Makala

Ndindi Nyoro: Sasa sio mchele na nyama tu, tumeongeza chapati na uji shuleni

January 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro amepanua hafla za kula mchele na nyama sasa akiongeza chapati na uji katika shule za harambee eneo bunge lake.

Hafla hizo za sherehe za mchele na nyama hunogeshwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, akisema kwamba ni utamaduni wa Mwafrika kujadiliana ndani ya mlo.

Bw Nyoro alisema uji utakuwa ukiwekwa sukari kwa mujibu wa utaalamu wa utamu wanaomshauri mbunge huyo.

“Sasa katika shule zote 62 zetu ambazo wanafunzi huingia asubuhi na kutoka jioni watakuwa wanakula Githeri kwa siku tatu, mchele kwa siku tatu na sasa chapati kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi,” akasema.

Bw Nyoro alisema hayo katika uwanja wa Mumbi mnamo Alhamisi ambapo alizindua awamu ya pili ya mpango wa Elimu Bora ambapo kila mwanafunzi atakuwa akilipa karo ya Sh1,009 hizo zingine akilipiwa na mradi huo wa mbunge wao.

Alizindua awamu ya kwanza ya mradi huo mwaka jana, kukizuka cheche kuhusu uwazi wa utoaji kandarasi za usambazaji wa nafaka na unga za kufanikisha mradi huo.

Mwenyekiti wa muungano wa wasambazaji bidhaa katika eneo hilo Bw Francis Maina alisema kwamba mradi huo umemaliza wanakandarasi wadogowadogo.

Bw Maina alisema kwamba kwa sasa mfumo wa shule kujinunulia chakula kibinafsi umezimwa na kwa sasa kandarasi hiyo imeunganishwa pamoja na kukabidhiwa aliye na uwezo wa kuhudumia usambazaji wa ujumla kwa shule hizo zote.

“Sasa huku Kiharu sio Githeri tu. Ongeza mchele hapo na chapati pia bila kusahau uji,” akasema Bw Nyoro.

Baadhi ya wanafunzi na wazazi wa Kiharu wakifuatilia uzinduzi wa masomo kwa bei nafuu wa mbunge wao Bw Ndindi Nyoro Januari 11, 2024. Picha|Mwangi Muiruri

Bw Nyoro aliongeza kwamba wale wanafunzi ambao watajiunga na shule 20 zilizo katika hatari ya kufungwa kutokana na idadi ndogo atawalipia karo mwaka mzima na pia awape sare za shule bila gharama.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na zaidi ya wabunge 10 wakiongozwa na Mbunge mwanamke Bi Betty Maina na Seneta Joe Nyutu.

Wanasiasa hao walimsifu Bw Nyoro kama aliye na maono ya maendeleo na ambaye ako na uwezo wa kumrithi Rais Ruto mwaka wa 2032.

Licha ya Bw Nyoro kukwepa kuzungumzia suala hilo la urithi, wadadisi wa kisiasa eneo hilo wamekuwa wakidai kwamba kuna uhasama wa kichinichini kati yake na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

[email protected]