na kusimulia masaibu aliyopitia yakiwemo ugumu wa kuwalisha watoto na kuwapeleka shuleni.


Miaka 34 iliyopita, Bw Andima aliacha familia yake changa na mkewe akabaki na mzigo mkubwa sana wa kuwalea watoto wanne ambao sasa ni watu wazima.

Hatimaye wamejumuika na kuyeyusha wingu jeusi la wasiwasi na huzuni.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan