• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Ngaruiya Junior alivyorukwa Kipetero na UDA

Ngaruiya Junior alivyorukwa Kipetero na UDA

NA MWANGI MUIRURI

IMEIBUKA sasa kuwa msanii Ngaruiya Junior aliyejiunga na kampeni za United Democratic Alliance (UDA) katika siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 hajapewa kazi licha ya kuahidiwa kwamba angeipata Dkt William Ruto akitwaa uongozi.

Badala yake, amekuwa akiripoti katika afisi za Ikulu kila siku kwa mwaka mzima sasa akitegea kuajiriwa, lakini ikibidi awe na ngojangoja za kumuumiza matumbo.

Katika hafla za wasanii ambazo Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amehudhuria, amekuwa akisema kwamba msanii huyo “amepewa kazi na Rais William Ruto katika Ikulu”.

Bw Ngaruiya ni mzawa wa Kaunti ya Kiambu lakini akalelewa Nakuru.

Nyanya yake alizua sokomoko alipodaia kwamba mrengo wa Azimio ulikuwa umempa dili ya Sh15 milioni 2022, ili ataliki mrengo wa Ruto lakini akakataa.

“Ruto amekuwa rafiki wa familia yangu na mimi niliamua kukaa katika siasa zake,” akasema.

Alijiunga na wasanii wengine ambao walikuwa wakipigia debe uwaniaji wa Ruto kuwa rais na hatimaye akajiunga na kundi liitwalo Radico ambalo hushirikishwa na mwanaharakati Dennis Itumbi.

Sasa, imeibuka kwamba licha ya kuahidiwa kazi katika kitengo cha itifaki na usanii katika Ikulu, bado hajapewa kazi hiyo.

Ni katika hafla ya mazishi ya mamake ambayo Bw Itumbi alihudhuria na ambapo baadhi ya wasanii walimkumbusha kwamba “Junior bado anahangaika bila kazi”.

Akiwajibu, Itumbi alisema kwamba “huo ni ukweli lakini muelewe kwamba tuko katika mikakati ya kumtuza kwa kuwa ushirikiano wetu naye sio wa kuwekwa mzaha”.

Itumbi alisema kwamba “kwa sasa tunasaka idhini ya kumpa ajira Bw Junior kutoka kwa mkuu wa utumishi wa umma Bw Felix Koskei”.

Kabla hayo yafanyike, Itumbi alisema kuwa yeye ndiye anamshikilia Junior kwa gharama zake.

“Huyu mambo yake yako sawa na hatumwachilii. Mkiona anahangaika mjue ni kwa muda tu. Suala lake liko mikononi mwangu na yote yatakuwa sawa,” akasema.

Hata hivyo, imefichuka kwamba Junior anahangaika kuajiriwa kutokana na elimu yake ambayo ni ya kiwango cha msingi.

“Shida tuliyo nayo katika kesi ya huyu muungwana ni kwamba ni mtiifu kwa siasa yetu ndiyo, lakini kuna mikakati na masharti ya ajira ya serikali. Kazi tunayoambiwa tumpee inahitaji stakabadhi za elimu ya juu lakini huyu hana. Labda atulie huku ndani ya serikali akila marupurupu ya huduma za usanii katika mikutano ya kisiasa na kikazi,” akasema mmoja wa maafisa wa serikali.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Akothee ahimiza wanawake kuiga nyayo zake

Yabainika wazazi wanakarabati alama za KCPE za watoto wao...

T L