• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
NDIVYO SIVYO: Neno ‘hofia’ linatumiwa kiholela hasa katika tasnia ya uanahabari

NDIVYO SIVYO: Neno ‘hofia’ linatumiwa kiholela hasa katika tasnia ya uanahabari

Na ENOCK NYARIKI

KAULI, “sina hofu” na “sihofu’’ zina maana ile ile moja.

Tofauti iliyopo ni kuwa dhana hiyo moja inajitokeza kama nomino na kama kitenzi. Neno ambalo aghalabu hutumiwa katika mazungumzo kuelezea kitendo cha kuwa na woga ni “hofia”.

Ninadhani watu hulitumia neno hili hivyo ili kulitofautisha na nomino “hofu”.

Hata hivyo, “hofia” ni kauli ya kutendea ya kitenzi “hofu”.

Kiambishi {i} katika neno la kwanza huibua dhana mbalimbali.

Dhana mojawapo, na ambayo huibuliwa na vitenzi ambavyo viko katika kauli ya kutendea ni ile ya kitendo kutendwa kwa niaba ya mtu mwingine na kumwathiri kwa mema au mabaya.

Vingi vya vitenzi vya asili ya kigeni, hofu kikiwamo, vinaponyambuliwa katika kauli ya kutendea hukosa mantiki.
Dhana ya pili ni “kuhusu”.

Kiambishi {i} katika kauli “hofia usalama wake” kinawakilisha neno ‘kuhusu’. Kwa hivyo, isingekuwa sahihi kusema “hofia kuhusu usalama wake” kwa sababu kwa kufanya hivyo tutakinyima kiambishi {i} dhima yake. Sasa tuingie katika kiini cha mjadala.

Yapo baadhi ya mazingira ambapo tafsiri ya moja kwa moja ya dhana husaidia katika kupitisha ujumbe uliokusudiwa. Vyombo vya habari huitumia sana tafsiri hii pale ambapo huelezea dhana mpya ambazo isingewezekana kuzipa msamiati au istilahi ya papo kwa hapo kutokana na muda mfupi vilivyo nao vyombo hivyo wa kuandaa taarifa.

Hata hivyo, si wakati wote ambapo tafsiri ya moja kwa moja hukidhi haja. Zipo baadhi ya dhana ambazo baada ya kutafsiriwa na kutumiwa kwa muda fulani zilionekana kuwa na upungufu.

“Mkuu wa Sheria” ni mojawapo ya dhana hizo ambayo baadaye ilikosolewa kuwa “Mwanasheria Mkuu.”

Tafsiri nyingine za moja kwa moja zinatokana na athari ya lugha ya Kiingereza. Mfano mmojawapo ni “fear for their lives” ambayo baadhi ya watu huitafsiri kama “hofia maisha yao”.

Tafsiri hii imelemaa. Watu “hawahofii maisha yao” bali huhofia usalama wao au huhofu kuhusu usalama wao.

Si semi zote za Kiingereza zinazoweza kuhawilishiwa lugha ya Kiswahili pasi na kupotosha maana katika matini asilia. Sababu ni kuwa utamaduni ambamo semi zenyewe zimeundiwa ni tofauti na utamaduni wa Waswahili.

Alhasili, ni muhimu kuziepuka tafsiri za moja kwa moja pale ambapo tafsiri zenyewe huishia kupotosha ujumbe uliodhamiriwa.

Kauli ya Kiingereza “fear for their lives” ni watu kuhofu kuhusu usalama wao bali si “hofu kuhusu maisha yao”.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Kazi za Fasihi husemezana na kuathiriana

MAPITIO YA TUNGO: Musaleo! Riwaya inayoumulika uongozi wa...

adminleo