Nabii aliyeleta ‘yesu’ Kawangware afariki
MWILI wa nabii Sinaida Mary Akatsa almaarufu Dada Mary wa Kanisa la Jerusalem Church of Christ, Kawangware, Nairobi aliyeaga Oktoba 26, 2024, unatarajiwa kusafirishwa hadi Kaunti ya Kakamega Jumapili usiku Novemba 3, 2024.
Kulingana na mmoja wa familia yake aliyezungumza na Taifa Dijitali, alisema Dada Mary alifariki akipokea matibabu ya figo baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Dada Mary alipata umaarufu mwaka 1988 baada ya kumleta jamaa mwenye asili ya Kiasia, mtaani Kawangware. Alieleza wafuasi wake kuwa jamaa huyo alikuwa Yesu Kristo jambo ambalo lilipingwa na watu wengi.
Aliyekuwa mfuasi wake Francis Kirato alielezea Taifa Dijitali kuwa yesu huyo bandia alikuwa mrefu. Alitembea miguu tupu na kuvalia mavazi meupe.
Alisema jamaa huyo aliketi upande kulia wa Akasta wakati wa ibada huku akiwa amefunga kitambaa cheupe kwenye kichwa chake.
Pia, waliazimika kumwabudu na kumwelezea shida zao.
“Tulilazimika kupaza sauti zetu na kumuita Yesu wa Nazareti, Yesu wa Nazareti amekuja, tunaomba utuondolee dhambi zetu,” alitabasamu Bw Kirato.
Kulingana na Bw Kirato, jamaa huyo alizungumza nao lugha ya Kiswahili katika mikutano ya Jumatano, Ijumaa na Jumamosi.
“Baada ya mwezi mmoja, jamaa huyo alikuja kuchukuliwa na mwezake pia ambaye alikuwa mzungu na kuenda. Tuliamini alikuwa akirudi mbinguni,” aliongeza Bw Kirato.
Nabii Akasta alikuwa miongoni mwa wahubiri wa kike wa nchini.
Alifungua kanisa lake Kawangware karibu na eneo la Waislamu almaarufu Muslim katika miaka ya 1980 kabla ya kuhamia Kawangware 56 katika miaka ya 1990.
Mshiriki mwingine ambaye amehamia Kanisa la PAG, Kawangware 56, Margret Nasa Wambua, anasema alimjua Dada Mary mwaka 1988.
Bi Wambua anaamini maombi ya nabii huyo yalimfanikisha kupata watoto wengine watano.
“Dada Mary alikuwa mtu wa kawaida, alikuwa akija kwangu hapa. Siku moja alinieleza sababu yangu ya kukosa kuzaa ni kufungwa na yule mkunga alinizaisha mtoto wa pili. Nilikuwa nimeishi miaka mitano bila mtoto. Lakini wakati aliniombea nilipata ujauzito,” alisema Bi Wambua.
Miongoni mwa kanuni ambazo wafuasi wa Jerusalem Church of Christ walifuata ni kuvaaa mavazi marefu haswa kwa wanawake. Nabii huyo alidai kuwa kuvalia mavazi hayo yangezuia wachawi kuwaroga.
“Nilipopata mimba baada ya muda mrefu, Dada Mary alinieleza kuwa nivae nguo ndefu ili yule mkunga alinifunga asijue nina mimba. Na kupitia mavazi hayo nilijifungua watoto wengine watano mwaka baada ya mwingine,” alisema Bi Wambua.
Alihamisha kanisa hilo kutoka mtaa wa Muslim hadi Kawangware 56, baada ya Nabii huyo kununua kipande cha ardhi ambayo kuna uwanja mkubwa.
“Huo uwanja tulikuwa tukikimbia huku ukimwambia Mungu wako shida zako. Kama mimi nilizunguka uwanja huo mara 23 nikiomba mwanangu apone na akapona.”
Mwaka wa 1993, Dada Mary alianza kuuza vitu kadhaa kwenye madhabahu akidai kuwa ameviombea.
Hali iliyochangia Bi Wambua kutafuta huduma za kanisa la PAG.
“Nilishamgaa kwenda kanisani na nabii akaanza kutuuzia nguo, vyakua miongoni mwa vitu viingine ambavyo alidai ameombea. Hapo ndio niligundua roho alitoka ndani yake,” alisema Bi Wambua.
Katika mtaa wa Kawangware na Muslim, wanawake waliopata ujauzito baada ya kuombewa wa Dada Mary, walipewa agizo la kuwaita wanao wa kike Sinaida, Mtoto wa Kiume akiitwa Francis (jina la mumewe ambaye ni marehemu).
Akatsa alipata umaarufu mkubwa kwa kuwapiga makofi waumini waliochelewa kufika kwenye ibada zake.
Aliwaagiza wengine kulipa faini na kupiga magoti nje.
Nidhamu yake kali na mazoea yasiyo ya kawaida mara nyingi yalivutia ukosoaji haswa kwa kuagiza wanaume waliokosea wake wao kuvalia chupi za wanawake kichwani.
“Nilifedheheka sana siku moja mke wangu kunishtaki kwake na kunieleza nivalie chupi kichwani,” alisema mkaazi mwingine.
Akasta alizaliwa eneo la Bunyore, Kaunti ya Vihiga.