• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
NJEHU: Kenya isishiriki mikataba yoyote hatari kwa mazingira yake

NJEHU: Kenya isishiriki mikataba yoyote hatari kwa mazingira yake

Na FREDRICK NJEHU

KENYA na Amerika zimezindua awamu ya pili ya mazungumzo ya kibiashara, siku chache tu baada ya kinyang’anyiro cha uchaguzi nchini humo.

Amerika haijatia sahihi mikataba kama ile ya Basel na ya Paris ambayo inadhibiti usafirishaji wa taka za plastiki na udhibiti wa hali ya anga mtawalia.

Ukosefu wa Amerika kuonyesha uongozi katika mikataba hii ya kimataifa ni dhahiri kwamba watakapoenda katika mazungumzo hayo, watatumia mbinu kuwashawishi wenzao wa Kenya kulegeza misimamo yao na sheria zao kuhusiana na masuala ya kimazingira.

Nchi za kanda ya Afrika Mashariki ambazo zimekuwa zikiweka mikakati ya kuungana kiuchumi na kibiashara zimegadhabishwa sana na mashauriano haya.

Suala hili la usafirishaji taka limezua tumbo joto kwa wakazi wa bara la Afrika, na kulingana na ripoti kwenye mitandao ya kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari, mazungumzo haya huenda yakadhalilisha sheria za kimazingira kama udhibiti wa plastiki ambazo Kenya na nchi zingine za Afrika zimepitisha.

Mpangilio huu unaashiria kutumia mazungumzo haya kama mbinu ya kuhakikisha kwamba kampuni hizi zinaweza kufungua soko la bidhaa hizi kwa njia tofauti.

Njia ya kwanza ni kuhakikisha kwamba Kenya inafungua uwekezaji wa viwanda hivi kwa muundo, mbinu ambayo inatoa vikwazo vilivyowekwa kuzuia bidhaa za plastiki.

Vikwazo vingine ambavyo vinaweza kuzuia wawekezaji ni ushuru unaolipiwa bidhaa za kemikali na plastiki. Ushuru huu ambao uko kwa kiwango cha juu umewekwa kuhakikisha kwamba wawekezaji wa nchi za kigeni waweze kutumia sarafu za kigeni.

Mbinu nyingine ni kutumia vipengele vya kisheria ambavyo vinaruhusu nchi kufungua mipaka kwa bidhaa za Amerika ni kutoza ushuru. Mbinu ya tatu, ni kutumia uwekezaji wa kibiashara ili kuruhusu wawekezaji wa kampuni hizi kuweka viwanda katika bara la Afrika.

Hata hivyo, jambo la muhimu linalofaa kuzingatiwa ni sera ambazo Kenya na nchi zingine 34 zimeweka kudhibiti mifuko na bidhaa za plastiki ambazo zimeathiri mazingira hasa mito, maziwa, kwenye miji na vitongoji vinginevyo.

Ili kukabiliana na changamoto hii, shirika la Greenpeace limekuwa katika mstari wa mbele kuhimiza wizara husika ya biashara na viwanda kuchukua hatua dhabiti na kuhimiza Amerika kuondoa vipengele hivi ambavyo vinaweza kushusha hadhi ya kimazingira nchini Kenya na bara la Afrika.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mja akifuata taratibu za toba, Allah...

Mawaziri walio na ndimi telezi