Makala

Nimemaliza PhD na sasa nitaoa, mbunge afichua sababu

Na ELVIS ONDIEKI September 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Keiyo Kusini, Gideon Kimaiyo, amekiri kuwa aliapa kutooa hadi atakapomaliza shahada ya uzamifu (PhD).

Mbunge huyo alisema kuwa alijiwekea ahadi hiyo akiwa kijana.

Mnamo Septemba 20 2024, mbunge huyo mwenye umri wa miaka 37 alitimiza ndoto yake na kuhitimu na Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Masuala ya Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Hii anasema sasa inampa ‘ruhusa’ ya kuoa.

“Ndio, nimetimiza ndoto yangu na sasa niko huru kuoa hata kama ni hiyo Ijumaa jioni baada ya kumaliza sherehe ya kuhitimu,” alijibu kwa utani huku akicheka.

“Nilipoingia kwenye siasa, watu walisema singechaguliwa kwa sababu sikuwa nimeoa; kwamba ninapaswa kumtafuta mtu na kufanya harusi ya haraka. Nikasema ‘Hapana’.”

Ili kuthibitisha jinsi alivyo na msimamo thabiti, anasema hakutahiriwa hadi alipomaliza sekondari.

Wakati wavulana wenzake wakitahiriwa, yeye alifanya hivyo baadaye sana.

Hii haikuwa bila changamoto, kwani mara nyingi watu walimbandika majina.

Aliamua kuchelewesha tohara kwa sababu hakutaka kufuata njia ya kawaida kama wavulana katika eneo lake.

Sababu yake ilikuwa kwamba haitamkomboa kutoka kwenye umaskini uliokithiri ambao familia yake ilikuwa ikiishi.

Akiwa wa sita kati ya watoto tisa, alitoka kwenye familia iliyokuwa ikiuza pombe, na kulikuwa na siku nyingi aliporudi nyumbani na kukuta watu wakifurahia kileo lakini hakuna chakula, kwa sababu wazazi walikuwa na shughuli nyingi na hawakufikiria kuhusu kuwaandalia chakula.

“Unakuta kuwa baadhi ya wavulana wanapopitia tohara, wanaanza kunywa pombe kisha kuoa wakiwa na umri mdogo. Nilijiwekea ahadi ya kuepuka haya.”

“Iwapo singechagua njia tofauti, ningekuwa nimeoa na labda kuwa na watoto saba, kwa sababu vijana wa rika langu kijijini wako hivyo, wakihangaika na maisha,” akaongeza.

Kando na hayo, mbunge huyo alieleza changamoto alizokumbana nazo wakati wa masomo yake.

Anaeleza kuwa babake alikuwa akimlipia karo kwa kupeleka maziwa shuleni.

Hii ilikuwa katika Sekondari ya Kutwa ya Kiptulos.

“Ada zangu zililipwa kupitia maziwa ambayo baba yangu alikuwa akipeleka kila siku shuleni,” anasema. “Ilikuwa inatumika kutengeneza chai shuleni.”

Alifanya mtihani wake wa KCSE mwaka 2004 na akapata alama ya B. Alikuwa anahitaji B+ ili kujiunga na chuo kikuu.

Hata hivyo, anasema kuwa alifunza katika shule ya Msingi ya Kaptarkok kwa miaka miwili wazazi wake wakitafuta karo.

Mnamo Septemba 2006, alijiunga na Chuo cha Utalii.

Alipitia changamoto kadhaa akiwa shuleni na wazazi wake wakalazimika kuuza shamba ili aweze kuendelea na masomo yake.

Imetafsiriwa na Winnie Onyando