Makala

Ndege rasmi ya Rais kutupwa kwa kukosa ufaafu kwa matumizi ya sasa

Na BRIAN WASUNA September 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HARAMBEE One, ndege rasmi ya Rais wa Kenya yenye umri wa miaka 30, ambayo imewahudumia Marais wanne wa taifa hili, kwa sasa iko Uholanzi kutengenezwa kwa mara ya mwisho kabla ya kustaafishwa na nafasi yake kuchukuliwa na ndege mpya ya kisasa.

Waziri wa Ulinzi Bi Soipan Tuya amethibitisha kuwa ndege hiyo iko katika bohari la kampuni ya Fokker Services Group – kampuni inayotengeneza vipuri vya ndege za chapa ya Fokker – kwa kipindi cha mwaka mmoja kutengenezwa kwa mara ya mwisho.

Kwa mujibu wa Fokker Services Group, Harambee One imepitwa na wakati na haitafaa tena kwa matumizi ya sasa, kwani kuendelea kuitengeneza kumeonekana kutokuwa na manufaa tena kwa sababu ya gharama kubwa ya vipuri.

“Kwa sasa, (ndege ya Rais) iko nje ya nchi kutengenezwa kwa mwaka mmoja. Tunatarajia kuirejesha mwaka wa 2026,” Bi Tuya alisema katika mahojiano kwa simu na Taifa Jumapili mnamo Ijumaa, akiongeza kuwa gharama ya vipuri kwa ndege za zamani imepanda mno kiasi kwamba haiwezi kuvumiliwa tena.

Taarifa hiyo kutoka Fokker imelazimu Wizara ya Ulinzi kuanza mipango ya kununua ndege mpya itakayochukua nafasi ya Harambee One, ambayo ilinunuliwa mwaka wa 1996 chini ya utawala wa marehemu Rais Daniel Arap Moi.

“Hatujafanya maamuzi rasmi kwa sasa. Tunatumia chaguo mbalimbali kama ndege za watu mashuhuri za Jeshi la Anga, ndege za kibiashara kama Kenya Airways au kukodisha ndege. Lakini haya ni maamuzi ya muda mfupi ambayo hayawezi kudumu,” Bi Tuya akaeleza.

Bi Tuya aliongeza kuwa ununuzi wa ndege mpya ya Rais unaweza kufanyika ndani ya miaka miwili ijayo, kutegemea upatikanaji wa fedha katika bajeti ya jeshi.

Mtaalamu wa masuala ya anga wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) aliambia Taifa Jumapili kuwa matatizo ya kiufundi ya Harambee One yamevuruga ratiba za safari za Rais mara kadhaa, na hata kuwa tishio kwa usalama licha ya juhudi za wahandisi wa Jeshi la Anga.

Aliongeza kuwa ununuzi wa ndege mpya hauwezi kuepukika, kwani hata baada ya Harambee One kurudi mwaka ujao, Rais Ruto anaweza kuhitajika kutumia ndege za kibiashara au kukodisha hadi ndege mpya itakaponunuliwa.

Mtaalamu huyo alisema dalili za uzee wa Harambee One zimekuwa dhahiri hasa katika kipindi cha mwaka uliopita ambapo hitilafu kadhaa zimeripotiwa ndani ya anga ya Kenya na pia katika mataifa ya kigeni.

Mara kadhaa, KDF imelazimika kumpa Rais Ruto na ujumbe wake ndege mbadala.

Wakati wa kufungwa kwa Mkutano wa Pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mnamo Februari 8, 2025, Marais waliokuwa wamehudhuria walikuwa wakiondoka Dar es Salaam kuelekea nchi zao.

Rais William Ruto alikuwa mwenyekiti mwenza wa mkutano huo pamoja na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Kwa mujibu wa itifaki ya mikutano ya kiwango hicho, Marais huondoka kwa utaratibu ule ule waliowasili. Hivyo, Rais Ruto alitarajiwa kupanda Harambee One – Fokker 70 ER ya miaka 30 – saa kumi na moja jioni na kuondoka Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere kabla ya Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.

Hata hivyo, Harambee One ilizua mkanganyiko wa itifaki baada ya kupata hitilafu za kiufundi na kushindwa kupaa.

Wahandisi walipokuwa wakihangaika kuirekebisha, Rais Ruto alishuhudia marais wenzake, wakiwemo wa Somalia, wakiondoka kabla yake.

Zaidi ya saa mbili baadaye, haikuonyesha dalili ya kuwa tayari kuruka, hali iliyowalazimu maafisa wa Kenya na Tanzania kuamua kuwa Rais Ruto na ujumbe wake walale tena Dar es Salaam.

Jeshi la Anga la Kenya lililazimika kutuma ndege nyingine kutoka Nairobi kuhakikisha Rais Ruto na ujumbe wake waliweza kurudi Nairobi asubuhi iliyofuata.

Hitilafu hiyo ilisababisha matumizi ya ziada kwa gharama za chakula, malazi, na mafuta kwa ndege aina ya Dash-8 iliyotumwa kutoka Nairobi jioni hiyo.

Katika safari nyingine kuelekea Uswizi, mfumo wa Harambee One ulivuja baada ya ndege kupaa kutoka Nairobi, na kuwalazimu marubani wa Jeshi la Anga kutua kwa dharura jijini Cairo kuepusha janga.

Chanzo cha habari kiliongeza kuwa muundo wa ndege hiyo una hitilafu ambayo imekuwa ikisababisha mlango kushindwa kufunguka mara kwa mara.

“Haifai tena kwa safari wala kiuchumi,” alisema mtaalamu huyo.

Kadri mataifa na mashirika ya ndege yanavyoendeleza mabadiliko kwa kununua ndege mpya, vipuri vya ndege za zamani kama Fokker 70 ER vimekuwa adimu na ghali, kwani waundaji wanapendelea kutoa vipuri vya ndege mpya ambazo zipo kwa wingi duniani.

Mwaka wa 2020, Rais Uhuru Kenyatta alipendekeza ndege hiyo ibadilishwe, lakini janga la corona lilibadili vipaumbele vya nchi nyingi, ikiwemo Kenya.