NAROK: Eneo ambako ndugu huoza dada zao bila kuchukuliwa hatua
Na BENSON MATHEKA
WATOTO wasichana eneo la Olpusimoru, Kaunti ya Narok wanakabiliwa na hatari ya kuozwa mapema na ndugu zao bila kuchukuliwa hatua na yeyote, uchunguzi wa Taifa Leo umefichua.
Wanaume hao wanaogopewa hivi kwamba hakuna anayethubutu kupinga hatua yao, wakiwemo wazazi wao wanaokumbatia mila na utamaduni zao kwa dhati.
Kwa wanaume hao, msichana ni mali inayofaa kuuzwa wakati wowote mtu akipenda, hata kama ni kumbadilisha na mifugo wachache.
Vijana hao wanaogopewa sana hivi kwamba wanaharakati na maafisa wa utawala ambao wasichana hao hukimbilia kupata hifadhi ili wasiozwe mapema kwa wazee wa rika la mababu wao, wanaishi wakihofia maisha yao.
Lakini kwa Pasta Stella Kerema na mumewe, ni lazima desturi hii ikomeshwe kwa vyovyote vile. Stella anahofia kwamba maisha ya wasichana katika eneo la Olpusimoru yataathirika iwapo wakazi hawatabadilisha tabia.
“Kama kuna yeyote anayejali maisha ya mtoto msichana, anafaa kufika hapa na kupigana kwa jino la ukucha kuzima desturi hii iliyopitwa na wakati,” alisema.
Mhubiri huyo amefaulu kuwaokoa wasichana wanne waliokuwa wamepangiwa kuozwa wakiwa na umri mdogo na kuhakikisha wanaendelea na masomo yao.
“Huwa wanakimbilia katika kanisa ninaloongoza nikiwa na mume wangu. Siwezi kuwafukuza licha ya upinzani kutoka kwa jamii,” anasema.
Juhudi zake hazijaungwa na shirika lolote la serikali, mashirika ya kutetea watoto au baadhi ya maafisa wa utawala katika eneo hilo. Anatoa mfano wa kisa kimoja ambapo ndugu wa msichana aliyetorokea kwake ili asiozwe walivamia nyumba yake.
“Mnamo Juni 6 2017, nilipiga simu kwa Childline Kenya kupitia nambari ya kuripoti dhuluma kwa watoto 116 kwamba msichana mwenye umri wa miaka 13 aliyepata alama 270 kwenye KCPE alikuwa akiozwa na ndugu yake kwa mwamamume mzee,” alisema Bi Stella.
Kwenye maelezo yaliyonakiliwa na Child Line Kenya, hakufichua jina la mwanamume huyo kwa kuhofia maisha yake.
Anasema siku moja kabla ya kupiga simu hiyo, mwanamume huyo alikuwa ameongoza wanaume wengine kuvamia nyumba yake kumsaka msichana huyo alipopata habari kwamba alikuwa amekimbilia huko.
Kulingana na ripoti ya Childline Kenya iliyopokelewa Juni 6, 2017, wazazi wa msichana huyo ni wazee na walikuwa wakiishi Mazelek Tanzania, mwanao alipopanga kumuoza dada yake.
“Baba ni mzee sana na aliacha mali yake kwa wanawe na ni wao waliopanga kumuoza kwa mzee anayefahamika kama Julius Lolgeso kutoka Nadoshoge, Tanzania,” Bi Stella alisema.
Mumewe alipouliza wazazi wa msichana huyo kwa nini hawakutaka kumpeleka shule ya upili, walidai hawakuwa wamepata shule ya kumpeleka. Stella asema yeye na mumewe walitafuta shule lakini wazazi walikataa kumlipia karo.
“Baba alipoulizwa, alisema japo alitaka kumlipia msichana huyo karo ya shule, wanawe hawakutaka dada yao asome,” alieleza. Stella anasema alijitolea kumtafutia msichana huyo shule nyingine lakini wazazi walikataa kulipa karo wakisema hawakuwa na pesa hadi wauze mifugo.
Anasema aliomba shule iwapatie muda watafute pesa lakini walikataa kulipa karo huku ndugu ya msichana akisema ni lazima aozwe. “Walisema wangempeleka Tanzania akarudie darasa la sita na msichana alikuwa tayari kufanya hivyo kabla ya kugundua kwamba walikuwa wamepanga kumuoza kwa mzee wa rika la babu yake,” anasema Bi Stella.
Kwa mara ya pili, msichana huyo alitorokea kwa nyumba ya Stella na wakalazimika kumficha katika eneo ambalo hakuna aliyemfahamu.
Hii ilikasirisha ndugu wa msichana huyo wakavamia nyumba yake na kusaka kila mahali. Walipomkosa, walianza kutisha Stella na mumewe.
Stella anasema alipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Olpusimoru na maafisa wakamuita ndugu na baba wa msichana huyo lakini hawakuenda.
Polisi pia hawakumpatia nambari ya kuripoti kisa hicho lakini walimwambia wangempa akihiitaji. Ajabu ni kwamba ndugu ya msichana alienda kupiga ripoti katika kituo hicho kwamba baadhi ya watu walikuwa wameiba dada yake.
Licha ya kuwa Stella alikuwa amepiga ripoti, mwanamume huyo hakuchukuliwa hatua. Stella anasema ingawa Childline Kenya iliahidi kuwasiliana naye haraka ili imuunganishe na afisa wa watoto kaunti ya Narok hakupata msaada wowote. “Sikuona yeyote hapa, sikupigiwa simu na yeyote,” alisema.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Childline Kenya Martha Keya, Stella alitumwa kwa afisa wa watoto kaunti ya Narok lakini alipopigiwa simu hakupatikana.
“Hakuna aliyewasiliana nami. Nilihakikisha msichana huyo alijiuunga na shule ya upili. Yeye ni mmoja wa wanne ambao walipitia masaibu sawa lakini sawa wako salama shuleni,” alisema.
Hata hivyo, alikataa tufichue shule wanazosomea kwa sababu ya usalama wa wasichana hao. Anasema akipata msaada anaweza kusaidia wasichana wengi wanaoteseka kwa kuozwa na jamaa zao badala ya kuwasomesha.