• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
MWITHIGA WA NGUGI: Kenya yahitaji tiba ya kudumu si siasa hizi za ubinafsi

MWITHIGA WA NGUGI: Kenya yahitaji tiba ya kudumu si siasa hizi za ubinafsi

Na MWITHIGA WA NGUGI

KWA muda sasa tangu uchaguzi wenye utata wa mwaka 2017, mawimbi mengi ya kisiasa yamekuwa kama busu tamu la kisiasa, lenye kuleta mahasimu wa kisiasa karibu.

Mnamo Jumanne, tulishuhudia harakati ya kukabidhi Rais Uhuru Kenyatta ripoti ya jopo la Muafaka wa Maridhiano (BBI) inayotarajiwa kuleta uwiano zaidi kitaifa na pia kuzuia mikwaruzano na ghasia za kisiasa na hususan ambazo hushuhudiwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Ni bayana kwamba tangu tulipoikitisha demokrasia ya vyama vingi na kutupilia mbali chama kimoja dhalimu, mengi machungu wameyapitia Wakenya walipa ushuru.

Ndiposa hata sasa, nashindwa kuelewa kama kweli ripoti ya ‘salamu za heri’ kweli zitatatua matatizo ya Wakenya.

Wapokot kwa sasa wanalia mafuriko na maafa ya makumi kama si mamia, na isisahaulike wakati wa kiangazi ujapo wao watakuwa wa kwanza kulia kwa kiu na njaa.

Lakini swali ni je, kwa nini hatuna sera au hata mikakati ya kutuwezesha kuyakabili majanga yanayowazonga kila leo?

Hapa tunaona kuwa tungali kwenye ‘mtego mkuu wa kisiasa’.

Lakini hata hivyo, viongozi waliochaguliwa hawafai kugawanya Wakenya kwa misingi ya ukiritimba wao.

Wakenya wanachotaka ni kuona demokrasia yetu ikikua, na kukihakishia kizazi cha kesho uwepo wa mwanya wa watoto wa masikini kukaa meza moja na ‘walala hai’ wenye nguvu na mamlaka.

Ama kweli, mashinani wengi wanalia.

Kwa mfano, niko karibu na boma la rais wetu Uhuru Kenyatta, mamia ya vijana hapa hawana kazi na hata wengi wanajuta kwa nini walimchagua, na ndiposa nauliza, hii BBI ni ya kuwatoa Wakenya kwenye lindi la umasikini au ni kuhusu kuwapa wanasiasa fisadi nafasi ya kuendelea kuunajisi uchumi wa nchi yetu?

Wakenya wanafaa kuukubali ukweli mmoja, siasa za Kenya ni udanganyifu mtupu, uongozi wa nchi umefanywa biashara na mirathi, yaani mwanasiasa akifa ni sharti mtoto wake awe kiongozi hapa au pale.

Wakenya wanachohitaji kwa sasa si mambo ya kugawana mamlaka na wala si nani atakayekuwa rais baada ya yule anayekalia kiti kwa sasa.

Wakenya wenzetu kule Pokot wanasombwa na maji na makumi hawajulikani walipo, serikali inaonekana kujikokota kuwanusuru wenzetu.

Kwa kifupi, Wakenya hatufai kupigana kwa sababu ya mamlaka na uongozi wa nchi.

Kwa hivyo, itabidi kila mmoja wetu aiangalie nchi yetu kwa jicho pevu na kuacha tamaa za siasa za kujitajirisha kwa jina la uhusiano na rais wa nchi.

Lakini hata hivyo, siku ya kufa kwa nyani miti yote huteleza na ndiposa naamini kitendawili cha BBI kitawapiga chenga matapeli wengi wa kisiasa hatimaye.

 

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Heko Wanyama kuanzisha wakfu

Black Junior FC yazidi kujiimarisha mashinani

adminleo