Nilivyomjua Sajini Nyawira: Mwanajeshi huyo mpiga picha alikuwa kipenzi cha wanahabari
NA KALUME KAZUNGU
“KALUME Kazungu, uko wapi? Bado dakika chache tuondoke wajua. Fanya hima.”
Hayo mara nyingi ndiyo yaliyokuwa matamshi ya Sajini Roselyne Nyawira wakati akinihimiza kuharakisha kufika, iwe ni kwenye uwanja mdogo wa ndege wa Mokowe kuabiri helikopta yao kuelekea msitu wa Boni, ama kwenye uwanja wa Ndege wa Manda, hasa punde kunapokuwa na hafla maalumu inayohusu wanajeshi wa Ulinzi Kenya (KDF) na inayofaa kuangaziwa kwa vyombo vya habari.
Kwa muda mfupi niliomfahamu Sajini Nyawira, alikuwa afisa mpole, mtulivu na aliyeitekeleza kazi yake kwa uangalifu mno.
Licha ya kuwa mchache au mfupi wa maneno, moyo wake safi ulidhihirishwa wazi na tabasamu iliyokuwepo kila mara kwenye uso wake.
Kila mara nilipokutana au kutagusana na Bi Nyawira katika kazi yangu ya uanahabari, nilimpata akiwa amebeba kamera yake begani au akipiga picha maafisa wenzake wa KDF kwenye shughuli zao za kila siku.
Sajini Nyawira alikuwa miongoni mwa maafisa wa Kitengo cha Mikakati ya Mawasiliano na Uhusiano Mwema Jeshini-yaani KDF Strategic Communications.
Ni kupitia jukumu alilotekeleza ambapo aliifanya kazi ya waandishi habari Lamu kuwa rahisi kwani alihakikisha kuna mtagusano na muingiliano bora kati yetu sisi wanahabari na wanajeshi wanaoendeleza operesheni ya usalama kwenye msitu mkuu wa Boni.
Ni kupitia mazingira mema ya kikazi aliyounda Sajini Nyawira ambao uliniwezesha mimi binafsi kama mwanahabari kujenga urafiki na maafisa wengi wa KDF, wakubwa kwa wadogo, hasa wale wanaohudumu Kaunti ya Lamu.
“Kalume, wajua lazima tushirikiane katika hizi kazi zetu ndipo tuweze kuilinda na kuijenga nchi yetu. Kenya ni yetu sote na majukumu yetu yanahitajika tuyatekeleze kwa uwajibikaji mwingi,” akasema Bi Nyawira.
Kuzuru vijiji vya Mararani ndani ya msitu wa Boni
Ninakumbuka vyema Januari 26, 2023, ambapo kupitia juhudi za Sajini Nyawira na wenzake, waandishi wa habari wa Lamu waliweza kuzuru vijiji vya Mararani na Mangai, ndani ya msitu wa Boni, Lamu Mashariki.
Ikumbukwe kuwa msitu huo umekuwa ngome kuu ya Al-Shabaab kutekeleza mashambulio na mauaji ya wakazi na walinda usalama kwenye sehemu tofautitofauti za Lamu.
Hii inamaanisha kuwa kuufikia msitu huo na hata kuzuru vijiji vilivyoko ndani lazima kupata usaidizi, ushauri na idhini ya maafisa wa usalama, ikiwemo KDF.
Ziara hiyo ya wanahabari, ambayo pia ilishirikisha maafisa wengine wakuu wa KDF, ikiwemo Meja-Jenerali Juma Mwinyikai, ilinuia kutathmini hali ya usalama msituni Boni wakati ambapo Operesheni ya Usalama ya Amani Boni (OAB) inaendelea kutekelezwa na vitengo mbalimbali vya usalama.
Operesheni hiyo ilizinduliwa na serikali kuu mnamo Septemba, 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.
Jukumu la wanahabari siku hiyo lilikuwa kutathmini na kupata matukio ya hali ilivyo sasa, ikiwemo kuwauliza wananchi wa jamii ya walio wachache ya Waboni kuhusiana na hali ya usalama na maendeleo yalivyo tangu serikali ilipozindua operesheni hiyo.
Miongoni mwa shughuli nyingine zilizonitangamanisha na Sajini Nyawira ni ile ya Januari 30, 2023 wakati maafisa wa KDF walipokuwa wakiwapeperusha kwa ndege walimu karibu 30 waliofaa kuhudumia shule tano za msitu wa Boni.
Walimu hao walisafirishwa kutoka uwanja wa ndege wa Mokowe, taarifa ambayo pia niliipeperusha au kuiangazia kwenye gazeti la Taifa Leo na lile la Daily Nation.
Mara ya mwisho kutagusana na Sajini Nyawira ilikuwa Februari 8 mwaka huo huo wa 2023, ambapo nilikuwa nikiangazia taarifa ya maafisa wa KDF kuwasaidia wanafunzi watatu werevu na wenye uhitaji wa Lamu, ambapo waliwafadhili kwa kuwasafirisha kwa helikopta yao kutoka uwanja wa ndege wa Manda, kaunti ya Lamu hadi Nairobi walikofaa kujiunga na Shule ya Upili ya Kijeshi ya Moi Forces Academy.
Mshtuko mkubwa kwa wanahabari
Aidha kifo cha ghafla cha Sajini Nyawira kimepokelewa kwa mshtuko mkubwa, si kwangu pekee kama Kalume Kazungu, bali pia miongoni mwa wanahabari wengine wengi waliomfahamu afisa huyo aliyejenga urafiki na wengi.
Sajini Nyawira ni miongoni mwa maafisa wa KDF walioangamia kwenye ajali ya helikopta ya jeshi iliyoanguka na kulipuka eneo la Elgeyo Marakwet Alhamisi mchana.
Katika mahojiano na Taifa Dijitali Ijumaa, Msemaji wa KDF, Brigedia Zipporah Kioko alitaja ajali hiyo ya ndege na maafa yaliyotokea kuwa pigo kubwa.
“Ni wakati mgumu kwetu sote. Namuomba Mwenyezi Mungu awakubali wenzangu wote walioangamia kwenye ajali mbinguni. Pia azifariji familia zote zilizopoteza wapendwa wao kwenye mkasa wa ajali ya helikopta jana,” akasema Brigedia Kioko.
Ajali hiyo pia ilipelekea kifo cha Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Francis Ogolla, hivyo kuitumbukiza Kenya kwenye hali ya majonzi na maombolezo.
Mbali na Jenerali Ogolla na Sajini Nyawira, maafisa wengine wa jeshi walioangamia kwenye ajali hiyo mbaya ni Brigedia Swale Saidi, Kanali Duncan Keittany, Luteni Kanali David Sawe, Meja George Benson Magondu, Kapteni Sora Mohamed, Kapteni Hillary Litali, Sajini Mkuu John Kinyua Mureithi na Sajini Cliphonce Omondi.
Rais William Ruto tayari ametangaza siku tatu mfululizo za kuwaomboleza maafisa hao wa jeshi huku akiamuru bendera kupeperushwa nusu mlingoni.
Mungu azilaze roho za maafisa wetu wa jeshi, ikiwemo Jenerali Ogolla na Sajini Nyawira, mahali pema peponi.