Makala

MWANGI: Vijana wasisingizie ukosefu wa kazi nchini kuwa wazembe

August 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DAISY MWANGI

MIAKA iliyopita vijana walikuwa na bidii ya mchwa.

Wengi hawakusoma wala kuhitimu na shahada zozote, lakini walijitolea kufanya kazi za juakali na za kilimo. Azima yao ilikuwa kujipatia rikizi ya kila siku.

Kijana wa umri wa miaka 25,kwa mfano, alikuwa ashaoa ama kuolewa iwapo ni msichana. Hivyo alizimika kufanya kazi mchana kutwa ili kukimu mahitaji ya familia yake.

Yamkini hayo ni ya enzi hizo.

Siku hizi vijana wamekuwa wazembe ajabu. Licha ya wengi wao kupata elimu na kuhitimu vyema, hawataki kuchoka. Wanapopata kazi kwa mfano, wanachelewa kufika kazini kila siku, wanazembea kazini na hata kutokuwa tayari kufundishwa mambo mapya. Ndiposa utawapata vijana wa umri wa miaka 30 wakiishi na wazazi wao ili kuepuka kugharimika kwa njia yoyote ile.

Kila waamkapo, kazi yao ni kutazama filamu kwenye televisheni au kuzama kwenye mazungumzo ya muda mrefu na marafiki zao kwenye simu za mkononi. Wengi hawabanduki mitandaoni. Mbali na hilo, vijana hao hao wanapenda vileo kupindukia. Wataamka asubuhi na mapema kunywa pombe.Wanapopata pesa kidogo tu, wanaelekea vilabu kula ujana wao na kuponda raha.

Ingawa kuna uhaba wa kazi miongoni mwa vijana nchini, vijana hawafai kutumia kisingizio hicho kuwa wavivu. Wanafaa kujitolea kutafuta cha kufanya. Kwa mfano kuna ukulima.

Tatizo ni kuwa, vijana wengi waliosoma na kuhitimu hadi vyuo vikuu wanahusisha kilimo na uchafu.

Kazi yenyewe yaweza kuwa chafu lakini pesa zinazotokana na kazi yenyewe ni tamu.

Heri vijana wakome kuchagua kazi. Badala ya kuamka kila uchao kuketi sebuleni kuangalia runinga na simu mkononi kupekua mitandao, vijana wapasa kutafuta njia mbadala kujipatia riziki.

Nao wazazi wana jukumu kuwashauri wanao. Iwapo mwanao amefikisha umri wa kujitegemea, basi anapasa kuanza kujipigania binafsi. Wazazi wanapowalisha na kuwavisha vijana wa umri wa miaka hata zaidi ya 30, wanachangia uzembe wa vijana hawa. Vijana wanakosa sababu zozote za kufanya bidii kwa kuwa kila watakacho wanapewa.

Kama wewe ni tajiri, basi ni heri umfunze mwanao kufanya biashara ama umwajiri katika kampuni yako aweze kujitegemea.

Unapomwacha azembee na kumpa hela atakazo, ni kupalilia uvivu.

Na siku utakapoondoka, ataparamia mali yako na kuifuja kisha ateseke.Kwa hivyo wazazi tuache kuwapa wanetu samaki, bali tuwafunze kuvua.

Viongozi wa kidini pia wana jukumu la kuwazungumzia vijana.

Kuwaeleza kuwa uvivu haufai,hata kwenye Biblia Takatifu, asiyefanya kazi hafai kula.