Nguli wa Kiswahili wamzuru manju stadi Maulidi Juma
Na MISHI GONGO
WADAU katika fani ya usanii na lugha ya Kiswahili kutoka maeneo mbalimbali nchini, Jumamosi walikutana Mombasa kumuenzi gwiji wa nyimbo za taarab Maulidi Juma ambaye nyimbo zake zilivuma sana katika miaka ya ‘80 na ‘90.
Hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Swahilipot Mombasa, ilihudhuriwa na wapenzi wa Kiswahili wakiwemo waandishi wa vitabu vya Kiswahili, watunzi wa mashairi (malenga), wahadhiri na watafiti wa mila na tamaduni za Waswahili nchini.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Ustadh Wallah bin Wallah, Bw Nuhu Bakari, Lolani Kalu, Hassan Morowa, Salim Makayamba, Andrew Watuha, Thomas Koskei na wahadhiri Henry Indindi, Mathias Momanyi na mtafiti wa mila na tamaduni za Waswahili, Bi Hamira Saidi.
Maulidi Juma alikabidhiwa vyakula na bidhaa nyinginezo na mashabiki waliohudhuria.
Hafla hiyo ilifanyika baada ya runinga ya NTV kuangazia jinsi wasanii walivyotelekezwa nchini.
Waliohudhuria hafla hiyo walimsifu mutribu huyo kwa ufasaha wake wa lugha na utunzi wa mashairi ya kipekee.
Bw Maulid Juma ni mtunzi wa nyimbo kedekede za Kiswahili na lugha ya Kigiriama.
Akizungumza na ‘Taifa Jumapili’, mshairi Bw Hassan Muchai (Muchai bin Chui) ambaye ni mwandishi wa ‘Taifa Jumapili’ alisema wasanii wakongwe wamesahaulika.
“Tunapaswa kuwazika wakiwa hai, tuwaenzi wakiwa bado wako duniani. Bw Juma amekuwa na mchango mkubwa katika fani ya sanaa nchini,” alisema.
Alipendekeza serikali kuwa na taratibu za kuwatambua wasanii wakongwe.
“Kampuni ya Nation imejitolea katika kuwaenzi wasanii wakongwe nchini,” alisema.
“Wengi wa watunzi wa mashairi walijifunza kutoka kwa nyimbo za Maulidi Juma, ni wajibu wetu kama jamii kumuenzi na kumtukuza kwa mchango huo,” alieleza.
Mwandishi Wallah bin Wallah alimsifu Bw Juma kwa kuwa mtunzi wa mashairi yenye mafunzo tele.
Nyimbo za Maulidi Juma zilivuma kote nchini na mataifa mengine ya bara Afrika.
Japo kwa sasa hali ya afya ya gwiji huyo imedhoofika, bado anakumbuka baadhi ya nyimbo alizoimba.
Bi Amira Said alizitaja nyimbo za Bw Juma kuwa za kipekee na zilizotoa mafunzo kwa jamii.
“Nyimbo zake zilizungumzia maudhui mbalimbali yakiwemo mapenzi, kuishi na watu vizuri, harusi, siasa na kadhalika,” akaeleza.
Alimsifu manju huyo akisema kutokana na nyimbo zake na sauti ya kumtoa nyoka pangoni, alichaguliwa kuwatumbuiza Hayati Jomo Kenyatta na Daniel Moi katika hafla mbalimbali.
Bw Juma aliyejawa na furaha, aliwashukuru mashabiki wake huku akiwashauri wasanii wanaoinuka kuepuka vileo na dawa za kulevya.
Mzee Maulidi aliitaja Jumamosi kama mojawapo ya siku bora zaidi katika maisha yake.
Alielezea furaha yake kwa wote walioenda kumuenzi. Alitoa ushauri kwa wote waliokuwapo kukienzi Kiswahili kwa dhati kwani pamoja na kuwa ni lugha yetu ya taifa, kimewapa watu wengi riziki.
Takriban wakereketwa 100 wa Kiswahili walihudhuria hafla hiyo.
Baadhi ya nyimbo zake Mzee Maulidi ni pamoja na Sijasema naambiwa nimesema, Nimpendaye yu mbali, Hiyo isiwe ndiyo sababu, Maneno mabaya si mema miongoni mwa nyingine nyingi.