• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
NGILA: Ukosefu wa ufadhili unavuruga ukuaji wa teknolojia

NGILA: Ukosefu wa ufadhili unavuruga ukuaji wa teknolojia

Na FAUSTINE NGILA

KATIKA ziara zangu kwenye vituo mbalimbali vya teknolojia humu nchini, nimebaini kuwa ukosefu wa ufadhili wa kutosha unalemaza juhudi za mamia ya vijana waliojitolea kubuni suluhu za kiteknolojia kuifaa nchi.

Nilipozuru kituo cha Sote Hub mjini Voi, niliduwaa kuona wavulana wa umri wa miaka 20 wameunda mfumo wa kipekee wa usalama huku wasichana wa umri wa miaka 17 nao wakijivunia kutengeneza teknolojia ya kukomesha uhasama baina ya binadamu na ndovu katika mbuga ya Tsavo.

Nilipowatembelea wakali wa kituo cha SwahiliBox, jijini Mombasa, nilikutana na Firdaus Salim mwenye umri wa miaka 18 ambaye huamka kila asubuhi na kusafiri kutoka Mariakani hadi Mombasa Old Town kukata kiu ya teknolojia. Yeye ni msimbaji kwa lugha ya kisasa ya Python.

Nilipofika Swahilipot Hub, nilikutana na vijana wengi ambao wanajizatiti kutimiza ndoto zao katika usimbaji, uundaji wa programu, usanii na uigizaji.

Nikiwahoji wakuu wa vituo hivi, niligundua kuwa wao hujifadhili huku wakitegemea mno wafadhili wa mataifa ya kigeni ambayo yametambua uwezo na ari yao ya kubuni suluhu kwa matatizo ya kiuchumi Pwani.

Hali ni sawa katika vituo vya Nailab cha Nairobi, Mount Kenya Hub na Dehub vya Nyeri, Ubunifu cha Machakos, Lake Hub cha Kisumu, Eldohub na Dlab Hub vya Eldoret.

iHub cha Nairobi kilichokuwa cha kwanza kupigia debe teknolojia Kenya, mwezi uliopita kililazimika kununuliwa na CcHub cha Nigeria kutokana na ukosefu wa ufadhili.

Ni aibu kubwa kwa serikali kuu na serikali za kaunti kufumbia macho mustakabali wa uchumi wa nchi. Ni fedheha kwa wasimamizi husika wa serikali kujitia hamnazo licha ya vijana kujitolea kuonyesha makali yao katika teknolojia.

Inashtua serikali haiungi mkono juhudi hizi kwa vyovyote.

Ingawa kuna Wizara ya Teknohama inayosimamia masuala yote ya teknolojia na kila kaunti kutenga fedha za kufadhili ubunifu, wapenzi wa teknolojia wametengwa, wakatekelezwa na kuachiwa mzigo wa kusaka ufadhili wao wenyewe.

Kenya inafaa kuwekeza ipasavyo katika teknolojia maanake uchumi wa usoni utategemea pakuu ubunifu.

Ingawa serikali ilipendekeza mpango wa kila eneobunge kuwa na kituo cha ubunifu hapo 2016, miaka mitatu baadaye hakuna cha kujivunia, bado serikali inajikokota.

Hili ni wazo zuri ambalo wakati wake wa kutekelezwa ni sasa, la sivyo mustakabali wa uchumi na ajira kwa jumla humu nchini utazidi kulemazwa na visiki ambavyo vinaweza kuondolewa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Shirika la Posta lahitaji uvumbuzi

ONYANGO: TSC kuwaajiri walimu vibarua si suluhu tosha

adminleo