Makala

Ng’ombe Meja alivyoteka wengi maonyesho ya kilimo Mombasa

Na FATUMA BUGU September 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAGENI wengi katika Maonyesho ya Kilimo ya Mombasa, walieleza mshangao kwa kushuhudia ng’ombe mrefu mwenye uzani wa zaidi ya kilo 1,000.

Maonyesho hayo ya siku tano, yaliyoanza Septemba 3 hadi 7, yaliwaleta pamoja zaidi ya waonyeshaji 1,000 waliovutia wageni kwa ubunifu katika sekta za kilimo, teknolojia na kilimo biashara.

Lakini ng’ombe huyo mkubwa alikuwa miongoni mwa vivutio vikuu.

Ng’ombe huyo mwenye umri wa miaka mitatu, aliyepewa jina la utani Meja, aliletwa kutoka Afrika Kusini.

Wageni walijitahidi kutafuta nafasi karibu na zizi lake, wengine wakinyanyua simu zao juu kurekodi picha na video za mnyama huyo mkubwa ajabu.

“Hii ni mara yetu ya kwanza kuleta uzao huu kwenye maonyesho. Tulitaka watu waone kwamba ng’ombe hawa wanaweza kuishi na kustawi hapa nchini pia,” alisema mlezi wake Mohamed Chibea.

Kwa mujibu wa walezi wake, Meja hulishwa mara tatu kwa siku, akila angalau kilo nane za wishwa pamoja na malisho maalum ili kudumisha misuli yake mikubwa.

Ili kumweka katika hali bora, huoshwa mara tatu kwa siku hasa msimu wa joto.

“Amevutia watu wengi sana kwenye maonyesho haya. Kila mtu alitaka kumwona kwa karibu kwa sababu ya umbo lake,” alisema mlezi mwingine, Bw Nicholas Mutuku.

Chianina ni mojawapo ya mifugo ya zamani na mikubwa zaidi duniani, kutoka Bonde la Chiana nchini Italia, ambako wamefugwa kwa zaidi ya miaka 2,000.

Hapo awali walitumiwa kama ng’ombe wa kazi na Warumi, lakini kwa sasa Chianina wanathaminiwa kwa nyama yake ya hali ya juu inayojulikana kwa kuwa laini na isiyo na mafuta mengi.

Uzani

Ng’ombe dume wakubwa wanaweza kufikia uzito wa kilo 1,700 na urefu wa mita 1.8 hadi begani, jambo linalowafanya kuwa uzao mzito na mrefu zaidi duniani.

Ngozi yao nyeupe, chini nyeusi na misuli iliyochongoka huwapa mwonekano wa kipekee.

Uzao huu pia unasifika kwa kutopata magonjwa mengi ya kawaida ya ng’ombe, kuzoea mazingira mbalimbali, na kuzalisha nyama nyingi ila huwa na mifupa na mafuta kidogo.

Sifa hizi zimewafanya kuwa maarufu Ulaya, Amerika Kaskazini na sasa wanazidi kushamiri Afrika.

Kwa wengi waliotembelea maonyesho hayo, kumwona Meja kwa macho yao kulikuwa tukio la kipekee maishani huku wengine wakimfananisha na farasi.

“Sijawahi kuona ng’ombe kama huyu maishani mwangu. Kama mtu angeleta huyu kama mahari, hii ni zaidi ya milioni, hakuna familia inayoweza kukataa kunipa mke, ni jambo la ajabu,” alisema Kevin Nyongesa, mmoja wa wageni.

Wengine walimwona Meja kama alama ya kile ambacho ufugaji wa kisasa unaweza kumaanisha kwa mustakabali wa kilimo nchini Kenya.

“Ni jambo la kushangaza, kama muujiza. Lakini pia linaonyesha kuwa ufugaji nchini mwetu unaweza kuwa na mustakabali mkubwa tukiamua kuwekeza kwa dhati. Mimi pia natamani kuwa naye shambani kwangu,” alisema John Charo, mgeni mwingine.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa Kilimo Kinachozingatia Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kilimo kwa Ukuaji Endelevu wa Uchumi.