NGILA: Tunahitaji sera kudhibiti magari ya kielektroniki
Na FAUSTINE NGILA
JUMATATU wiki hii, gari la kieletroniki la kampuni ya Amerika ya Tesla lilizua mchecheto kwenye mitandao ya kijamii nchini, wengi wakidai ndilo la kwanza kuwahi kufika Kenya.
Watoto walionekana kwenye video wakichangamkia gari hilo ambalo limeundwa kibunifu kuliwezesha kuwa na mbawa.
Ingawa magari ya kielektoniki yamekuwepo humu nchini tangu 2016, hilo ni gari la kipekee ambalo ni nadra kuliona katika barabara za Kenya.
Lakini kwa wapenzi wa magari ya kifahari ya kielektroniki wanaomezea mate kumiliki kama hilo, itawabidi kusubiri zaidi hadi pale taifa litakuwa tayari kuwekeza katika miundo ya kuchaji betri za magari ya aina hiyo.
Kufikia sasa, Kenya imepiga hatua tu chache katika mchakato huo, Nairobi ikijivunia maeneo manne pekee ya kuchaji magari ya kielektroniki.
Licha ya kuwa mojawapo ya mataifa ya kwanza barani Afrika kununua magari haya, mustakabali wa sekta hii mpya umo mikononi mwa serikali yetu hasa katika ujenzi wa vituo vya kuchaji magari mbalimbali ya kieletroniki na sera za kudhibiti ada na mazingira.
Ilivyo kwa sasa, vituo vya petrol haviwezi kugeuzwa maeneo ya kuchaji kwani walioviunda hawakufikiria kuhusu siku za usoni kama hizi, ambapo walimwengu watakoma kutumia magari ya mafuta.
Kumekuwa na pendekezo la kuchaji magari nyumbani yanapoegeshwa usiku mzima, lakini huo ni mlima kwa maelfu ya wamiliki wa nyumba za kukodi mijini.
Suluhu bora ni kujenga vituo mahususi vya kuchaji magari haya ya kielektroniki katika maeneo pana ya maegesho mijini, maeneo ya kuoshea magari na pia kando ya barabara zote kuu nchini.
Tatizo ni kwamba, hapo ndipo utawaona wawekezaji walafi waking’ang’ania maeneo hayo.
Ingawa shirika la kutengeneza umeme la KenGen limeanzisha mradi wa kupiga jeki wazo hili, bado umesalia katika awamu ya majaribio na utekelezaji kamili utakuwa baadaye mwakani.
Baadhi ya kampuni kama Nopia Ride, Knights Energy na Stimaboda pia zimejitosa katika soko hilo.
Lakini ukosefu wa sera za kudhibiti sekta hii huenda ukasambaratisha juhudi za kuwekezwa kwa miundomsingi bora.
Ni kweli kwamba dunia ya sasa inawazia sana kuhusu machafuko ya hewa kutokana na magari ya mafuta.
Hivyo, tunapojiandaa kwa matumizi ya kawi safi katika magari ni vyema kuweka mwongozo wa jinsi sekta ya uchukuzi itaendeshwa miaka ya usoni.
Naelewa kwamba magari ya mafuta yataendelea kuwepo kwa miaka mingi ijayo, lakini hatimaye hata mataifa yanayostawi yatakumbatia haja ya kuondoa teknolojia za kale zinazochafua mazingira.
Hivyo, kuzima ukora wa baadhi ya wawekezaji kutuletea chaji duni, kama jinsi ambavyo kuna aina mbalimbali za simu na chaja tofauti; magari ya kieletrokini ni tofauti na pia chaja zake ni tofauti. Muda wa kujaza betri pia ni tofauti.
Hivyo tusipopata sera za kudhibiti masuala haya basi huenda kukawa na wawekezaji wengi tu watakaofanya watakavyo bila kujali wenye magari.