Ni muhimu watoto kuruhusiwa kushiriki michezo
Na MISHI GONGO
MICHEZO ni kiungo muhimu katika ukuaji na uimarikaji wa mtoto katika nyanja mbalimbali.
Michezo huchangia katika ukuaji wa akili, mawazo, kuwafanya watoto kuwa na uwezo wa kutatua mizozo baina yao na hata kuwapa ujuzi wa kutangamana na watu wengine.
Zamani watoto wakishiriki michezo mengi iliyohusisha wao kukimbia, kurukaruka na kadhalika.
Mifano ya michezo iliyochezwa na watoto wa miaka ya tisini hadi 2000 ni kama mpira wa kulengana kwa wasichana, kupika, kuruka blada, uku na mingineyo huku wavulana wakicheza mpira wa miguu, michezo ya kutengeneza magari, kujenga nyumba, kuigiza taaluma mbalimbali ,kulenga shabaha, kuogelea na kadhalika.
Michezo hiyo iliwawezesha watoto kunyoosha viungo vyao na kuwa wachangamfu.
Hata hivyo, michezo hiyo kwa sasa imepotea mijini ambapo watoto wengi kwa sasa wanapendelea kuchezea simu aina ya smartphone, michezo ya kudhibitiwa na rimokonto au kuangalia sinema katika runinga.
Kulingana na utafiti uliofanywa hivi majuzi na shirika la utafiti la watoto Mudorch, ni kwamba watoto kuangalia runinga au kipakatalisha kwa zaidi ya muda wa saa moja kwa siku kunawaathiri akili zao na pia kupunguza uwezo wao wa kukumbuka vitu.
Utafiti uliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2019 ulipendekeza watoto kuanzia umri wa miaka miwili hadi mitano kuangalia televisheni kwa saa moja kwa siku huku wale wa chini ya umri wa miaka miwili ikipendekezwa kutoruhusiwa kuangalia runinga.
Aidha mtoto kuangalia televisheni kwa muda mrefu pia kumehusishwa na watoto kupata athari za kiafya kama kuwa wazito kupindukia na kufanya vibaya katika masomo yao.
Bi Dolicate Oloo mwalimu mkuu katika shule ya mmiliki binafsi ya Skyways alisema kuwa ni muhimu kwa watoto kucheza michezo ya kurukaruka.
Alisema watoto wanaofaulu zaidi darasani ni wale walio wachangamfu uwanjani.
“Katika shule yetu tunawahimiza watoto kucheza. Mara kwa mara tunaandaa warsha za michezo ambazo tunawahusisha wazazi na watoto wao. Hili pia husaidia wazazi na watoto kuwa na uhusiano mwema,” akasema.