MWITHIGA WA NGUGI: Masaibu yetu kama nchi ni mwiba wa kujidunga wenyewe
Na MWITHIGA WA NGUGI
TANGU minong’ono ya kuibadilisha Katiba yetu ianze miezi kadha iliyopita, mengi ama kweli yamekwenda kombo.
Mnamo 2010 Wakenya wengi walijawa na furaha huku wakijua fika kwamba, Katiba yenye kuzingatia ugatuzi hatimaye ingehakikisha ugavi sawa wa asilimali za nchi ungefaulisha ndoto za Wakenya.
Lakini tunachosikia kila uchao ni wizi wa mali ya umma na ufisadi wa kiajabu.
Leo hii ninachoona kupitia darubini ya uzalendo ni ubomozi wa uchumi badala ya ujenzi.
Wakenya wanalia ukosefu wa maendeleo, ukosefu wa dawa hospitalini na njaa inayowaponza wengi kutokana na umasikini na ukosefu wa ajira.
Ninachojaribu kutafakari kila uchao ni iwapo Wakenya wanachohitaji ni mageuzi ya kikatiba ama ni kutafuta suluhu ya mahitaji yao ya kimsingi.
Kinachothibitika wazi ni kwamba, wanasiasa wanachofanya ni kujitafutia makuu wanapopata nafasi, nia yao kwa kifupi wanacholilia ni maslahi yao ya kibinafsi ya kupata viti vikuu na mamlaka.
Kila siku, kama taifa, tunapoteza wakati mwingi tukizichapa siasa, mara siasa za urithi wa urais na kampeni za 2022, jambo ambalo limefanya ukungu tusifaulishe miradi ya maendeleo wala kuvishinda vita dhidi ya ufisadi nchini.
Ni uchungu mwingine zaidi kuona kaunti zetu zikipigania ongezeko zaidi la fedha, ilhali wananchi hawajapata maelezo faafu kuhusu matumizi ya mgao wa hapo awali.
Badala ya kuzisikiliza kelele nyingi za wanasiasa na utapeli wao, wanachofaa kukumbushwa ni kuwa, mjinga akierevuka mwerevu huwa mashakani.
Nchi yetu kusema kweli imeshindwa kujikwamua kutoka tope la umaskini, kutokana na ulafi wa viongozi wachache waliotwikwa mamlaka na ‘Wanjiku.
Katika kaunti nyingi, wananchi wanalalamikia ubadhirifu na ufujaji wa pesa za umma.
Ikumbukwe juzi ya Mungu, Rais alifutilia mbali ujenzi wa bwawa la Kimwarer, kutokana na utapeli na udanganyifu katika utekelezwaji wake.
Je, ni hadi lini kama Wakenya tutaendelea kukaa kimya wakati uchumi wetu unanajisiwa na wachache wenye nguvu na mamlaka na kuwaacha Wakenya wengi kwenye lindi la umaskini?
Wakati umefika kwa wapiga kura kuzinduka na kufikiria mara mbili kabla ya kuwachagua viongozi wao. Kuchaguana kikabila au kufuata mawimbi ya vyama vya kisiasa ni wazo finyu ambalo limetuletea matatizo si haba.
Wakati ni sasa, kuanzia kaunti ya Kiambu, Nairobi, Mombasa na kwingineko, Wakenya hebu waamke na kila wakati wachague viongozi bora wala si bora tu viongozi, ili tujiepushe na kilio cha muiba wa kujidunga.