• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Nduma zenye sumu zinavyotua kwenye sahani

Nduma zenye sumu zinavyotua kwenye sahani

NA SAMMY WAWERU

UNAPOSHABIKIA kipande cha viazivikuu maarufu kama nduma, umeshawahi kujiuliza kilikokuziwa?

Hii ni hoja muhimu kabla ya kuteremsha kitafunio hicho chenye mashabiki wengi hasa maeneo ya mijini.

Nduma hukuzwa kwa wingi maeneo ya mashambani, japo baadhi ya ‘wakulima’ wenye chanzo cha maji mijini wanazilima.

Wanazaraa wa mijini, wapo wanaokuza zao hilo kwa kutumia majitaka jambo linaloibua maswali kuhusu usalama wake kiafya.

Kwa wakazi wa Kaunti ya Nairobi, endapo umezuru mtaa wa Mwiki, Mathare, Kariobangi, Zimmerman, Githurai (44 na 45), Kahawa West, Kasarani, Kahawa Wendani, kati ya mitaa mingine, kwenye mapito ya majitaka hutakosa kuona mindumaa inayolimwa.

Nduma changa zilizopandwa baada ya zingine kuvunwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Si mtindo ulioanzishwa leo, jana wala juzi, ila umekuwepo kwa muda.

Kwa mfano, katika mtaa wa Githurai 44 pembezoni mwa barabara kuu ya Thika – Nairobi, maarufu kama Thika Super Highway, kuna wakulima wanaozalisha viazi vikuu hivyo.

Hata hivyo, kiini cha maji kunawirisha zao hilo ni kipi?

Majitaka yanayotoka Githurai, Kahawa Wendani na Sukari, na vilevile Kambi ya Jeshi ya Kahawa Garisson yaliyoelekezwa kwenye mto wa kuyasafirisha ndiyo yanatumika.

Kwenye mahojiano na mmoja wa wanaoendeleza shughuli hiyo tutakayemuita Mercy, japo si jina lake halisi, anasema anazalisha nduma kama njia mojawapo kujiendeleza kimaisha.

“Ni zao lenye ushindani mkuu sokoni na linalonipa mapato ya haraka,” akaambia Taifa Leo Dijitali.

Mtaa wa Kahawa West, taswira ya aina hiyo pia si tofauti, cha kushangaza zaidi zao hilo likikuzwa kandokando mwa barabara.

Unapozuru barabara ya Northern Bypass, makutano yake na Kamiti Road, wapo wanaolima zao hilo kwa wingi.

Mtaro wa majitaka ulioelekezwa kwa ‘shamba’ la nduma. PICHA|SAMMY WAWERU

Taswira hiyo si tofauti na mitaa ya Zimmerman, Mwiki, Mathare, Kariobangi, Kasarani, na hata Ruai.

Mkulima mwingine tutakayemuita John, anasema ili kufananisha zao hilo na yanayotolewa mashambani, hupakwa udongo.

“Aghalabu, hupaka udongo wanunuzi waamini nduma tunazolima Nairobi zimetoka mashambani,” anafichua baadhi ya hadaa wanazotumia.

Kando na nduma, mimea mingine inayolimwa katika mashamba na ploti za mitaa hiyo ambazo hazijaboreshwa ni pamoja na mboga za kienyeji, sukuma wiki, spinachi na wengine miwa na ndizi.

Majitaka, ni yale machafu yanayoachiliwa kutoka kwenye majengo ya kukodisha na mengine ya malandilodi.

Aidha, kemikali zinazotumika hasa kwenye vyoo, kifupi zinaishia kwenye mazao yanayokuzwa kwa kutumia majitaka, baadhi zikiwa zimeundwa kwa kutumia malighafi hatari na yenye sumu.

Charles Opiyo, mtaalamu wa masuala ya lishe kutoka Global Alliance for Improved Nutrition (GAIN), shirika lenye asili ya Uswisi lililoanzishwa na Umoja wa Mataifa (UN) 2002 ili kukabiliana na changamoto za kibinadamu zinazosababishwa na utapiamlo, anasema usalama wa chakula unaanzia pembejeo na maji yanayotumika.

Dimbwi la majitaka kando ya nduma. PICHA|SAMMY WAWERU

“Maji yanayotumika kuzalisha mazao ni mojawapo ya nguzo kuu kuangazia usalama wa chakula. Majitaka si salama katika kilimo,” Opiyo anasisitiza.

GAIN hushirikiana na serikali za mataifa, wafanyabiashara na mashirika ya kutetea haki za kijamii, lengo likiwa kubadilisha mfumo wa chakula ili uwe salama.

Huku mitaa inayoendeleza kilimo kwa kutumia majitaka, Serikali ya Kaunti ya Nairobi inaonekana kufumbia machi suala hilo.

Ni hatari, ikizingatiwa kuwa maradhi kama vile Saratani yanahusishwa na ulaji wa chakula kilichokuzwa kwa kutumia kemikali.

Mwaka 2019, kabla ya kubanduliwa, aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko alitoa onyo kwa wakazi wanaofanya kilimo kwa kutumia majitaka.

Halmashauri ya Kitaifa kuhusu Mazingira (NEMA), pia inaonekana kuwa usingizini wenyeji Nairobi wakiendelea kulishwa nduma hatari.

  • Tags

You can share this post!

Maana halisi ya ‘AirBnBs’ na kwa nini jina hilo...

Lizzie Wanyoike alivyowindwa na vijana kijijini kama swara

T L