NGILA: Teknolojia pekee haitoshi kuzima wizi wa pesa za benki
Na FAUSTINE NGILA
MATUKIO ya wizi wa takribani Sh11.6 milioni wikendi ya Pasaka katika mashine za ATM za benki ya Barclays uliwashtua wanabenki wengi, hasa kwa sababu hakuna mabavu yaliyotumika wala mtu yeyote kujeruhiwa.
Katika mojawapo ya ripoti za polisi, ilithibitishwa kuwa mashine ya ATM mtaani Mutindwa ambapo Sh6 milioni ziliibwa, haikuwa na kamera fiche za kurekodi matukio wala mlinzi, jinsi ilivyo katika mashine nyingine.
Katika kisa cha mashine ya ATM ya Hospitali ya Mater, Viwandani, kamera fiche zilipakwa mafuta ya kulainisha ngozi ili kulemaza uwezo wake wa kurekodi wizi huo wa Sh1 milioni.
Hali ilikuwa vivyo hivyo katika mashine ya ATM katika Hospitali Kuu ya Kenyatta ambapo Sh4 milioni zilitolewa huku hela nyingine zikiibwa katikati ya jiji kuu la Nairobi ambapo polisi walisema hawakupata taarifa kuhusu tukio hilo.
Visa hivi vinazua maswali mengi kuliko majibu, wengi wakikisia kuwa ulikuwa wizi uliopangwa na wezi, wafanyakazi wa benki ya Barclays na polisi ili kujitajirisha na hela hizo.
Licha ya benki hiyo kusema kuwa inashirikiana na makachero kuwatambua wezi hao na kuwachukulia hatua mwafaka, twajua kwamba uwezekano wa hilo kutokea ni finyu mno, na inachotakiwa kufanya ni kuziba mianya yote ya wizi.
Pia, natoa wito kwa benki nyingine humu nchini kuweka mikakati mwafaka kuzuia matukio kama haya.
Utasamehewa kuamini kuwa wizi kama huu huanzishwa na mfanyakazi ndani ya benki ambaye amekuwa akilalamika kwa muda mrefu kuhusu malipo ya ‘kitoto’, ambayo humghadhabisha na hatimaye kuamua ‘kujilipa’.
Lakini kwa yakini wizi kama huu hutokana na uroho na tamaa ya kutajirika haraka, hasa kwa wafanyakazi ambao ni rahisi kuhadaiwa na wezi ambao wamezoea kufanikisha wizi kama huu.
Hata hivyo, ni aibu kwa mfanyakazi kuiba mali ya mwajiri wake, eti kwa kuwa amedhalilishwa kimalipo.
Pesa za wizi kama hizo haziwezi kumfikisha kwenye ndoto zake maishani; mara nyingi watu kama hao hujipata kwenye taabu nyingi zaidi kuliko yale ‘malipo duni.’
Kwa kuwa wizi kama huu hupunguzia benki imani kwa wateja, benki zinafaa kuhakikisha usalama umewekwa katika kila mashine ya ATM.
Pia ni hatua muhimu kutumia teknolojia ya kufuatilia na kunasa sauti za simu za wafanyakazi ambao wanashukiwa kuwa na njama ya kuiba.
Benki zinafaa kuwa na idara ya kufuatilia kila usambazaji wa pesa, kuhesabu hela kwa mbashara na kutambua wizi mara moja, kwa kuwa katika wizi wa pesa, hakuna suluhu moja ambayo inatosha kukomesha uovu huo.
Teknolojia pekee haitoshi katika kazi nzima ya kulinda pesa, kwani haiwezi kutambua kuna polisi au mlinzi aliyehongwa kutekeleza wizi, lakini mikakati kadhaa ya pamoja itasaidia pakubwa kupunguza, kama si kutokomeza wizi wa pesa za benki.