Makala

Ni mkosi au sadfa? Wanafunzi walioathiriwa na Covid-19 sasa waathiriwa na mafuriko

May 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

JE, ni mkosi wa aina fulani ama sadfa ya kimatukio?

Hilo ndilo swali linalowaandama wanafunzi wengi wa Kidato cha Nne nchini, baada ya Rais William Ruto kuahirisha tarehe ya shule kufunguliwa kwa muda usiojulikana.

Kwenye hotuba aliyotoa moja kwa moja kwa Wakenya kutoka Ikulu ya Nairobi, Ijumaa, Rais Ruto alitangaza kuahirisha tarehe ya wanafunzi kufungua shule kutoka Mei 6 hadi siku isiyojulikana.

Rais alitaja hali hiyo kuchangiwa na mafuriko ambayo yamekuwa yakiendelea katika sehemu tofauti nchini.

Hapo awali, shule zote zilikuwa zimepangiwa kufunguliwa Aprili 29, lakini tarehe hiyo ikaahirishwa hadi Mei 6 na Waziri wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu.

Katika hatua hizo zote, wanafunzi wanaoonekana kuathiriwa sana ni wale walio katika Kidato cha Nne, kwani huu ndio mwaka wao wa mwisho katika shule za upili.

Kinaya ni kuwa, wanafunzi wao hao ndio walioathiriwa na hatua ya serikali kusimamisha masomo kwa karibu mwaka mmoja mnamo 2020, kutokana na janga la virusi vya corona.

Wakati huo, wanafunzi hao walikuwa katika Darasa la Nane.

Katika hatua ya kuwazuia wanafunzi kuathiriwa na maradhi hayo, aliyekuwa Waziri wa Elimu, marehemu Prof George Magoha, alisimamisha shughuli zote za masomo kwa muda wa miezi tisa ili kudhibiti maenezi ya virusi hivyo hatari.

Kulingana na wanafunzi kadhaa waliozungumza na Taifa Dijitali katika eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, hata wao wameachwa kwenye mshangao kuhusu ikiwa mwelekeo huo ni mkosi au sadfa ya matukio.

“Mbona sisi ndio tunaoathirika kila mara na majanga yanayotokea? Kwa kweli, niko katika hali ya mshangao. Pengine hili ni fumbo ambalo mwanadamu hana jibu lake halisi,” akasema Brenda Mwikali, ambaye ni mwanafunzi katika shule moja ya kibinafsi katika kaunti hiyo.

Ijapokuwa wengi wao walionekana kuunga mkono hatua ya serikali kuchukua hatua hiyo, walisema inafaa kuwaruhusu kurejea shuleni mara moja, baada ya kiwango cha mafuriko kupungua.

“Bila shaka, hii ni hatua nzuri, japo serikali inafaa kuturuhusu kurejelea masomo mara tu hali itakapokuwa shwari,” akaeleza mwanafunzi ambaye hakutaka kutajwa.