NGILA: Uchumi wa dijitali nchini umekua, lakini visiki bado vipo
Na FAUSTINE NGILA
KATIKA miaka 10 iliyopita, teknolojia imegeuza jinsi wanadamu wanavyotangamana na kufikiria.
Imesaidia kukuza kila sekta, kwa kutoa suluhu kwa changamoto nyingi za kifedha, kiafya, mawasiliano, uchukuzi, kilimo, biashara na elimu.
Simu za kisasa zimekuwa mstari wa mbele katika mageuzi haya. Hapo 2010, simu nyingi zilikuwa aina ya mawimbi ya 2G na 3G lakini sasa simu za 4G zimeenea hadi vijijini.
Wakati huo, watumizi wa intaneti walikuwa milioni 3.9 lakini kwa sasa wamefika Wakenya milioni 46.8. Kenya ni ya pili barani Afrika kwa kasi ya intaneti baada ya Madagascar.
Ni kukua huku kwa umiliki wa simu na kasi ya intaneti ambako kumechangia pakubwa katika maendeleo ya uchumi wa dijitali.
Kwa sasa, kuna programu nyingi za simu ambazo zinatoa suluhu za kilimo, ambapo wakulima hupata soko la moja kwa moja bila kuwategemea mabroka wapunjaji.
Tofauti na mwongo mmoja uliopita, Wakenya sasa wanaweza kununua bidhaa mitandaoni wakiwa tu nyumbani.
Wanaweza kusafiri katika maeneo ya mijini kwa vigari vya kibinafsi kwa kuagiza huduma hiyo kwa simu.
Ukianzisha biashara utahitajika kuunda programu ya simu ili kufikia wateja ambao wengi wako mitandaoni. Malipo mengi kwa sasa yanapitia kwa simu. Kutoka akaunti milioni 16 za malipo ya kidijitali hapo 2011 hadi milioni 54.8 mwaka 2019, hitaji la kumiliki akaunti ya benki limepitwa na wakati.
Licha ya mafaniko haya yote, Kenya ingali inakabiliwa na changamoto kadhaa katika sekta ya dijitali.
Kwa mfano, udukuzi uliongezeka katika kipindi hicho ambapo Kenya ilipoteza Sh21 bilioni hapo 2017 kutokana na wizi wa wadukuzi ulioongezeka kufikia Sh29.5 mwaka wa 2018 kulingana na shirika la takwimu la Serianu.
Wizi wa taarifa za siri kupitia mitandao ya kijamii ya Facebook, WhatsApp na Instagram uliongezeka licha ya Wakenya wengi kuendelea kujiunga na majukwaa hayo.
Bei ya intaneti nchini ingali juu ikilinganishwa na mataifa jirani. Kwa mfano, kampuni ya Zantel nchini Tanzania inawapa wateja data ya 1GB kwa Sh22 kwa siku. Hapa Kenya, Safaricom inawapa wateja 1GB kwa Sh100 kila siku.
Kando na hili, gharama ya kuhifadhi data mitandaoni iko juu ajabu. Utalipa Safaricom Sh1,392 kila mwezi kuhifadhi data ya 100GB pekee. Kampuni zenye data nyingi zitalipa Sh237,000 kwa mwezi kuhifadhi data ya 20TB.
Kisiki kingine kimekuwa ukosefu wa elimu kuhusu sarafu za dijitali. Watu wengi wamepoteza hela zao baada ya kuwaamini walaghai wa mitandaoni wanaowahadaa kuwasaidia kununua Bitcoin.
Katika mwongo unaoanza 2020, ni vyema serikali iweke sera madhubuti za kukabiliana na vizingiti hivi, ili ifikapo 2030, tusiwe tunazungumzia masuala ya 2020.