Ni miili na mauti kwa Binzaro ikihofiwa mahubiri ya ‘mwisho wa dunia’ yanaendelea
KWA zaidi ya juma moja sasa, taifa limekumbwa na jinamizi jipya lililojitokeza katika kijiji cha Kwa Binzaro, Kaunti ya Kilifi – tukio ambalo limeibua kumbukumbu mbaya za mauaji ya Shakahola, ambapo mamia ya miili ilipatikana imezikwa msituni.
Katika hali inayoonekana kuwa mwendelezo wa itikadi potovu ya kidini, wapelelezi wa mauaji tayari wamefukua miili 32 kwenye makaburi ya kina kifupi msituni humo, huku mamlaka zikihofia kuwa idadi ya waliokufa huenda ikawa kubwa zaidi.
Mwanapatholojia wa serikali, Dkt Richard Njoroge jana alisema vipande 52 vya miili vimepatikana.
Kila mwili unaochimbuliwa unaibua simanzi na mshangao. Mafuvu ya vichwa, mabaki ya mifupa na miili iliyooza imeendelea kutolewa msituni humo.
Kinachotia hofu zaidi ni kwamba baadhi ya waliotambuliwa si wakazi wa eneo hilo.
Miili hiyo ilizikwa uchi na uso ukielekea juu, hali inayoashiria ukatili wa hali ya juu, taswira ya huzuni ambayo inafufua kumbukumbu za mauaji ya Shakahola, ambayo yalitia doa picha ya Kenya kimataifa.
Serikali iliwahi kulazimika kusitisha matangazo ya moja kwa moja wakati wa uchimbaji wa miili Shakahola, Kilifi kama njia ya kulinda hadhi ya taifa.
Lakini kwa sasa, hali ya Kwa Binzaro – kilomita 30 pekee kutoka Shakahola – inazua maswali kuhusu iwapo kweli tishio hilo lilizimwa au liliahirishwa tu.
Katika baadhi ya maeneo, wanyama wa porini wameonekana kuvuruga makaburi hayo, kana kwamba hata nao hawakubaliani na unyama huu kufichwa.
Uchunguzi unaonyesha wengi wa waliopatikana wamezikwa katika msitu huo ni waathiriwa waliosalia baada ya tukio la Shakahola.
Baadhi yao walihepa msako wa polisi, wengine wakarudi eneo hilo la Pwani baada ya kukataliwa na familia na jamii zao.
Wakiwa hawana pa kwenda, walijikuta tena wakitumbukia katika mtego ule ule wa imani potovu, kufunga hadi kufa.
Maafisa wa uchunguzi wanaamini mahubiri ya mwisho wa dunia bado yanaendelea, licha ya kukamatwa kwa mhubiri Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International.
Mshukiwa mmoja aliyekamatwa, ambaye anatajwa kuwa mfuasi wa ngazi ya juu wa kundi hilo, amewapa maafisa wa uchunguzi maelezo ya kutisha.
Anadai ana taarifa kamili za vifo vya watu 49 – akieleza kuwa 33 wanatoka Migori, Siaya, Kakamega na Homa Bay, huku 16 wakiwa ni kutoka Pwani na kwingineko nchini.
Alikiri kuwa baadhi ya vifo vilikuwa tayari vimeanza kabla hajajiunga na kundi hilo msituni, hali inayoongeza hofu kuwa huenda waliokufa ni wengi zaidi.
Polisi wamebaini kuwa wengi wa washukiwa 11 walioko rumande kwa sasa, wana uhusiano wa moja kwa moja na mauaji ya Shakahola.
Inaaminika kuwa baada ya Shakahola kusambaratishwa, kundi hili lilijipanga upya kimyakimya na kuendeleza mafundisho ya Mackenzie.
Kesi iliyowasilishwa mahakamani Malindi inataja majina ya watu wanne waliotembea nchi nzima wakirai wafuasi wa Mackenzie kujiunga na imani hiyo na kufunga hadi kufa.
Cha kushangaza ni kuwa hakuna hata familia moja kutoka Kwa Binzaro wala vijiji jirani iliyotangaza kupoteza jamaa.
Kwa mujibu wa sensa, kijiji cha Kwa Binzaro kina wakazi 591 pekee, na hakuna ripoti yoyote ya mtu kupotea kutoka Makongeni, Mkondoni, Sosobora, Ndigiria Mriqchagwe, Matolini au Kisiki.
“Hatuna ripoti yoyote ya watu kupotea hapa. Familia zote ziko salama,” alisema mkazi mmoja aliyekataa kutajwa jina.
Julius Hare, kiongozi wa Nyumba Kumi katika eneo hilo, alisema kuwa jamii imebaki na mshangao mkubwa baada ya ugunduzi wa maiti hizo.
Matukio haya ya Kwa Binzaro yameibua hofu mpya kuwa huenda Kenya inashuhudia mwendelezo wa mauaji ya kimfumo kupitia itikadi za kidini potovu.
Wito kwa serikali ni kuchukua hatua ya haraka, si tu kuchunguza, bali kuzuia kundi hili kuendelea kuvutia waumini na kueneza ajenda yao ya kifo.
“Kwa sasa, ufukuaji huu wa miili umeathiri shughuli zetu za kila siku. Tunategemea msitu huu kwa mambo mengi, ikiwemo kuni na makaa tunayotumia na pia kuuza ili kujipatia kipato,” anaeleza.
Anasema kuwa wakazi wote wa eneo hilo wako salama, lakini ana wasiwasi kuwa shughuli za kidini zinazofichuliwa zinaweza kuwa na athari mbaya kwa vijana wa eneo hilo.
Gladys Kadzo, mkazi wa muda mrefu wa kijiji cha Kwa Binzaro tangu mwaka wa 1992, pia anaufahamu msitu huu kwa kina. Kwa miongo kadhaa, yeye na mumewe waliendesha shughuli za kuchoma makaa katika eneo hilo.
“Naufahamu msitu huu toka mwanzo hadi mwisho. Nimetumia sehemu kubwa ya maisha yangu hapa. Nilikuwa nachoma makaa na mume wangu, lakini sasa ni mzee sana na dhaifu kuweza kutembea kama zamani,” anasema.
Bi Kadzo anaeleza kuwa hajawahi kusikia ripoti zozote kuhusu watu kupotea au mazishi kufanyika msituni. Hata hivyo, anakumbuka kuwa aliwahi kuona kibanda kilichoezekwa kwa nyasi kikiwa ndani kabisa ya msitu.
“Mtu aliyekuwa akiishi pale aliondoka kabla tukio hili halijafichuliwa,” anasema, na kuongeza kuwa alishangazwa sana na taarifa za ufukuaji wa miili.
“Msitu huu ni mkubwa mno. Huwezi kujua kinachoendelea kila sehemu kwa wakati mmoja.”