• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
‘Ni muhimu kuwa mwangalifu unapopiga selfie’

‘Ni muhimu kuwa mwangalifu unapopiga selfie’

Na SAMMY WAWERU

MITANDAO ya kijamii kama Facebook, Instagram, na WhatsApp imesheheni picha zilizopakiwa na watumiaji wake.

Wengi hasa huchapisha ama kuonyesha maeneo walikozuru, wanachofanya au hata hali wanayopitia.

Katika pilkapilka za kusafiri, hafla ya harusi, maeneo ya burudani na sebuleni, ni miongoni mwa yanayoongeza kwa picha zinazopakiwa.

Mbali na kutaka kuonekana, lengo lingine la watumiaji wa mitandao wenye uraibu huo ni kupokea maoni ya wachangiaji na picha zao kupata alama ya kupendwa.

Hakuna kinachowafurahisha kama kuona wanapata ufuataji mkubwa mitandaoni na kumiminiwa sifa.

Hata hivyo, unapojipiga picha kwa simu, maarufu kama ‘selfie’ unatakiwa kuwa makini unapotekelezea shughuli hiyo. Wengi huonekana kuchangamka angaa picha ionekane ya kuvutia.

Sababu hasa ya himizo la kuwa makini, baadhi ya maeneo kama vile barabara, mito na bahari si salama. Taarifa ya wanandoa wachanga na jamaa wao watatu waliozama majini katika jimbo la Tamil Nadu, Kusini mwa India, wakati wakijipiga selfie, inaendelea kusambaa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Inasemekana walizama majini wakijaribu kupiga picha wakiwa wameshikana mikono karibu na bwawa. Aidha, mmoja wao aliteleza huku akiwa amewavuta wenzake.

Mei 2019, nchini India watu watatu waliripotiwa kufariki baada ya kupigwa dafrau na garimoshi wakati wakipiga selfie.

Inadaiwa visa vya watu kufariki wakipiga selfie nchini humo vimekita mizizi.

Hapa nchini Kenya, Desemba 2017 mwanamume mwenye umri wa miaka 24 aliripotiwa kufa maji katika Mto Molo wakati akipiga selfie. Vyombo vya habari viliarifiwa kuwa Elvis Keter aliteleza, akiwa na wenzake watatu.

“Kama idara ya usalama tunashauri vijana, wengi wakiwa ndio waathiriwa wawe waangalifu ni wapi wanapigia picha. Kwa mfano, kwenye mto, dimbwi, au bahari, wahakikishe wameandamana na wataalamu wa kuogelea,” ashauri Charles Gathogo, afisa wa usalama.

Pia, ni muhimu wanapoingia maeneo ya kujivinjari yenye vidimbwi vya kuogelea, mito, bahari au mbuga za wanyama, wawe na idhini kutoka kwa asasi husika ili tukio linapojiri wataweza kuokolewa.

  • Tags

You can share this post!

Rwanda yapiga hatua kuu kiteknolojia kutengeneza...

Aliyekiri mauaji ya wakili alivyofichua eneo la tukio

adminleo