• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Mwathiriwa asimulia jinsi shambulio garini lilivyomuacha na ulemavu

Mwathiriwa asimulia jinsi shambulio garini lilivyomuacha na ulemavu

NA FRIDAH OKACHI

WAATHIRIWA wa ajali iliyosababishwa na vilipuzi vya magaidi kwenye barabara kuu ya Thika Superhighway mnamo Mei 4, 2014, wanapoteza matumaini ya kupata fidia baada ya idara husika kuwaeleza kuwa bado pesa hizo hazijpatikana.

Idara hiyo inasema mmiliki wa gari lililohusika kwenye ajali hiyo hajajitokeza.

Bw Simon Kinyua, mkazi wa Kahawa Sukari alipoteza jicho moja na kupata ulemavu katika mguu mmoja baada ya kemikali ya vilipuzi kusaga nyama ya mguu, hali iliyolazimu yeye kukatwa mguu.

Mwaka mmoja baada ya tukio hilo kufanyika, Bw Kinyua alijua angepata fidia kutoka kwa serikali au mmiliki wa gari ambaye kufikia sasa bado hajawahi kumwona.

Bw Kinyua analalamikia kuzungushwa kutoka idara moja hadi nyingine licha ya waliotekeleza tukio hilo kufungwa jela.

“Nina familia inayonitengea. Nilipoteza mguu na jicho la kulia baada ya mlipuko huo. Magaidi walioshtakiwa na kupatikana na hatia walifungwa jela ila sisi tuko tu,” akasimulia Bw Kinyua.

Miaka 10 iliyopita, Bw Kinyua alijipata akiwa amelazwa hospitalini, hii ikiwa ni baada ya gari alilotumia kusafiri kutoka mjini kulipuliwa.

Siku hiyo alikuwa mwingi wa matumaini angefika kwa nyumba na kukutana na familia yake iliyokuwa inarudi mjini kutoka mashambani – Ukambani.

Visa vya vilipuzi hivyo vilikuwa vimezidi na hivyo serikari ilikuwa imetoa masharti kila abiria kukaguliwa.

Baba huyo wa watoto watatu, alieleza Taifa Jumapili kwamba wakati wa ukaguzi, mizigo iliyokuwa ikiwekwa ndani ya matatu haikuwa inakaguliwa.

Na hatima yake ya kukutana na familia yake ilibadilika mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

“Safari ilianza ambapo kwa kawaida watu walishuka na kupanda. Kufika Roasters, gari lililipuka. Kwa dakika kadha, sikusikia kilichoendelea. Kisha nikaamka na kuona baadhi ya abiria wanashuka huku wakipiga kamsa,” akaeleza.

“Tulibaki ndani ya gari sisi abiria kadha… Nafiri walidhani tumekufa. Nilipiga nduru nikitaka kunusuriwa. Nilipotazama mguu wangu wa kulia, niliona mifupa pekee,” akaongeza.

Manusura huyo anasema msamaria mwema alijitolea na kuwapeleka katika hospitali ya St Francis-Mwiki.

Anaeleza kuwa akiwa kwenye lile gari, alikuwa akiona moshimoshi tu hadi alipofika katika hospitali.

“Macho yangu yalisalia kukodoa kodo bila kuona chochote. Niliposikia sauti ya daktari, nilimuuliza, ‘huu uchungu utaisha saa ngapi?’ naye daktari akanifahamisha kuwa muda sio mrefu ningekuwa naingizwa kwenye chumba cha upasuaji,” akakumbuka matukio jinsi yalivyojiri siku hiyo ya shambulio.

Bw Kinyua alipelekwa kufanyiwa upasuaji bila jamaa yake kufahamu alikokuwa.

Mkewe, Bi Edith Kinyua, aliyekuwa ameshafika mjini jioni ya ajali akitoka ‘ushago’, alikesha usiku kucha bila kufahamu alikokuwa.

Bi Edith Kinyua ni mkewe Bw Simon Kinyua aliyepata majeraha kwenye shambulio la kigaidi garini. PICHA | FRIDAH OKACHI

Asubuhi iliyofuata, aliona ni vyema kufika kwenye eneo la tukio ili kumtafuta mumewe. Alikuwa amesikia katika vyombo vya habari.

“Kabla ya kusikia taarifa kuwa kuna gari lilipuka barabarani, nilikuwa nimezungumza na mume wangu ambapo alikuwa amenieleza tungekutana nyumbani. Sasa nilipofika Nairobi na kumpigia simu bado alikuwa hapokei simu,” akasema Bi Kinyua.

Alijawa na wasiwasi kila wakati alipopiga simu ya mumewe na kupata hapatikani.

“Asubuhi nilipiga na kupata ni mteja. Nilifika katika eneo la tukio na kufahamishwa waathiriwa walipelekwa katika hospitali hii na ile. Hatua ya kuanza kumtafuta ilianza katika hospitali ya St Francis ambapo nilimpata,” akasimulia mke huyo.

Mvutano kati ya serikali na hospitali hiyo ya kibinafsi ulianza.

Serikali ikitaka waathiriwa wote kupelekwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH).

Mvutano huu ulitokea pindi tu serikali ilichelewa kulipa hospitali hiyo ya kibinafsi. Wakati huo, Bw Kinyua alitarajiwa kufanyiwa upasuaji wa jicho.

“Hapa ndio drama ilianza… kumbuka daktari amenieleza kuwa jicho la upande wa kulia halina uwezo wa kuona. Lile la upande wa kushoto linaweza kurekebishwa kupitia upasuaji baada ya kemikali za vilipuzi kutatiza mishipa. Afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Kasarani aliingilia kati na hivyo tukapata uhamisho,” akasema Bw Kinyua.

Wiki moja baadaye, mwathiriwa huyo alikuwa hajafanyiwa upasuaji wowote. Hii ni baada ya serikali kugharamikia kwa kulipa bili ya Sh45,000 pekee. Bili hiyo ilifanya usimamzi wa hospitali hiyo kuwataka wagonjwa kupewa chaguo la kujisajili upya.

“Siku hiyo nilitoka hospitali nikiwa na wasiwasi wa kupoteza jicho ambalo bado sikuwa nimefanyiwa upasuaji. Nilijua uwezo wa kuona ungepotea lau singeshughulikiwa mapema,” akaeleza.

Hata hivyo alitafuta huduma za matibabu katika hospitali ya kibinafsi iliyomsaidia kupata kuona tena.

“Pandashuka za pale KNH zingenipotezea uwezo wa kuona kabisa. Rafiki alijitokeza na kunipeleka hospital ya kibinafsi iliyonisaidia kupata kuona kwa jicho moja,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mnyama Haaland ‘aua Arsenal’ kwa kuongoza Man City...

Wakazi Lamu waona faida za njia za cabro walizodharau

T L