• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
NDIVYO SIVYO: Methali mtoto wa nyoka ni nyoka huvumisha mwigo wa sifa hasi tu

NDIVYO SIVYO: Methali mtoto wa nyoka ni nyoka huvumisha mwigo wa sifa hasi tu

Na ENOCK NYARIKI

METHALI huchangamana sana kimaana, hali ambayo aghalabu huwakanganya watumiaji wazo na kuwafanya kuzitumia visivyo katika mazungumzo yao.

Uchangamano huo husababishwa na mfanano wa msamiati ambao hutumiwa kufafanulia sehemu za methali hizo.

Mathalani, umakinifu mkubwa unahitajiwa ili kufahamu kuwa methali ‘Aisifuye mvua imenyea’ na ‘Kitanda usichokilalia hujui kunguni wake’ zinatofautiana kimaana licha ya kuwa na ukuruba wa aina fulani unaoletwa na msamiati uliotumiwa kuzifafanua kwa sehemu.

Kile kinachojitokeza katika methali zote mbili ni kuwa mtu anaweza kulieleza jambo fulani vizuri kutokana na tajriba aliyo nayo kuhusu jambo lenyewe.

Katika makala haya, tutafafanua matumizi mwafaka ya methali “Mtoto wa nyoka ni nyoka” ambayo baadhi ya watu huikosea katika mazungumzo.

Juzi, mmoja wa masahibu wangu aliitumia methali hiyo alipokuwa akimsifia mtoto mwenye umri wa takribani miaka mitatu aliyekitongoa Kiswahili kama baba yake.

Ingawa niliuelewa vyema ujumbe ambao bwana mwenyewe alitaka kuupitisha, hakika methali yenyewe haikuafiki muktadha wa matumizi.

‘Mtoto wa nyoka ni nyoka’ hutumiwa mzungumzaji an apotaka kulipitisha funzo kwamba aghalabu mtoto wa mtu mwenye sifa mbaya huishia kuwa na sifa mbaya.

Haiwezi kutumiwa kuwili; yaani kuelezea hali ambapo mtoto wa mtu mbaya huishia kuwa na sifa mbaya na mtoto wa mtu mzuri kuwa na sifa nzuri.

Msamiati “nyoka’’ unatusaidia kufikia uamuzi kwamba methali yenyewe hutumiwa kwa njia hasi tu.

Methali hii hata hivyo inakinzana kimaana na nyingine inayosema: Moto hauzai moto. Hii ya pili inatoa funzo kwamba si lazima mtoto achukue sifa sawa na za mzazi wake.

Lengo la mzungumzaji liwapo ni kueleza kwamba mtoto fulani ameishia kuziiga sifa nzuri za mzazi wake – ufundi wa kukisema Kiswahili katika muktadha huu – basi methali ambayo itatumiwa kuielezea hali hiyo ni “Mwana wa mhunzi asiposana huvukuta”.

Katika methali hii yanajitokeza mambo mawili; mwigo wa sifa pamoja na ustadi wa kulitekeleza jambo. Hata hivyo, inaweza pia kuzua wazo kwamba inawezekana mtoto kuiga sehemu ya sifa za wazazi au ukoo iwapo haiwezekani mtoto mwenyewe kusuluhia kikamilifu.

Alhasili, methali “Mtoto wa nyoka ni nyoka” na “Mtoto wa mhunzi asiposana huvukuta” zina uhusiano wa aina fulani kwa sababu zote zinaeleza kuhusu mwigo wa sifa au tabia fulani kutoka kwa wazazi. Hata hivyo, methali ya kwanza inavumisha sifa mbaya ilhali ile ya pili inavumisha sifa nzuri.

You can share this post!

VITUKO: Sindwele akutikana barabarani si wa maji si wa...

GWIJI WA WIKI: Mohammed Ghassani

adminleo