Mzozo wa familia Kisumu uliosababisha mauti na kifungo cha miaka 60 Jela
RUSHDIE OUDIA NA LABAAN SHABAAN
HII ni simulizi ya familia tatu zilizounganishwa na upendo na ujirani mwema lakini zikasambaratishwa na tukio la mauaji yaliyovuruga uhusiano kabisa.
Ni juma moja tangu Mahakama ya Kisumu kumhukumu Bw Joseph Ayomo, 30, kifungo cha miaka 40 jela kwa kumuua Bi Beverly Akinyi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Akinyi aliyekuwa na umri wa miaka 21, alikuwa mchumba wake Bw Evans Aloyo Otieno ambaye ni kaka wa kambo wa Ayomo.
Kabla ya hukumu juma lililopita, Bw Ayomo tayari alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 20 baada ya korti ya Winam, Kisumu kumpata na hatia ya jaribio la mauaji.
Bw Ayomo alimdunga kisu kaka yake Aloyo mara 21 kabla ya kumchinja koo. Ilionekana miujiza kwa mwathiriwa kuponea shambulio hili hatari.
Lakini tukio hilo la Julai 24, 2018 na mchakato wa korti wa miaka 6 umegeuka kuwa kizungumkuti kwa familia hizi mbili na ile ya Ayomo.
Katika kipindi chote cha kesi kortini, familia za Ayomo na Aloyo zilitengana.
Mshikamano thabiti uliounganisha familia hizi mbili kwa miaka ishirini ulimalizwa na mauaji ya Beverly.
Taifa Leo imebaini kuwa familia hizi zilikutana mapema miaka ya 1990 wakiwa majirani mtaani Makogilo katika mitaa ya mabanda ya Manyatta, Kisumu.
Bw Aloyo alikuwa angali mdogo na hakuwa amejiunga na shule ya msingi.
Bw Ayomo alikuwa mzaliwa wa nne katika familia ya watoto sita huku Bw Aloyo akiwa mtoto wa kipekee wa mama ambaye alikuwa mke wa kwanza wa marehemu James Otieno aliyefariki 1996.
Mtoto wa kipekee
Aliacha familia ya wake zaidi ya mmoja ambayo ilikuwa na umoja.
Aloyo alieleza kuwa, licha ya Ayomo kuwa kaka yake wa kambo, alijitolea kumsaidia pamoja na ndugu zake wawili.
Aliwakuta wakiishi maisha magumu Nairobi.
Wake wawili wa marehemu Otieno, Dolly Achieng na mke mwenza Mary Otieno pia waliishi kwa amani.
Baada ya mume wao kufariki, Dolly ambaye alikuwa mwanabiashara shupavu, alifungua biashara ya vifaa vya ujenzi kwa faida ya Mary eneo la Wang’arot, Kaunti ndogo ya Seme.
Lakini mahojiano na familia hizi mbili yalifichua hali ya taharuki na uhasama ulioletwa na ushindani wa mali.
Katika kipindi cha kesi mahakamani, Dolly na mwanawe Bw Aloyo walikaa mbali na nyumba yao ya mashinani hadi Desemba mwaka jana.
Kila mara familia hizi zilipokutana katika Mahakama Kuu jijini Kisumu, hawakusalimiana ama kuangaliana ana kwa ana.
Ndani ya mahakama, walichagua kuketi mbali mbali. Kikao kilipokamilika, familia moja ingesubiri nyingine itoke kwanza ili wasikutane kwenye barazani.
Jaji wa Mahakama Kuu Roselyn Aburili alipotoa hukumu ya kifungo cha miaka 40 kwa Bw Ayomo, mama yake Mary alitazama sakafuni huku bintiye Violet akiwa amejifunika uso akilia.
Alionekana ameamini kuwa laana ya ugomvi mbaya wa familia ilikuwa imemtupa mwanawe gerezani.
Mauaji yatia doa uhusiano
Bw Aloyo alithibitisha kuwa tukio hilo la mauaji lilitia doa uhusiano wake na kaka yake wa kambo na familia nzima.
Kwake, ilikuwa ni kesi ya usaliti, kutokuwa na shukrani na maswali mengi yasiyo na majibu.
“Huyu ni mtu niliyemsaidia alipokuwa mdogo, nikamnunulia viatu na kumrudisha Kisumu 2009. Nilimchukua na hadi leo sielewi ni kwa nini alifanya alichofanya,” alisema Bw Aloyo.
Mfanyabiashara huyo alisema tukio hilo lilibadilisha kila kitu katika familia.
Hata jitihada za kushughulikia suala hilo ziligonga mwamba sababu ya kutoaminiana.
“Tuliangazia uwezekano wa kushughulikia suala hili kwa njia tofauti tukiwa familia, lakini baadhi ya ndugu zangu walisisitiza kwamba tuende mahakamani. Kwa kweli kulikuwa na bado kuna mvutano kati yetu kama familia kwani maswali mengi yamesalia bila majibu,” akasema Bw Aloyo.
Marehemu Bw Otieno alikuwa tajiri aliyemiliki mijengo. Alimiliki nyumba za kukodisha Manyatta, Nyalenda, Sky Way, Siaya na Ringa kaunti ya Homa Bay.
Baada ya hukumu kutolewa, Mary alihusisha kesi ya mahakama na mzozo wa mali kati ya familia ya mke mwenza na familia yake.
Yeye pamoja na binti zake pia walishikilia kuwa Bw Ayomo hakumuua Beverly wala hakumshambulia kaka yake wa kambo.
“Mwanangu alihukumiwa bila kufuata haki. Hii ni njama ya na kisa cha ugomvi wa mali. Mimi na watoto wangu tumenyimwa udhibiti wa mali ya marehemu mume wangu. Ushahidi uliotolewa mahakamani ulionyesha wazi kwamba mwanangu hakuwa karibu na eneo la mauaji. Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi huu,” akasema Bi Otieno.
‘Njama na kisa cha ugomvi wa mali’
Taifa Leo ilimuuliza Bw Aloyo ikiwa kulikuwa na mgogoro wa umiliki wa mali ambao ungeweza kusababisha mauaji ya Beverly.
Aloyo alishangaa akiuliza ni kwa nini mamake wa kambo hakuwahi kuangazia suala la mali.
Caren Anyona hajawahi kuelewa kwa nini bintiye wa pekee alifariki mikononi mwa watu waliolelewa pamoja, watu aliowapenda na kuwapenda sana.
Bi Anyona na marehemu binti yake Beverly waliishi upande wa pili wa ua kutoka kwa familia ya Dolly tangu mapema miaka ya 1990.
Anakumbuka jinsi hata baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu na kuanzisha biashara iliyofana Kisumu, Bw Aloyo bado angerudi Makogilo kumtembelea mama yake.
Bi Anyona alihamia mtaa wa Elgon Estate kwenye Barabara ya Kibos na ndiye aliyemjulisha Bw Aloyo kuhusu nyumba ambayo ilikuwa wazi katika eneo hilo hilo, wakati mfanyabiashara huyo alipokuwa akitafuta nyumba.
Ni wakati huo ndipo alipokutana na Beverly ambaye alimwita Cassie, na ua la maisha yao ya uchumba yakachanua japo kwa siri.
Bw Aloyo alikaa hapa kwa muda mfupi kabla ya kuhamia mtaa wa Aliwa Estate karibu na eneo la Car Wash ambapo Beverly angekutana na mauti yake baadaye.
Asimulia kwa uchungu
Bi Anyona alisimulia mahakama kwa uchungu jinsi alivyopata tu kujua kuhusu uhusiano wa bintiye na Bw Aloyo baada ya kupigiwa simu kuarifiwa kuhusu mauaji yake.
“Nilijua binti yangu alikuwa katika Chuo Kikuu cha Kenyatta wakati wa kifo chake. Sikujua hata wawili hao walikuwa kwenye uhusiano na hakuwahi kuniarifu kuwa yuko Kisumu. Laiti angalinifahamisha alikuwa Kisumu, pengine angalikuwa hai leo,” akasema Bi Anyona.
Anyona aliambia Taifa Leo jinsi kifo cha mtoto wake kilivyomtia kiwewe na kudhoofisha hali yake ya afya kwa kupata vidonda vya tumbo na shinikizo la damu.
Aliambia mahakama jinsi alivyomlea bintiye akiwa pekee yake na kwamba Beverly aliahidi kumjengea nyumba baada ya kukamilisha elimu ya chuo kikuu na kupata kazi.
Kwa mujibu wa Hakimu, Bw Ayomo hakuonyesha majuto yoyote kwa uhalifu aliofanya wala hakuonyesha huruma kwa familia ya marehemu.
Hili ndilo lililomkasirisha Bi Anyona. Alishutumu familia ya Bw Ayomo, ambayo alikuwa ameijua kwa miongo kadhaa, kwa kutoomba msamaha wala kusikitikia chochote kilichojiri.
“Nina huzuni kwamba ni familia ile ile nimekuwa karibu nayo tukishiriki mambo mengi ambayo iliua binti yangu,” alisema Bi Anyona.
Ijapokuwa alihisi ametulizwa kwamba haki, ingawa ilicheleweshwa, ilikuwa imetolewa, bado alitamani mahakama itoe hukumu kali zaidi kwa muuaji wa binti yake.
Kwa hali ilivyo bado haijabainika iwapo kifo cha Beverly kilipangwa au kama alikufa katika tukio la ajali wakati wa ugomvi wa kifamilia uliodumu muda mrefu.