Makala

Mwasisi wa wakfu wa kusaidia wale ndoa zao zinayumba

November 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

 

Na PETER CHANGTOEK

ALIPOAMUA kuolewa na maridhia wake wa moyoni, matarajio yake hayakuwa mengine, ila ni kuwa na maisha yasiyokuwa na farakano.

Hakujua kuwa mambo yangekuja kuenda segemnege, na maisha yake kumithilishwa na kaka tupu la yai, ambalo halina thamani hata kidogo.

Lakini maisha ya ndoa ya Bi Esther Kisaghu yalipogeuka, na kuwa lindi la machozi na majonzi, aliamua liwe liwalo, na kuondoka katika ndoa, na baadaye ukurasa mpya maishani, ukafunguka.

Aliliasisi Wakfu wa The Rose; shirika lisilokuwa la serikali, ambalo huwasaidia waathiriwa wa dhuluma za nyumbani, ambazo zimekuwa zikikithiri na zinaendelea kukithiri siku baada ya nyingine, si tu nchini Kenya, bali pia katika nchi nyingi duniani.

Anasimulia kuhusu mkasa uliompata, ambao nusra umwondoe duniani, pindi tu alipoolewa na muhibu aliyekuwa akimwamini na kumthamini kwa hali na mali na kwa dhati.

“Nilizipitia changamoto za binafsi. Mimi niliathirika na vita vya nyumbani nilipokuwa ndani ya ndoa. Nilianza kama msichana yeyote yule, ambaye anafurahia kuolewa. Tulipooana tu, kukawa na hali ya mabadiliko,’’ asema Bi Esther, akiongeza kuwa mumewe alianza kumfokea na kutomheshimu. Hapo ndipo masaibu yalipoanza kumwandama.

Mzawa wa Kaunti ya Taita Taveta, awali, Esther alisomea katika Shule ya Msingi ya Kilifi, walikohamia kwa sababu babaye alikuwa mwalimu, kisha akapandishwa cheo kuwa afisa wa elimu.

Kisha, alijiunga na Shule ya Upili ya Alliance, na baada ya hapo, akajiunga na chuo kikuu kimoja kule Marekani, kwa minajili ya kusomea shahada ya Usimamizi wa Biashara.

“Nilipofika katikati, mpenzi wangu akaniambia nirudi tuoane, nikaacha masomo katikati. Nilikuwa nimemaliza miaka miwili….. hiyo shahada haikukamilika,’’ anasimulia huku huzuni ikidhihirika dhahiri shahiri usoni pake.

Hata hivyo, baada ya kuoana, mambo hayakuenda jinsi alivyokuwa akidhani. Lo! Kumbe udhaniaye ndiye siye! Alidhani kuwa alikuwa amempata mpenzi wa dhati, lakini alishangaa ghaya ya kushangaa, alipoanza kudhulumiwa, kuteswa na kubezwa na mumuwe!

“Mwaka wa pili baada ya kuoana, alianza kuninyonga. Mimi nikanyamaza,’’ anasema Esther ambaye aliolewa akiwa na umri wa miaka 27.

Mambo yalipochacha, aliamua ima fa ima, na kujinasua kutoka kwa ulimbo uliokuwa umemnasa na kumbana.

“Nilipoona ndoa yangu imekumbwa na vita zaidi na zaidi, na naendelea kuteseka na mwanangu anaendelea kuteseka, nikatafuta namna ya kuondoka nchini kwa usalama wangu. Kwa vile niliona maisha yangu yalikuwa hatarini mume wangu alipojaribu kunidunga kisu, nikajua nimeona kifo. Katika hali ya kutafuta usalama, nikasema wacha niende chuoni Marekani nisomee shahada yangu ya pili,’’ anasema, akisisitiza kwamba hiyo ilikuwa hali ya kuondokea kifo kilichokuwa kikimkodolea macho!

Hivyo basi, akajiunga na Chuo Kikuu cha Boston, kusudi asomee shahada ya uzamili; Afya ya Umma zingatio likiwa Afya ya Kimataifa (Masters in Public Health – International Health).

Ni katika harakati yake ya kusomea taaluma hiyo ambapo aling’amua kuwa dhuluma za nyumbani zinaweza kuzuiwa.

“Katika hali ya kusoma miaka hiyo minne nilihakikisha nitasaidia watu nyumbani,’’ anadokeza.

Baada ya kukamilisha kusomea taaluma hiyo, Bi Esther, ambaye ni mzazi wa mtoto mmoja wa kiume, alirejea humu nchini, na kuufungua ukurasa mpya maishani kwa kuasisi ‘The Rose Foundation’.

Azma yake ilikuwa kuwahamasisha watu kuhusu uzuiaji wa dhuluma za nyumbani.

“Nikiwa mwanzilishi wa ‘The Rose Foundation’, nimekuwa na huo msukumo kuongea juu ya vita vya nyumbani ili niwasaidie wale waathiriwa wamenyamaza, wanaoogopa kuongea juu ya vita vya nyumbani kwa vile wanaona hakuna usaidizi wowote,’’ asimulia mwasisi huyo.

Amekuwa akiwahamasisha waja, hususani vijana, kuhusu uzuiaji wa dhuluma za nyumbani kupitia kwa mafunzo na warsha mbalimbali. Hali kadhalika, amezipeleka kampeni hizo makanisani, japo anasema kuwa makanisa yamezipokea kampeni hizo kwa mtazamo hasi.

Anasema kuwa watoto wengi huathirika mno kisaikolojia wanapoona dhuluma hizo zikiendelea nyumbani.

“Asilimia 60 ya watoto 10 wa kiume waliokumbwa na dhuluma nyumbani, wakiwa watu wazima, wakioa, pia upo uwezekano watakuwa wa kudhulumu,’’ anafichua.

Msamaha

Anasisitiza kuwa ni jambo aula kwa wale waliodhulumiwa katika ndoa kuwasamehe wale waliowatendea dhuluma hizo. Hata hivyo, anawasihi waliosamehewa kuwajibika ipasavyo.

Mwanzilishi huyo wa shirika hilo lisilokuwa la serikali anasema kuwa ana mipango ya kuzifikisha huduma zake katika kaunti zote nchini.

“Shirika la ‘The Rose Foundation’ limeanza majadiliano na Kaunti ya Taita Taveta…… kwa dhuluma za kijinsia, Taita Taveta ni namba tatu. Halafu tukiona tumeimarika vizuri (hapa) Kenya, tuangalie mataifa jirani….. kufunza mataifa mengine kwamba tunaweza kuzuia vita vya nyumbani,’’ anafichua.