• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
NGILA: Mwezi huu wa Oktoba utumike kuvumisha usalama mitandaoni

NGILA: Mwezi huu wa Oktoba utumike kuvumisha usalama mitandaoni

Na FAUSTINE NGILA

DUNIA imetenga mwezi Oktoba kueneza umuhimu wa usalama mitandaoni huku udukuzi, wizi wa fedha na utambulisho bandia ukitawala.

Kenya kwa mfano, ilipoteza Sh29 bilioni mwaka uliopita na Sh21 bilioni mwaka wa 2017 kupitia maovu haya.

Kando na hayo, watumizi wa Intaneti wamepoteza udhibiti wa data zao za siri. Kampuni za mitandao ya kijamii kama Facebook inayomiliki pia Instagram na WhatsApp, Twitter na Google zimeonyesha wazi kuwa haziko tayari kuwalinda wateja wake.

Ni kutokana na hali hii ambapo wizi hufanyika mitandaoni. Licha ya serikali ya Kenya kujitahidi kuzima mtindo huu, wadukuzi wameibuka na mbinu mpya za kuiba hela za watu binafsi na kampuni kwenye akaunti zao za benki.

Ili kukabili hali hii, ni lazima vyombo vya kutambua na kuzuia wizi huu vibuni mbinu madhubuti.

Teknolojia za kisasa za kusaidia katika mchakato huu kama Blockchain na Artificial Intelligence zimependekezwa, lakini ni wazi kuwa Wizara ya Teknohama inajikokota kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na wataalamu katika sekta ya teknolojia.

Mwezi huu wa Oktoba tunafaa kushuhudia kampeni za serikali kueleza watu jinsi ya kujikinga dhidi ya wadukuzi na wezi wa data wanaotumia utambulisho bandia baada ya kuiba ama kitambulisho au simu zya mwananchi.

Wengi huishia kuomba mikopo kwa programu za simu za mikopo, wengine kwenye benki huku wengine wakitumia utambulisho huo kuomba marafiki na familia ya aliyeibiwa mamilioni ya pesa.

Licha ya kuwa na sheria dhidi ya wizi wa mitandaoni, maafisa wetu hawajamakinika vilivyo kwani hawajapewa mafunzo yanayofaa. Wezi wanajua pengo hili na linawapa motisha kuendelea kuiba.

Hivyo ni muhimu kwa serikali kuunda kikosi maalum cha polisi ambacho kitafundishwa kuhusu mbinu zote za hila mitandaoni na jinsi ya kuzizima.

Tunaishi katika mageuzi ya kiteknolojia, ambayo yanafanyika kwa kasi. Iwapo wezi wataipiku serikali kwa kwenda na kasi hiyo, basi huenda wahalifu wa mitandaoni wakaiba matrilioni ya pesa.

Na si serikali pekee, sekta ya kibinafsi pia inapaswa kuwa mstari wa mbele, hasa benki kupigia debe haja ya kuhakikisha fedha kwenye akaunti ziko salama.

Tunafaa kuona matangazo na shughuli za uhamasisho kote nchini mwezi huu kuhusu suala hili, iwapo tunalenga kuulinda uchumi wetu dhidi ya watu wanaovuna wasipopanda.

You can share this post!

WASONGA: Mutyambai akabiliane na maafisa majambazi

SHINA LA UHAI: Homa ya nyongo ya manjano katika watoto...

adminleo