Ni soja usiku, mchana mwanafunzi
NYAKATI za mchana, utamkuta Samson Metiaki Sarinke akiwa katika pilikapilika za kuhama ukumbi mmoja wa mhadhara hadi mwingine katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), Nairobi.
Lakini jua likizama, mwanafunzi huyu wa kitivo cha mawasiliano na elimu ya vyombo vya habari, hugeuka na kujigubika magwanda ya mlinzi wa usiku chuoni humo.
“Maneno pekee hayawezi kueleza jinsi maisha yangu yalivyo magumu,” anakumbuka Samson, akiangazia safari ya maisha yake iliyojaa pandashuka.
“Nilikiuka milima ya vizuizi ili kufika nilipo.”
Kwa mwanarika huyu mwenye umri wa miaka 28, ndoto ya kupata elimu ya juu ilisitishwa kwa muda wakati matatizo ya kifedha yalipomlazimisha kuonyesha chuo mgongo katika mwaka wake wa pili 2018.
Hapo ndipo aliamua kuselelea maeneo ya Bonde la Ufa kufanya kazi za sulubu ili kujikimu kimaisha na kujaza kibaba kwa akiba mwishowe ajiondolee kero ya karo.
Bila kuchoka, alivuka mipaka ya Kenya kuingia Uganda na kurejea mara kwa mara katika harakati ya kutimiza ndoto yake.
Alikuwa taniboi wa malori yaliyosafirisha mahindi na mazao mbalimbali ya shambani.
“Nilisafirisha mahindi kati ya Pokot Magharibi, Turkana na maeneo ya Uganda na kila safari ilinipa angalau Sh1,000,” alifichua.
Kurejea shuleni
Lakini, katika pandashuka za usakatonge, akilini mwake Samson mlijaa mikakati thabiti ya kurejea chuoni.
Akitambaliwa na azimio lisiloyumbayumba, alirejelea uanachuo mwaka wa 2021, ila wakati huu akiwa na uthabiti na ukomavu.
“Haikuwa rahisi kwangu kurejelea maisha ya kawaida ya mwanafunzi,” anakiri Samson, sauti yake ikisheheni utulivu.
“Lakini nilijua elimu kwangu ni kipaumbele,” anaongeza.
Akiwa na kiu kubwa ya kufaulu, Samson alitafuta fursa ambazo zingemruhusu kusawazisha shughuli zake za masomo na mahitaji ya maisha ya kila siku.
Malengo yake yalimpeleka katika taasisi ya Lavington Security Limited, ambako alipokea mafunzo ya kuwa mlinzi kabla ya kuanza kazi ya askari wa usiku katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Anachapa kazi hii kwa sasa jua likitua na kuingia darasani jua likichomoza.
“Ndani ya sare hii ya mlinzi kuna mtu mwenye talanta nyingi na matarajio,” Samson alijitapa akibingirisha fimbo aliyoshika kwenye beji kifuani.
“Mimi ni mwandishi wa habari, mwanamuziki, na pengine mwanajeshi siku za usoni.”
Samson aliambia Akilimali Dijitali kuwa kazi yake huchangia hadi asilimia 50 ya karo huku akipigwa jeki na familia.
Licha ya hatua hii, haijakuwa rahisi kwake kwani mara kadhaa ameahirisha elimu ili kukusanya fedha kujaza nakisi ya kila muhula.
“Wenzangu wengi wamehitimu, lakini mimi nimelazimika kuvumilia. Kuna mwanga wa matumaini kwa sababu safari hii inakaribia mwisho wake,” mwanafunzi huyu wa mwaka wa nne alisema kwa ujasiri.